![]() |
Jeneza lenya mwili wa Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli likiwa mbele ya Mapadre na Maaskofu wa Kanisa Katoliki wakati wa misa ya kumuombea katika Uwanja wa Magufuli, leo. |
MWANDISHI WA PANORAMA
ALIYEKUWA Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dk. John Pombe Magufuli amezikwa kaburini leo, Machi 26, 2021 katika eneo maalumu la familia lililo katika kijiji alichozaliwa wilayani Chato, Mkoa wa Geita.
Amezikwa kijeshi lakini ibada ya maziko yake imeongozwa Askofu wa Ngara, Severine Niwemugizi na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyewaongoza viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na umati mkubwa wa wananchi wa Mkoa wa Geita, vitongoji vyake, mikoa jirani na waombelezaji wengine kutoka nchi nzima na nchi za jirani.
Awali kabla ya kuzikwa kwake ilifanyika misa ya kumuombea katika Uwanja wa Michezo wa Magufuli iliyoongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga.
Mapema asubuhi, mwili wa Hayati Rais Dk. Magufuli aliondolewa nyumbani kwake na kupelekwa kanisani ambako ilifanyika misa ya kumuombea iliyohudhuriwa na wanafamilia na baadaye mwili wake ulipelekwa Uwanja wa Magufuli ilikofanyika misa iliyoongozwa na Askofu Mkuu Nyaisonga aliyekuwa sambamba na maaskofu 26 wa Kanisa Katoliki.
Aidha, misa hiyo ilihudhuriwa na Rais Samia, mjane wa marehemu, Janeth Magufuli, Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, Spika wa Bunge, Job Ndugai, Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Marais Wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Dk. Jakaya Kikwete, viongozi wengine wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na umati mkubwa wa wananchi.
![]() |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary Majaliwa wakiweka shada la maua kwenye kaburi la Hayati Rais Dk. John Magufuli |
Akizungumza katika misa hiyo, Rais Samia aliwashukuru watu wote waliohusika kushughulikia msiba huo wa kitaifa tangu Hayati Rais Dk. Magufuli alipofariki dunia, Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Emilio Mzena ya jijini Dar es Salaam kutokana na maradhi ya moyo.
Rais Samia aliishukuru kamati ya mazishi ya kitaifa iliyoongozwa na Waziri Mkuu Majaliwa, familia na ofisi binafsi ya Hayati Rais Dk. Magufuli kwa kufanikisha uagaji wa mwili wake katika sehemu zote ulizopita, mazishi ya kitaifa yaliyofanyika jijini Dodoma na hatimaye maziko yake kijijini Chato.
Aidha, Rais Samia aliwashukuru viongozi wa ndani na nje waliojitokeza kumsindikiza Hayati Rais Dk. Magufuli katika safari yake ya mwisho kwani ujio wao umedhihirisha mapenzi ya dhati waliyokuwa nayo kwake.
![]() |
Mjane wa Hayati Rais Dk. John Magufuli, Janeth Magufuli akiweka shada la maua kwenye kaburi la mume wake |
Alitoa pole kwa mjane wa Hayati Rais Dk. Magufuli, Janeth Magufuli, familia na wananchi wa Chato na aliihakikishia familia hiyo kuwa hataitupa na kwamba atahakikisha anatekeleza ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na ahadi alizotoa Hayati Rais Dk. Magufuli, siyo tu kwa wana Chato, bali kwa Watanzania wote.
Amewataka Watanzania wote kuendelea kumuombea Hayati Rais Dk. Magufuli ili apumzike kwa amani na kwamba japokuwa mwili wake umezikwa kaburini lakini maono na mikakati yake ingali inaishi.
![]() |
Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi akitoa salamu za pole wakati wa misa ya kumuombea Hayati Rais Dk. John Magufuli katika Uwanja wa Magufuli |
Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi ambaye alipewa fursa ya kuzungumza kabla ya Rais Samia, alisema kifo cha Hayati Rais Dk. Magufuli kimemuumiza yeye na Watanzania wote.
