HATUA ya kutangaza kuwa raia wake waaitarajie demokrasia imeibua maswali mengi juu ya uongozi wa Kapteni Ibrahim Traore nchini Burkina Faso.
Traore aliyeingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi mwaka 2022, alisema demokrasia iliyoletwa na mataifa ya Magharibi imesababisha mauaji mengi barani Afrika, hivyo haoni kama inapaswa kukumbatiwa.
USHAWISHI WAKE MITANDAONI
Mara tu baada ya kuingia madarakani, Traore alijizolea umaarufu mkubwa katika majukwaa mbalimbali ya kidigitali, akitafsiriwa na kizazi cha ‘Gen Z’ kuwa ni kiongozi wa aina yake.
Mvuto wake mkubwa kwa vijana si tu ulitokana na umri wake mdogo wa miaka 34 wakati anaingia Ikulu, bali pia sera zake za kupinga mataifa ya Magharibi.
Katika hotuba zake, alijipambanua kuwa ni ‘adui’ wa mabeberu, akieleza anavyochukizwa na namna rasilimali za Afrika zinavyoibiwa na wakati mwingine kuuzwa na viongozi wanaoshirikiana na Marekani na mataifa ya Ulaya.
ALIVYONG’ANG’ANIA MADARAKA
Alipoingia Ikulu, Kapteni Traore aliahidi kuwa isingepita miaka miwili kabla ya kuachia madaraka na kupisha Uchaguzi Mkuu utakaowapatia wananchi haki ya kuchagua rais wanayemtaka.
Hata hivyo, ahadi hiyo ilipotelea gizani baada ya uamuzi wake wa kujiongezea miaka mitano ya kuendelea kuiongoza Burkina Faso.
Kama hiyo haitoshi, Kapteni Traore alipiga marufuku vyama vya siasa kuendesha shughuli zao. Kwa ufupi, alivifungia vyote.
AMESHINDWA KUMALIZA UGAIDI?
Licha ya jitihada kubwa ambazo uongozi wake umekuwa ukisema umeifanya, hali ya usalama nchini Burkina Faso bado ni ‘pasua kichwa’.
Jeshi la nchi hiyo linadhibiti asilimia zisizozidi 30 tu ya ardhi ya Burkina Faso. Maeneo mengi yako chini ya vikundi vya kigaidi, kikiwamo cha Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) chenye ushirikiano na Al-Qaeda.
Ripoti ya hali ya ugaidi duniani ya Global Terrorism Index ya mwaka 2026 Iko wazi, kwamba Burkina Faso ni ya pili baada ya Pakistan.
Kwa mwaka 2025 pekee, watu 846 waliuawa, ikiwa ni asilimia 15 ya wahanga wa matukio ya kigaidi duniani kote.
PRESHA KUTOKA KWA DIASPORA
Raia wa Burkina Faso waishio nie ya nchi wameungana na wenzao wa mataifa mengine ya Ukanda wa Sahel kutaka viongozi wa kijeshi kuachia madaraka.
Ifahamike kuwa mbali ya Burkina Faso, Mali na Niger nazo zinaongozwa na viongozi walioingia Ikulu kwa kupindua serikali zilizokuwa madarakani.
Kupitia Umoja wao wa Alliance of Democrats of the Sahel (ADS), diaspora wanataka kuona wananchi wakiwa na haki ya kuchagua viongozi, badala ya jeshi kuongoza nchi.
“Tunapambania amani na kurejea kwa demokrasia,” anasema Rais mpya wa ADS, Mayra Djibrine, na kuongeza: “Tutatumia njia za kidiplomasia kushinikiza viongozi wa kijeshi kuachia wafungwa wa kisiasa na kuandaa chaguzi.”
Hata hivyo, kwa baadhi ya wachambuzi wa siasa, hawaioni nguvu ya Diaspora ikitosha kuleta mabadiliko hayo. Kwamba raia wa ndani ndiyo wenye nguvu ya kuondosha tawala za kijeshi katika mataifa yao.
“Huwezi kutisha viongozi hawa (wa kijeshi) kwa matamko kutoka Brussels (Ubelgiji), Paris (Ufaransa), au kwingineko,” anasema mchambuzi Daouda Emile Ouedraogo.






