NDUVA AAGA, AMSHUKURU RAIS SAMIA UUNGAJI MKONO WA MTANGAMANO WA EAC

Date:

Share post:

DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Veronica Nduva ametoa shukrani za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano wa karibu alioupata katika kipindi chote cha utumishi wake katika EAC.

Nduva amemtaja Rais Samia kama kiongozi mwenye uchu wa maendeleo ya jumuiya na anayethamini nafasi ya mwanamke katika uongozi.

Veronica Nduva

Aidha, amemsifu Rais Samia kwa utayari wake wa kushirikiana naye wakati wote, akisisitiza kuwa Tanzania inaendelea kutambulika kama kinara wa mtangamano na maendeleo ya jumuiya na kwamba uongozi wa Rais Samia umeongeza msukumo wa ajenda hiyo kwa maslahi ya wananchi wa Afrika Mashariki.

Vilevile, amemshukuru Rais Samia kwa ushirikiano, msaada na uwezeshaji alioupata akiwa Tanzania akibainisha kuwa muhula wake unatarajiwa kumalizika mwezi Aprili 2026.

Kwamba kwa msingi huo, ziara hiyo ilikuwa ya heshima ya kumuaga na kusisitiza thamani ya ushirikiano kati ya Tanzania kama nchi mwenyeji na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Rais Samia amesema Tanzania ni mdau mkubwa wa shughuli za maendeleo Afrika Mashariki na itaendelea kuunga mkono ajenda za kikanda zinazolenga kuleta maendeleo kwa wananchi, ikiwemo kurahisisha biashara kati ya nchi wanachama, kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, pamoja na masuala mengine ya kipaumbele.

Rais Samia amempongeza Nduva kwa mchango wake wa kuimarisha biashara ndani ya jumuiya na kueleza kuwa Tanzania inaendelea na marekebisho ya itifaki ya umoja wa forodha ili kuruhusu uendeshaji wa kamati ya marekebisho ya biashara (trade remedies committee) kabla ya kuiwasilisha katika ofisi ya katibu mkuu wa jumuiya hiyo.

Kadhalika, Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania inatambua jukumu lililo mbele ya wakuu wa nchi la kuteua katibu mkuu mpya wa EAC na kwamba Tanzania imeweka mkazo katika kupata kiongozi bora kwa kuzingatia katiba ya jumuiya na kanuni ya mzunguko (rotation) baina ya nchi wanachama.

Tanzania itaunga mkono yeyote atakayeteuliwa au kupendekezwa kuwa mwenyekiti au katibu mkuu wa jumuiya.

Mazungumzo hayo pia yalilenga kukamilisha hatua za mwisho za maandalizi ya mkutano wa wakuu wa nchi wa EAC utakaofanyika Machi 7, 2026 jijini Arusha, ambapo Rais Samia amesisitiza uongozi, utayari na dhamira ya Tanzania kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa mafanikio kwa kutoa ushirikiano na mazingira wezeshi yanayostahili kama nchi mwenyeji.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Katibu Mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki, Veronica Nduva.

Miongoni mwa ajenda zinazotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo ni uteuzi wa katibu mkuu mpya wa EAC, sambamba na masuala mengine ya kipaumbele kwa maendeleo na mtangamano wa Jumuiya

About The Author

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

spot_img

Related articles

UCHUMI WA CHINA WAZIDI KUIMARIKA

BEIJING, China LICHA ya vita vya Marekani na Iran kuonekana kuitikisa dunia, China imeendelea kupiga hatua kubwa katika eneo...

SIKU 100 ZA RAIS MPYA WA VENEZUELA: MABADILIKO NA MASWALI MAPYA

CARACAS, Venezuela BAADA ya vikosi vya Marekani kumng’oa madarakani aliyekuwa Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro kwenye oparesheni ya Januari...

MAELFU YA FAMILIA SUDAN BADO WAKIMBIA VITA, HALI YA MAISHA YAZIDI KUWA MBAYA

MAELFU ya familia nchini Sudan bado wanalazimika kuyakimbia makazi yao, miji na hata mipaka ya nchi kufuatia vita...

ISRAEL YAENDELEA NA OPERESHEN DHIDI YA HEZBOLLAH NCHINI LEBANON

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Jeshi la nchi yake linaendelea na operesheni dhidi ya wanamgambo wanaoungwa...