JERUSALEM, Palestina
NI katika kambi za raia wa Palestina wanaoishi kwenye mahema baada ya makazi yao kusambaratishwa na mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Mbali ya changamoto lukuki zinazowaandama katika makazi hayo duni, kubwa na ya kuogopesha ni hii ya panya na nguchiro kung’ata watoto.
Samah al-Daabla, mmoja ya wanaoishi kwenye kambi, anasimulia namna wadudu hao walivyomng’ata mkono mtoto wake mwenye umri wa miaka minne. Anasema:
“Ilikuwa saa 8 usiku, ambapo tulishitushwa na kelele za mtoto wetu aitwaye Mayaseen. Mume wangu alipowasha tochi, nguchiro alikimbia. Nilipomtazama mtoto, mkono wake ulikuwa unavuja damu. Damu zilitapakaa kila sehemu.”
Mayaseen alipatiwa matibabu, ikiwamo kuchomwa sindano ya kinga ya ‘tetanus’ lakini ametumia siku kadhaa akisumbuliwa na homa na kutapika.
Hii haijaishia kwa Mayaseen tu. Video fupi zilizosambaa mitandaoni zimeonesha panya, nguchiro na wadudu wengine wakizunguka huku na kule kwenye kambi zinazohifadhi raia wasio na makazi katika eneo hilo la Ukanda wa Gaza.
Si tu kusababisha usumbufu, bali pia wamekuwa wakiwang’ata watoto wachanga, wagonjwa na wazee wanaoishi kambini hapo.
Ni kama anavyosimulia Rizq Abu Laila, ambaye anaishi kambini akiwa na familia yake ya watoto wanne, akiwamo mmoja mwenye ugonjwa wa saratani. Anasema:
“Hatuwezi kulala. Tukilala, (panya na nguchiro) wanawang’ata watoto na kutusumbua. Kuna panya na nguchiro wengi sana. Naapa, hatuwezi kuvumilia.
“Panya wametafuna nguo zetu na wanakula unga tulionao kwa ajili ya chakula. Mbu ni wengi sana, harufu nayo ni mbaya. Tunaomba jumuhiya za kimataifa zitusaidie.”
Aidha, mmoja ya wazee, licha ya kuwa na kidonda cha muda mrefu kutokana na ugonjwa wa kisukari, ameeleza pia kung’atwa kidole na nguchiro.
Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa (UN) imeeleza kuwa wadudu aina ya panya na nguchiro wanapatikana katika asilimia 80 ya kambi za Gaza na kutesa watu milioni 1.45.
Wanapong’ata husababisha magonjwa mbalimbali, yakiwamo ya ngozi, upumuaji, damu na hata kutia sumu kwenye vyakula.
Mwakilishi wa Shirika la Afya la Kimataifa (WHO) nchini Palestina, Dkt. Reinhilde Van De Weert, amesema asilimia kubwa ya magonjwa katika kambi yanatokana na mazingira mabaya wanayoishi.






