NA RIPOTA WA PANORAMA
HAYATI Rais Dk. John Pombe Magufuli, leo ameagwa na wabunge na watumishi wa Bunge katika viunga vya Bunge la Jamhuri, kabla mwili wake haujapelekwa Uwanja wa Jamhuri kwa ajili ya mazishi ya kitaifa.
![]() |
Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumza wakati wa kuaga mwili wa Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli katika viunga vya Bunge, Jijini Dodoma.
Spika wa Bunge, Job Yustino Ndugai amewaongoza wabunge na watumishi wa Bunge kumuaga Hayati Rais, Dk. Magufuli akiwa sambamba na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson na Spika wa Baraza la Wawakilishi.
Akizungumza kabla ya kuagwa kwa Hayati Rais Dk. Magufuli, Spika Ndugai amesema historia ya Rais Hayati Dk. Magufuli inaonyesha amekuwa miongoni mwa wana jumuiya ya Bunge kwa miaka 26.
“Amekuwa sehemu ya jumuiya hii tangu mwaka 1995 kama mheshimiwa mbunge, naibu waziri, waziri na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais wetu katika historia yake amekuwa mwenzetu hapa bungeni kwa miaka 26, amekuwa sehemu ya jumuiya hii tangu mwaka 1995.
“Leo ni siku ya majonzi makubwa hapa bungeni kwa kuwa tumefiwa na mwenzetu, tumelemewa, tumechanganyikiwa, Watanzania tunalia, sisi wabunge tunasema asante Mungu kwa ajili ya Rais John Pombe Magufuli aliyeishi siku zote kwa kumtanguliza Mungu mbele.
“Namshukuru Mungu kwa kunipa fursa ya kufanya kazi na Hayati Rais Magufuli kwa miaka 20 bungeni kama rafiki yangu, ndugu yangu na kama kiongozi wangu, safari imetimia na mwendo ameumaliza, rafiki yangu John leo amelala mbele yetu.
“Dk. Magufuli ulikuwa mtu mwema, alipanda mbegu, alikuwa mpanzi kama yule mpanzi wa kwenye Biblia, naamini mbegu aliyopanda imedondoka kwenye udongo mzuri, amepanda barabara za lami kila sehemu ya nchi yetu, madaraja ambayo hatukuamini kama tungeyaweza, amejenga masoko, amejenga meli, viwanja vya ndege, reli ya kisasa SGR, Bwawa la Umeme la Nyerere Rufiji, shule, viwanda, vyuo, vituo vya afya, hospitali, amejenga, amejenga, amejenga,” ameomboleza Spika Ndugai.
Aidha, amesema ni jambo la kumshukuru Mungu kulipatia taifa Rais Samia Suluhu Hassan na amemuombea siha njema, uhodari, subira, ustahimilivu na asipungukiwe hekima na kwamba wabunge watasimama naye.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa kuaga mwili wa Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo.
Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kila anapoangalia jeneza la Hayati Rais Dk. Magufuli anahisi kama anampigia simu akimpa maagizo na maelekezo.
“Sina kubwa la kusema, waliotangulia wamesema mengi kuhusu mpendwa wetu, binafsi napata shida kusema, naona kama vile ananipigia simu, ananipa maagizo, naomba mnivumilie, ni siku ngumu kwetu.
“Kila mmoja ana neno la kumuelezea Dk. Magufuli, tukianza kuelezea hatutamaliza, amefanya mambo mengi kwenye majimbo yetu, tunachokifanya leo hapa ni kumuombea dua, ni majonzi makubwa kwetu, na sio kwetu tu Watanzania bali Afrika inamlilia, inasikitika, nchi za SADC, Bara la Afrika linamlilia.
“Alikuwa sehemu ya viongozi wa bara hili, hivyo majonzi haya siyo ya kwetu peke yetu. Jukumu letu ni kumuombea, tunamlaza katika nyumba yake ya milele Machi 26, leo tumepata fursa ya kuja kumuombea.
“Kwa uzoefu ambao tumeupata Dar es Salaam, watu walikuwa wengi sana hivyo kwa hapa Dodoma tumeamua kubadilisha utaratibu, badala ya kwenda kuaga na kumuangalia tutakachofanya ni kuzungusha mwili mara mbili au tatu uwanjani,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema baada ya kuagwa katika uwanja wa Jamhuri, gari lililobeba mwili wake litapita katika barabara mbalimbali za Jiji la Dodoma ili wananchi waone jeneza lake.
Amesema wakati Watanzania wakimuombea Hayati Rais Dk. Magufuli na kumuaga katika viwanja hivyo vya Bunge, mama mzazi wa Hayati Rais Dk. Magufuli yupo kitandani kwa mwaka wa pili akiugua hivyo amewaomba Watanzania wamuombee.
Spika wa Bunge, Job Ndugai na mkewe, Dk. Fatma Mganga wakiweka shada la maua katika Jeneza la Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli wakati wa kuaga mwili wake katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Wabunge wakitoa heshima za mwisho kwenye Jeneza lenye mwili wa Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli katika viunga vya Bunge.