KYIV, Ukraine
UKRAINE na Israel ni mataifa yaliyokuwa na uhusiano mzuri, kabla ya hivi karibuni kuzuka kwa kasheshe, ambayo Urusi imetajwa kuwa chanzo chake.
Mgogoro ulianzia kwa mwandishi wa habari, Kateryna Yaresko, ambaye anaripoti habari za uchunguzi dhidi ya uhalifu dhidi ya Serikali ya Ukraine.
Aprili 12, 2026, Yaresko alitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook kuripoti juu ya meli iliyowasili katika bandari ya Israel ikiwa imebeba nafaka aina ya ngano zilizoibiwa Ukraine.
Kwa mujibu wa mwandishi huyo, meli hiyo inayofahamika kwa jina la Abinsk inatumiwa na Urusi kufanya uhalifu huo.
Yaresko alisema Abinsk ilitia nanga katika bandari ya mjini Haifa, Israel, ikiwa na mzigo wa tani 43,765.18 za ngano kutoka Ukraine.
Siku chache baada ya ripoti hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha, naye aliibua shutuma za aina hiyo, akisema meli iliyobeba nafaka zilizoibiwa na Urusi nchini kwake iliwasili Israel.
Sybiha aliongeza kuwa kwa muda mrefu wameziomba mamlaka za Israel kufanya uchunguzi juu ya meli hiyo, lakini wenzao hao hawakufanya hivyo.
“Ni ngumu kuelewa kwanini Israel haifanyii kazi ombi la Ukraine juu ya bidhaa za wizi zinazowasili Haifa,” alisema kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X.
Aidha, Waziri huyo alienda mbali zaidi na kusema kitendo cha Israel kufumbia macho uhalifu unaofanywa na Urusi kinahatarisha uhusiano wa mataifa hayo.
Siku hiyo pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar, alijibu shutuma hizo, akidai hakuna ushahidi uliowekwa mezani.
“Mahusiano ya kidiplomasia, hasa kwa mataifa marafiki, hayaendeshwi kupitia Twitter au vyombo vya habari,” alisema, huku akisistiza kuwa Israel itachuguza na kuchukua hatua kali endapo itabaini kuwapo kwa uhalifu huo.
Kwa upande wake, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, alisema Israel inafahamu wazi kuwa ni kosa la jinai kununua bidhaa za wizi.
“Urusi imekuwa ikiiba nafaka katika ardhi ya Ukraine. Tumechukua hatua zote za kidiplomasia kukomesha uhalifu huo,” alisema.
Rais Zelenskyy aliweka wazi kuwa tayari Serikali yake inaandaa vikwazo kwa nchi au watu watakaojihuisha na nafaka zinazouzwa na Urusi zikitokea Ukraine.