“Msiba huo ni mzito kwa Watanzania wote. Natoa pole kwa Rais Mama Samia, natoa pole kwa mama Janeth Magufuli, pamoja na watoto wetu, sio peke yako nasema poleni. Nawapa pole Mheshimiwa Hussein Mwinyi pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
“Nilimpenda sana Dk. Magufuli, kifo chake kimenishutua sana, baada ya kupata taarifa ya kifo nilikaa kimya kwa dakika mbili nikitafakari. Jambo ambalo ametuachia, pale alipofanya kijana huyu, kutekeleza maagizo ya baba wetu wa Taifa mzee Nyerere, kijana huyu amewaza na kuamua tuhamie Dodoma na kutekeleza jambo hilo kwa miaka miwili.
“Sisi wengine tulichukua miaka 40 na hatukufanya hivyo. Sio hilo tu ndugu yetu Dk. Magufuli amefanya mambo mengi sana na makubwa, mazuri na ya maana, ameyatekeleza kwa niaba yake na kwa niaba ya sisi wengine ambao hatukuwahi kutekeleza.Watanzania wenzangu, kwa kipindi cha miaka mitano tumepiga hatua, Dk. Magufuli ameishangaza dunia.
![]() |
Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi akiweka shada la maua kwenye kaburi la Hayati Rais Dk. John Magufuli |
“Ameleta maendeleo makubwa. Dk. Magufuli ameunganisha nchi kwa barabara za lami kwa muda mfupi wa miaka mitano, alikuwa mzuri wa takwimu angetuambia, lakini niseme barabara nyingi zimejengwa kwa muda mfupi. Amerahisisha biashara na masoko na uhakika wa mawasiliano, ndege zimerudi nchini, madege yetu wenyewe yanayokwenda kila mahali,” amesema Rais Mstaafu Mwinyi na kuongeza.
“Mama Siti yuko mbali ningemuuliza panaitwaje hapa, Chato. Huyu kijana wetu Hayati Dk. Magufuli amewaondolea fedheha Wamachinga ya kuwindwa kando kando za barabara, kwanza aliwapa muda rudini huko huko barabarani na kuahidi kuboresha mazingira ya biashara, anahurumia wanyonge, amewainua.
“Wamachinga amewaondolea manyanyaso ya kuwindwa kama ndege watundu, badala yake aliahidi kuwatengeneza mahala bora zaidi, sio machinga tu hata akina sie tumeingia kwenye huruma hiyo. Walikuwa wamepata mtu wa kuwasemea wa kuwafanya waonekane wa maana, huyu ndio Magufuli.
![]() |
Raus wa Zanzibar, na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Mwinyi na mkewe Mariam Mwinyi wakiweka shada la maua kwenye kaburi la Hayati Rais Dk. john Magufuli |
“Msinichoke kunisiliza na Watanzania wenzangu, aliyekuwa Rais wetu John Magufuli alifanya kazi kubwa ya kuinua wazee na masikini, narudia kwa kipindi kifupi cha miaka mitano nchi yetu ilipiga hatua kiasi cha kushangaza ulimwengu, kwanini?
“Alikuwa si mtu wa maneno, alikuwa wa vitendo na mfuatiliaji. Rais Magufuli amefanya mengi na kuondoka kwake ni msiba kwa kila mmoja wetu. Kama nilivyosema amefanya mengi, kila mmoja afikirie.
Kuhusu Rais Samia, Mwinyi amesema; “Mama Samia, Dk. Magufuli ameondoka, ametuachia wewe uliyekuwa msaidizi wake wa karibu sana, alichokusudia ndicho ambacho umekusudia wewe. Nimefurahi sana kusikia ile kauli kwamba wewe ndio Rais, kwa hiyo niseme, mambo mawili.
“Upokee pole kwa kuondokewa na mpendwa wetu, Hayati Dk.Magufuli na upokee pongezi kwa kupanda cheo, sote tunakuombea dua, mambo yaende vizuri, nchi hii uiweze na ushaiweza.”
![]() |
Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete akitoa salamu za pole wakati wa misa ya kumuombea Hayati Rais Dk. John Magufuli katika uwanja wa Magufuli |
Awali akitoa salamu kwa waombolezaji, Rais Mstaafu, Kikwete ametumia mwingi kumueleze Hayati Rais Dk. Magufuli jinsi alivyoipenda nchi ya Tanzania, alivyokuwa mchapakazi na alivyopanga naye mikakati ya kumsaidia katika ujenzi wa barabara na kwamba alimuamini na kumtumaini tangu akiwa Waziri.
