MANCHESTER, Uingereza
HILO ndilo swali wanalojiuliza mashabiki na hata viongozi wa Manchester City kwa sasa. Maisha yatakuwaje baada ya Pep Guardiola kuondoka mwishoni mwa msimu huu wa 2025-26?
Guardiola, raia wa Hispania mwenye umri wa miaka 54, hajathibitisha wala kukanusha taarifa zinazodai kuwa ataachia ngazi majira ya kiangazi laini tayari Man City imeanza kuhusishwa na kocha wa zamani wa Chelsea, Enzo Maresca.
Kuondoka kwa wachezaji waandamizi, Kevin de Bruyne, Kyle Walker na Ederson kunaweza kutoa picha ya kumalizika kwa zama za Guardiola katika klabu hiyo.
Pia, aliyekuwa Mkurugenzi wa Michezo kwa miaka mingi, Txiki Begiristain, na nafasi yake kuchukuliwa na Hugo Viana, kunatoa picha ya mabadiliko makubwa.
Swali ni je, Man City itaweza kuzipiku klabu zingine kubwa na kuwavutia wachezaji bora katika soko la usajili bila uwepo wa Guardiola?
Wakati wa usajili wa dirisha dogo la Januari, 2026, Man City iliwasajili wachezaji wawili waliokuwa gumzo sokoni, Antoine Semenyo na Marc Guehi.
Semenyo aliichagua Man City, licha ya kutakiwa Manchester United, Chelsea, Tottenham na Liverpool. Guehi naye alitua Etihad wakati huo akiwa na ofa za Liverpool, Tottenham, Arsenal, Bayern Munich, Inter Milan na Atletico Madrid.
Je, City itakuwa na ushawishi huo baada ya Guardiola kuwa nje ya benchi la ufundi na klabu kwa ujumla?
Maresca, kama ilivyoelezwa awali, anatajwa zaidi katika orodha ya makocha wanaopigiwa hesabu na mabosi wa Man City.
Alikuwa kocha wakati Leicester City ikipanda Daraja mwaka 2024. Aliiwezesha Chelsea kurejea Ligi ya Mabingwa Ulaya, pia akiipa mataji ya Conference League na Kombe la Dunia kwa ngazi ya Klabu.
Ni kocha anayeifahamu vizuri Man City. Alianza kama kocha wa timu za vijana mwaka 2020, kabla ya kupandishwa na kuwa msaidizi wa Guardiola mwaka 2022.
Kwamba Muitalia huyo alikuwa kwenye benchi la ufundi wakati Man City inatwaa mataji matatu kwa mpigo mwaka 2023. Ligi ya Mabingwa, Ligi Kuu na FA.
Wakala wake ni Jorge Mendes, ambaye ni rafiki mkubwa wa Mkurugenzi wa Michezo wa klabu hiyo, Viana.






