UTAFITI: VIJANA WENGI WANAKWEPA KUPIMA UKIMWI

Date:

Share post:

KASI ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa vijana imeendelea kuwa kubwa barani Afrika, huku kundi hilo likiwa na mwitikio mdogo katika kupima afya zao, kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO).

Hali ni mbaya zaidi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo maambukizi mapya kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 ymeripotiwa kufikia 370,000.

Hiyo ni sawa na asilimia 28 ya maambukizi mapya milioni 1.3 duniani kote, huku wasichana wenye umri huo wakiwa wengi, kuliko wenzao wa jinsia ya kiume.

WHO inasisitiza umuhimu wa kupima, ikieleza kuwa hatua hiyo ya kujua hali ya kiafya inaweza kusaidia matibabu ya mapema katika kukabiliana na ugonjwa huo.

“Kupata matibabu kutapunguza makali ya ugonjwa na hata kuzuia maambukizi kwa wengine,” inaeleza WHO.

Shirika hilo lilifanya utafiti wake katika nchi 28 za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ukihusisha vijana wa kiume na wa kike zaidi ya 58,000 na ukichukua miaka 12 (2010-2022).

“Utafiti wetu ulilenga kubaini kama wamewahi kupima Ukimwi. Katika nchi 28, ni asilimia 63 tu ya vijana waliosema wamewahi kupima. Ikimaanisha, mmoja kati ya vijana watatu hajawahi kupima,” ilieleza ripoti ya utafiti huo.

Vilevile, kulikuwa na tofauti kati ya nchi moja na nyingine. Hali ilionekana mbaya zaidi kwa Mali, Chad na Benin, ambako asilimia kubwa ya vijana walisema hawajawahi kupima Ukimwi ili kujua afya zao.

Zambia ikiwa na asilimia 76, ilionekana kuwa na mwamko mkubwa kwa vijana wake kupima, wakati huo Mali (6.7%) ikifanya vibaya zaidi.

Hata hivyo, robo-tatu ya nchi 28 zilizohusishwa katika utafiti huo zilionekana kutokufikisha asilimia 50 ya vijana waliopima afya zao.

Aidha, tofauti ya umri, kipato, elimu, na maeneo ya kuishi yalionekana kuwa na nafasi kubwa kwa vijana kufanya maamuzi ya kupima Ukimwi.

Mathalan, vijana wanaoishi mjini walikuwa na mwamko mdogo wa kupima, tofauti na wenzao wa maeneo ya vijijini. Ni kama ilivyo kwa wasomi dhidi ya wasiosoma.

Mbali ya mambo mengine, mazingira ya vijijini yanachagiza umbali wa kufikia vituo vya afya, pia ukosefu wa taarifa sahihi.

Wakati huo huo, dhana ya unyanyapaa nayo imeendelea kuwa kizingiti kikubwa. Kwamba vijana wengi wanahofia kupima wakiamini endapo watakutwa na maambukizi, watanyooshewa vidole na hata kutengwa katika jamii wanazoishi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

spot_img

Related articles

MEGAN AACHANA NA MPENZI WAKE KISA ‘KUCHEPUKA’

LOS ANGELES, Marekani BIBIYE mwenye jina kubwa katika soko la muziki wa Hip hop nchini Marekani, Megan thee stallion,...

SERIKALI YAWEKA WAZI MKAKATI WA KUIFANYA SEKTA YA MADINI KUWA MHIMILI WA UCHUMI

Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma leo Aprili 27, 2026,...

KINDA AJAX AZIGONGANISHA ARSENAL, CHELSEA

LONDON, Uingereza KLABU za Arsenal na Chelsea zimeingia kwenye vita ya kuiwania saini ya staa wa Ajax ya Uholanzi,...

MABORESHO YA UWANJA WA BENJAMINI MKAPA YAANZA RASMI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson...