TAKWIMU zinaonesha kuwa baada ya bangi, Heroin ni aina ya pili ya dawa za kulevya zinazotumiwa zaidi hapa nchini, huku kundi la vijana likiwa hatarini zaidi.
Heroin ni nini? Ni aina ya dawa ya kulevya inayotengenezwa na kemikali ya asili inayoitwa ‘morphine’ ambayo inapatikana kwenye utomvu wa tunda la mmea wa afyuni (opium poppy) unaolimwa zaidi kwenye nchi za Afghanistan, Myanmar na Laos.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya hapa nchini (DCEA), kuna njia tatu za utumiaji wa Heroin.
Mosi, hutumiwa kwa njia ya kuvuta ikiwa imechanganywa na kiasi kidogo cha bangi na sigara. Pili, kwa njia ya kunusa. Tatu, ni kwa kujidunga sindano.
Heroin ni kati ya dawa za kulevya zinazoongoza kwa kusababisha ‘uteja’ haraka, maradhi mbalimbali, na hata vifo vinavyotokana na kuzidisha kiasi cha matumizi.
DCEA katika tovuti yake, inaeleza kuwa Heroin inayofahamika pia kwa majina ya ‘unga’, ‘ngada’, ‘teli’ (cocktail), ‘msharafu’, ‘white’, ‘kijiwe’ na ‘brown’, ina watumiaji wengi wanaohitaji tiba.
Heroin, kwa mujibu wa DCEA, husababisha magonjwa ya moyo, ini, mapafu, meno, ngozi, figo na saratani, pia kushirikiana sindano za kujidunga kunaweza kuzalisha maambukizi ya kifua kikuu, Ukwimi na homa ya ini.
Pia, matumizi ya Heroin na pombe huweza kusababisha kifo. Mtumiaji anapoacha kutumia, hupitia changamoto za maumivu makali, homa, kuharisha, kizunguzungu na kichefuchefu.
Vilevile, matumizi ya Heroin, husababisha kukosa hamu ya kula, upungufu wa maji mwilini, kukosa choo, na mishipa ya damu kusinyaa.
Madahara yake kwa jamii ni pamoja na ongezeko la vitendo vya uhalifu (udokozi, unyang’anyi, utapeli na biashara ya ngono).
Kwa wawanawake, matumizi ya Heroin huweza kuharibu mimba au kuzaa watoto njiti, wenye uteja na heroin au udumavu wa mwili na akili.
Je, Sheria inasemaje juu ya kujihusisha na dawa hizo? Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95, kujihusisha na Heroin kwa namna yoyote ni kosa la jinai.
Kwa hiyo, kusafirisha ndani na nje ya nchi, kuuza, kuhifadhi, kusambaza, kutumia na kutengeneza Heroin ni kosa la jinai na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha gerezani.






