Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewataka wataalamu wa fani ya ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi nchini kuhakikisha wanatumia uwezo wao wa kitaaluma kuibua bunifu za kisayansi, zenye gharama nafuu na zenye tija kwa maendeleo ya Sekta ya Ujenzi.
Akizungumza Mkoani Morogoro wakati akifungua Semina ya Mafunzo Endelevu (CPD) pamoja na maonesho ya vifaa vya ujenzi yaliyoandaliwa na AQRB, Ulega amesisitiza kuwa ubunifu ni nyenzo muhimu katika dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria za upangaji miji na usanifu bora wa majengo, huku akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza ushindani wa nchi kitaifa na kimataifa, pamoja na kuvutia uwekezaji na kukuza sekta ya utalii nchini.
Amewataka kutoa huduma za kitaalamu kwa weledi ili jamii iweze kutambua tofauti kati ya wataalamu waliosajiliwa na wale wasiothibitishwa na serikali.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa AQRB, Arch Dkt. Daniel Matondo, amesema bodi hiyo itaendelea kusimamia na kuendeleza taaluma hiyo kwa weledi, huku ikiimarisha ushindani na ubunifu miongoni mwa wataalamu wa Sekta hiyo.
Naye, Rais wa Chama cha Wabunifu Majengo Tanzania, Mecky T’chawi, ameahidi kuendelea kushirikiana na serikali kupitia Wizara ya Ujenzi pamoja na Taasisi mbalimbali kuhakikisha Sekta ya Ujenzi nchini inakuwa ya kisasa na inayozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.












