MERSEYSIDE, Uingereza
BAADA ya beki wa kushoto Andy Robertson kuthibitisha kuwa ataondoka Liverpool mwishoni mwa msimu huu, klabu kadhaa barani Ulaya zimeanza kujipanga kuwania saini yake, zikivutiwa na uzoefu wake mkubwa pamoja na uwezo wake wa kucheza kwenye kiwango cha juu kwa muda mrefu.
Robertson, mwenye umri wa miaka 32, anatarajiwa kuhitimisha safari yake ndani ya Anfield baada ya kuitumikia Liverpool kwa takribani miaka tisa, kipindi ambacho amejijengea heshima kubwa kama mmoja wa mabeki bora wa kushoto waliowahi kucheza Premier League katika kizazi cha sasa.
Safari yake ya soka na mafanikio Liverpool
Mchezaji huyo raia wa Scotland alijiunga na Liverpool akitokea Hull City, na tangu hapo akawa sehemu muhimu ya kikosi kilichotawala soka la England na Ulaya chini ya kocha Jurgen Klopp. Uwezo wake wa kupanda na kushuka pembeni, kutoa pasi za mwisho (assists), pamoja na kucheza kwa nguvu na nidhamu ya kiulinzi, ulimfanya kuwa chaguo la kwanza kwa misimu mingi.
Katika kipindi chake Liverpool, Robertson amekuwa akihusishwa moja kwa moja na mafanikio makubwa ya klabu hiyo, ikiwemo kutwaa mataji makubwa kama Ligi Kuu ya England na Ligi ya Mabingwa Ulaya, sambamba na vikombe vingine vya ndani na kimataifa.
Mbali na mafanikio ya klabu, Robertson pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Scotland, jambo linaloonyesha uongozi wake na uzoefu mkubwa kwenye mashindano ya kimataifa.
Kwanini klabu nyingi zinamuwania?
Ripoti zinaeleza kuwa klabu mbalimbali zimeanza kumuangalia Robertson kutokana na sababu kadhaa:
Baadhi ya sababu zinazitajwa ni pamoja na uzoefu alionao wa kucheza mashindano mbalimbali makubwa kama Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, uwezo wa kiuongozi na ule wa kuhimili presha za kila namna za ndani na nje ya uwanja, ubora wake katika kupandisha mashambulizi wakati timu ikiwa na mpira, jambo linalohitajika sana kwenye mfumo wa kisasa wa mabeki wa pembeni.
Aidha, sababu nyingine ni unafuu wa upatikanaji wake kwani kutokana na umri wake na kuwa anatarajiwa kuondoka Liverpool, hivyo klabu zinaweza kupata huduma yake kwa bei isiyo kubwa sana.
Tottenham na Atletico Madrid zikitajwa
Klabu ya Tottenham Hotspur imetajwa kuwa miongoni mwa timu zinazomtolea macho beki huyo, huku ikionekana kuhitaji kuongeza ubora na ushindani kwenye nafasi ya beki wa kushoto ili kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya kampeni za ndani na Ulaya.
Kwa upande mwingine, Atletico Madrid ya Hispania nayo inatajwa kumuwania Robertson, ikiamini uzoefu wake na uwezo wa kucheza kwa nidhamu ya kiulinzi vinaendana moja kwa moja na falsafa ya kocha wao inayopendelea wachezaji wanaojituma na kuwa wagumu kuvunjika kiakili.
Juventus na Napoli nazo zipo kwenye mbio
Katika Serie A, vigogo Juventus na Napoli pia wameripotiwa kuonyesha nia ya kumsajili. Juventus inaaminika kutaka kuongeza uzoefu kwenye safu ya ulinzi, huku Napoli ikitafuta mchezaji mwenye uwezo wa kuongeza nguvu ya pembeni, hasa kwa mfumo wao unaotegemea mabeki wanaoshambulia.
Hatua inayofuata kwa Robertson
Ingawa bado haijajulikana ni klabu gani itashinda mbio za kumsajili, ni wazi kuwa Robertson bado ana mvuto mkubwa barani Ulaya. Uzoefu wake wa kiwango cha juu, pamoja na uwezo wake wa kuongoza kikosi, vinaendelea kumfanya kuwa mchezaji wa thamani kwa timu zinazotaka kupambana kwenye ligi zao na mashindano ya Ulaya.
Kwa sasa, macho na masikio ya mashabiki yanasubiri kuona ni wapi nyota huyo wa Scotland ataelekeza maisha yake mapya ya soka baada ya kuhitimisha ukurasa wake wa kihistoria ndani ya Liverpool.
Imeandaliwa na Hassan Mwasha






