Mkuu wa Taji wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, amekutana na Rais wa Baraza la Ulaya, Antonio Costa, katika mji wa Jeddah kwa ajili ya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano kati ya pande hizo mbili.
Katika mkutano huo, viongozi hao walifanya tathmini ya makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati kati ya Saudi Arabia na Umoja wa Ulaya, wakilenga kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali.
Aidha, walijadili njia za kukuza ushirikiano wa pamoja katika nyanja tofauti za maendeleo, sambamba na kubadilishana mawazo kuhusu hali ya sasa ya kisiasa na kiusalama katika eneo la Mashariki ya Kati.
Mazungumzo hayo pia yaligusia athari za kiuchumi na kiusalama zinazoikumba dunia, huku pande zote zikisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto hizo kwa manufaa ya pande zote mbili, kikanda na kimataifa.






