UINGEREZA YAONDOA VIKWAZO VYA MAFUTA YA URUSI

Kupanda kwa bei ya mafuta duniani kumeilazimu Serikali ya Uingereza kuondoa baadhi ya vikwazo dhidi ya mafuta ya Urusi, huku hofu ya upungufu wa nishati ikiongezeka kutokana na mvutano wa vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.

Hatua hiyo iliyoanza kutekelezwa leo pia imehusisha kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya usafirishaji wa gesi ya asili ya Urusi iliyoyeyushwa (LNG), katika juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa mafuta na gesi unaendelea kuwa wa uhakika nchini humo.

Mabadiliko hayo yanatajwa kuchochewa na athari za kuzuiwa kwa usafiri wa meli katika Mlango Bahari wa Hormuz, eneo muhimu kwa usafirishaji wa mafuta duniani, tangu kuanza kwa vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Hatua kama hiyo iliyochukuliwa na Marekani hivi karibuni ilikumbana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa baadhi ya washirika wake wa kisiasa na wanaharakati wa haki za kimataifa.

Wakati huo huo, bei za mafuta ya ndege barani Ulaya zimeongezeka maradufu tangu kuanza kwa vita hivyo, huku bei ya mafuta katika vituo vya mafuta nazo zikipanda kwa kasi.

Kutokana na hali hiyo, mashirika kadhaa ya ndege nchini Uingereza na maeneo mengine duniani yameahirisha safari baadhi ya safari zao na kuongeza gharama za tiketi ili kukabiliana na ongezeko la gharama za mafuta ya ndege.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here