Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga, amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya watumishi wote waliohusika na hoja 14 zilizobainika katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’.
Mhe. Sendiga alitoa agizo hilo wakati wa kikao cha kujadili taarifa ya CAG kuhusu Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’.
Katika kikao hicho, alisisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza uwezo wa halmashauri kugharamia miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ kwa kupata Hati Safi kwa miaka mitatu mfululizo, huku akiwataka viongozi na watumishi kuendelea kusimamia matumizi ya fedha za umma kwa uwajibikaji, uadilifu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
Vilevile, Mhe. Sendiga aliwapongeza viongozi, madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo kwa ushirikiano wao, akiwahimiza kuendelea kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya Mkoa wa Manyara.







