Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, Aprili 11, 2026, imefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika halmashauri hiyo kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi yanavyoendelea.
Akiongoza ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mandwanga, Mhe. Ally Ulaya, ameonesha kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, huku akimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndugu Anderson Msumba, kuongeza juhudi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati uliopangwa.
Amesema kuwa miradi hiyo ina manufaa makubwa kwa wananchi wa Mtama, hususan katika kuboresha huduma za kijamii kama afya, lakini akabainisha kuwa bado kuna haja ya kuongeza kasi ya utekelezaji wake.
“Tumeshuhudia namna miradi hii itakavyowanufaisha wananchi, lakini kasi yake hairidhishi. Ni muhimu kuongeza nguvu ili ikamilike na ianze kutoa huduma,” amesema Mhe. Ulaya.
Aidha, Mhe. Ulaya amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo ili waweze kukamilisha kazi kwa ubora na ufanisi, jambo litakalosaidia kudumu kwa muda mrefu na kutoa huduma iliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndugu Anderson Msumba, amesema halmashauri inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za ndani kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati, ikiwemo kuboresha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umeanza kuleta mabadiliko chanya katika Wilaya ya Mtama, ikiwemo kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.
Katika ziara hiyo, Kamati ilitembelea miradi ya ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Mtama pamoja na jengo la mionzi katika Kituo cha Afya Mtama.






