Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha elimu ya upandaji miti inatolewa kwa wanachi hususan wale wa vijijini ili waweze kushiriki vizuri katika biashara ya kaboni.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Dkt. Festo Dugange wakati akijibu maswali kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais bungeni jijini Dodoma leo Aprili 30, 2026.
Katika swali lake Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Maryam Azan Mwinyi alitaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ya upandaji miti ili wananchi hasa wale wa vijijini washiriki katika biashara ya kaboni.
Akijibu swali hilo, Dkt. Dugange amefafanua kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeendelea kutekeleza kampeni za upandaji miti katika halmashauri zote nchini, huku akiongeza kuwa vimeratibiwa vipindi vya redio na televisheni ikiwemo kipindi cha “Mazingira yetu na Tanzania Tuitakayo” kinachorushwa kila Jumatatu kupitia TBC ambapo elimu ya upandaji miti na biashara ya kaboni hutolewa.
Sambamba na hayo Dkt. Dugange ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa TFS kila kanda kusambaza miche kwa wananchi kwa ajili ya kuipanda katika maeneo yao na kuitunza, hatua itakayosaidia uhifadhi wa mazingira kuwa endelevu.
Hatahivyo Dkt. Dugange ameeleza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea kuwajengea uwezo maafisa mazingira katika ngazi ya Serikali za Mitaa kuhusu umuhimu wa upandaji miti na fursa ya biashara ya kaboni ili kuhakikisha wananchi wote wanashiriki katika biashara hiyo.






