LONDON, Uingereza
BAADA ya Harry Maguire kusaini mkataba mpya Manchester United, beki huyo amejitoa kwenye orodha ya wachezaji watakaokuwa huru kuziacha klabu zao wakati wa usajili wa kiangazi, 2026.
Je, ni wachezaji gani wengine watakaokuwa wamemaliza mikataba yao kufikia kipindi hicho? Makala haya yanachambua.
ALEX TUANZEBE
Nyota wa zamani wa Manchester United, ambaye kwa sasa anaitumikia Burnley. Raia huyo wa DRC ana umri wa miaka 28.
Endapo klabu hiyo haitampa mkataba mpya, basi Tuanzebe ataondoka bure kupitia dirisha kubwa la usajili.
IDRISSA GUEYE
Mkataba wake utakwisha majira ya kiangazi, ingawa Everton wanaruhusiwa kumpa nyongeza ya miezi 12.
Msenegal huyo mwenye umri wa miaka 36 anaungana na Vitalii Mykolenko na Michael Keane, ambao pia watakuwa huru majira ya kiangazi.
RYAN SESSEGNON
Beki wa kushoto wa Fulham mwenye umri wa miaka 25. Mkataab wake utakwisha majira ya kiangazi lakini klabu hiyo inaweza kumuongeza miezi 12.
Nyota mwingine tegemeo wa Fulham atakayekuwa huru kipindi hicho ni mshambuliaji Raul Jimenez.
IBRAHIMA KONATE
Atakuwa mchezaji huru majira ya kiangazi, ingawa beki wa kati huyo raia wa Ufaransa amesema anakaribia kuongeza mkataba wa kubaki Liverpool.
Mastaa wengine wa Anfield wanaomaliza mikataba yao kiangazi ni Andy Robertson, Rhys Williams, na kipa chaguo la tatu, Freddie Woodman.
BERNARDO SILVA
Kiungo huyo atamaliza mkataba wake kiangazi na ameshaweka wazi kuwa ataondoka katika klabu ya Manchester City.
Mbali ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 31, mwingine aliye ukingoni mwa mkataba wake ni beki John Stones.
CASEMIRO
Ana umri wa miaka 34 na mkataba wake na Manchester United utafikia ukomo majira ya kiangazi. Mbrazil huyo anahusishwa na klabu za Marekani.
Nyota wengine wa Old Trafford wanaoelekea ukingoni mwa mikataba yao ni Tyrell Malacia, Jadon Sancho, Tom Heaton na Dan Gore.
KIERAN TRIPPIER
Nyota wa kimataifa wa England mwenye umri wa miaka 35. Mkataba wake na Newcastle United utakwisha majira ya kiangazi. Ataondoka.
Wachezaji wengine wanaoelekea kumaliza mikataba yao ni Fabian Schar, Emil Krafth na Matt Targett, 30, Mark Gillespie na John Ruddy.
STEFAN ORTEGA
Kipa wa Nottingham Forest. Ana umri wa miaka 33 na mkataba wake mfupi aliosaini Januari, 2026 utakwisha majira ya kiangazi. Wengine ni Angus Gunn na Willy Boly.
BERTRAND TRAORE
Winga huyo wa Sunderland raia wa Burkina Faso atamaliza mkataba wake pia. Ni kama ilivyo kwa beki wa kushoto wa timu hiyo, Dennis Cirkin.
YVES BISSOUMA
Kiungo raia wa Mali anayekipiga Tottenham. Ana umri wa miaka 29 na mkataba wake utakwisha majira ya kiangazi.
Mwingine ni mchezaji wa muda mrefu zaidi klabuni hapo, Ben Davies, ambaye hajacheza tangu alipovunjika mguu Januari, 2026.
ADAMA TRAORE
Winga wa West Ham United. Ana umri wa miaka 30. Nyota wengine wa timu hiyo watakaomaliza mikataba majira ya kiangazi ni Callum Wilson na kipa Lukasz Fabianski.






