Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Serikali imeandaa mwongozo maalumu wa kisheria utakaowawezesha wanahabari wakongwe walioathiriwa na mfumo wa ithibati kurejea rasmi katika taaluma hiyo nchini.
Akisoma hotuba ya wizara hiyo leo Mei 4, 2026, Makonda alisema mwongozo huo umeandaliwa kupitia Bodi ya Uandishi wa Habari Tanzania kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Huduma za Habari, ambayo inalenga kukuza na kuimarisha taaluma ya habari nchini.
Aidha amefafanua kuwa mwongozo huo utaweka utaratibu wa kisheria wa kutambua na kuthibitisha umahiri wa wanahabari hao, hatua itakayowawezesha kupata ithibati ya kitaaluma na kuendelea na shughuli zao kwa mujibu wa sheria.
Hatahivyo Makonda ameongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuwapa fursa wanahabari wenye uzoefu mkubwa ambao walijikuta nje ya mfumo rasmi kurejea na kuchangia maendeleo ya sekta ya habari kwa kuzingatia misingi ya taaluma na maadili.
Sanjari na hayo wizara imeeleza kuwa itaendelea kuboresha mifumo na sera mbalimbali ili kuhakikisha taaluma ya habari nchini inakuwa na viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.