Ametumia nafasi hiyo kuelezea namna alivyompenda kutokana na uchapakazi wake na alieleza mshangao wake kwa watu waliokuwa wakieneza umbeya kuwa hampendi
“Ngoja niwaambie niliamua kumuita Dk.Magufuli na kumwambia atakuwa Waziri wa Ujenzi na tukawa na makubaliano sitamhamisha, kikubwa ilikuwa ni kumuwezesha ili atekeleze wajibu wake, wote ni mashahidi kwa kazi ambayo jembe langu JPM aliifanya.
“Hata wakati naelekea kustaafu, jina lake nilikuwa nalo muda wote katika watu watano ambao nilitaka mmoja wapo awe Rais baada ya mimi, nilijenga hoja kwanini Magufuli, pamoja na mivutano mimi nilijenga hoja tu na hatimaye akawa Rais wetu nimeona leo niseme hili watu waelewe,” amesema Dk. Kikwete.
Aidha, amesema kwamba hatasoma tena ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani wa Hayati Rais Dk. Magufuli alizokuwa anawasaliana naye saa nane usiku.”Ukiona simu ujue yeye, siku moja nikamwambia hulalia? akanijibu nimejifunza kwako. Nafarijika sana ameacha alama ambazo zitadumu kwa kizazi cha sasa na kijacho, amegusa maisha ya wengi.
![]() |
Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete na mkewe Salma Kikwete wakiweka shada la maua kwenye kaburi la Hayati Rais Dk. John Magufuli |
“Amepata bahati ya kusifiwa akiwa hai, amepata bahati ya kuliliwa na kupendwa, tumeshuhudia umati wa watu kila mahali. Wana CCM tujiepushe kuimba nyimbo za adui zetu, tutafarakana na kugawanyika, naogopa kuendelea kumuelezea tusije kukufuru,” amesema.
Akizungumzia ukaribu wa kikazi baina yake na Hayati Rais Dk. Magufuli alisema alimtumainia na kwamba hata alipoona changomoto katika wizara yoyote wakati akiwa madarakani alimpeleka Hayati Rais Dk. Magufuli kwenda kupambana nazo.
Rais Mstaafu Kikwete pia alimhakikishia Rais Samia kuwa, yeye na wastaafu wenzake wana muda mwingi na wa kutosha akiwahitaji.
“Umetuhakikishia kuwa nchi iko katika mikono salama, hakuna kitakachoharibika. Baada ya matatizo ya Zanzibar, Rais Mkapa aliunda Tume niliyoongoza mimi, lakini nilikufahamu zaidi Mama Samia ulipokuwa Waziri wangu katika Wizara ya Muungano.
“Ulifanya vizuri sana, sina shaka muungano wetu utaendelea kudumu, hata hivyo kipaji chako cha uongozi kilionekana na kuchanua ulipokuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba na hapo ndipo tukaona unatosha kuwa kiongozi mkubwa, ndio maana mwaka 2015 tutakuchagua kuwa mgombea mwenza, ukashiriki kuomba kura na tukashinda na mwaka 2020 katika Uchaguzi Mkuu umefanya tena hivyo.
“Matarajio ya Watanzania unayajua, wewe sio mwanagenzi bali umepikwa umepikika, wewe ni mtu sahihi, tuna imani kubwa na wewe, ni mchapakazi. Mimi na wastaafu wenzangu tutakuwa pamoja nawe, uliomba tushirikiane, ukitutuma tutakuitika. Ukituita tutaitika, ukikaa kimya na sisi tutaendelea na mambo yetu,” amesema Rais Mstaafu Dk. Kikwete
Katika hatua nyingine Chama cha NCCR-Mageuzi, kimeeleza kuguswa na kifo cha Hayati Rais Dk. Magufuli na kimetoa wito kwa Watanzania kusimama pamoja ili kuyaenzi mema aliyoyafanya.
![]() |
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia akisaini kitabu cha maombelezo |
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia alipofika kutia saini kitabu cha maombolezo ya Hayati Rais Dk. Magufuli, katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
“Tukitumia hekima zetu vizuri tukawa na utulivu wa fikra tukasikilizana tutamsaidia sana Rais aliyepo sasa wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniua, mama yetu Samia Suluihu Hassan.
“Niseme tu buriani Rais Dk. Magufuli, sisi wote hapa duniani tunapita. Kifo ni mtihani na ni fumbo la uumbaji kwamba binadamu aliyezaliwa kuna kufariki pia,” amesema Mbatia.