LONDON, Uingereza
BAADA ya Andoni Iraola kutangaza kuwa ataondoka Bournemouth, ameingia kwenye orodha ya makocha wa Ligi Kuu ya England (EPL) wanaoweza kuziacha klabu zao mwishoni mwa msimu huu.
Iraola mwenye umri wa miaka 43, ambaye aliajiriwa na Bournemouth mwaka 2023 kuchukua nafasi ya Gary O’Neil, anaweza kurudi katika klabu yake ya zamani ya Athletic Bilbao.
Wakati huo huo, Crystal Palace nayo itapoteza kocha mwishoni mwa msimu huu baada ya Oliver Glasner kusema ataondoka. Ripoti zinadai kuwa Iraola atachukua nafasi yake.
Kama si yeye, basi huenda akawa ni Thomas Frank aliyefukuzwa Tottenham au Sean Dyche, ambaye amekuwa nje ya kazi tangu alipotimuliwa na Nottingham Forest.
Hatima ya Pep Guardiola nayo iko angani, tetesi zikidai kuwa huenda huu ukawa msimu wake wa mwisho kuinoa Manchester City.
Makocha wanaohusishwa na kiti chake ni Enzo Maresca aliyeondoka Chelsea na kocha aliyefukuzwa Real Madrid, Xabi Alonso.
Liverpool nayo huenda ikawa na kocha mpya endapo itamfuta kazi Arne Slot. Timu hiyo haina matokeo mazuri msimu huu, licha ya kutumia Pauni milioni 450 katika soko la usajili.
Alonso, ambaye aliwahi kucheza Liverpool kwa mafanikio makubwa akiwa eneo la kiungo, ndiye anayehusishwa zaidi na kibarua hicho.
Manchester United nayo inatarajiwa kuwa na kocha mpya msimu ujao, ingawa pia inawezekana kumuajiri moja kwa moja Michael Carrick.
Wanaohusishwa zaidi na kibarua cha kupokea kijiti ni kocha wa sasa wa timu ya Taifa ya Ujerumani, Julian Nagelsmann, na Thomas Tuchel anayeinoa England.
Newcastle United nayo huenda ikawa na kocha mpya kwani Eddie Howe anapitia wakati mgumu wa kukosolewa na mashabiki wa timu hiyo.






