SERIKALI YATOA TAHADHARI DHIDI  YA INFLUENZA, UVIKO-19, DENGUE NA KIPINDUPINDU

Date:

Share post:

RIPOTA PANORAMA

SERIKALI imetoa tahadhari ya kuwepo ongezeko la magonjwa ya mlipuko yakiwemo mafua makali ya Influenza, UVIKO-19, homa ya Dengue na Kipindupindu na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia hatua za kinga ili kudhibiti maambukizi.

Taarifa hiyo ya serikali imetolewa Februari 25, 2026 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe akieleza kuwa takwimu za ufuatiliaji zinaonesha kuwa kila mwaka katika kipindi cha miezi ya Novemba hadi Aprili kuna ongezeko la wagonjwa wa mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 duniani kote.

Amesema magonjwa hayo ya njia ya hewa husambaa kwa urahisi kupitia matone madogo yanayotoka kwa mtu mwenye maambukizi anapokohoa, kupiga chafya au kuzungumza. Dalili zake ni pamoja na homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua na uchovu.

Dk. Magembe amewataka  wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kufunika pua na mdomo wanapokohoa au kupiga chafya, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, kuepuka misongamano isiyo ya lazima, pamoja na kuvaa barakoa wanapokuwa na dalili au wanapokaribiana na mtu mwenye dalili za magonjwa hayo.

“Kuna uwezekano wa kuongezeka kwa maambukizi ya homa ya Dengue katika kipindi hiki cha mvua. Ugonjwa huo huenezwa na mbu aina ya Aedes anayezaliana katika maji yaliyotuama. Dalili zake ni homa kali ya ghafla, maumivu ya kichwa, viungo, misuli na maumivu nyuma ya macho,” amesema Dk. Grace.

Amewataka wananchi kutokomeza mazalia ya mbu kwa kufukia madimbwi ya maji, kuondoa maji yaliyotuama kwenye vyombo, matairi na makopo pamoja na kujikinga kwa kuvaa nguo ndefu na kutumia dawa za kufukuza mbu.

Kuhusu Kipindupindu, Mganga Mkuu amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kudhibiti ugonjwa huo na kutoripotiwa kwa mgonjwa mpya kwa takribani mwezi mmoja, bado kuna hatari ya maambukizi mapya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na uwepo wa maambukizi katika baadhi ya nchi jirani.

Amesisitiza umuhimu wa kuchemsha au kutibu maji ya kunywa, kunawa mikono kabla ya kula na baada ya kutoka chooni, kuosha matunda kwa maji safi, kutumia vyoo bora na kuhakikisha chakula kinaandaliwa katika mazingira safi na salama.

Amesema serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa magonjwa hayo na kutoa taarifa kwa umma kadri itakavyohitajika iwapo kutatokea mabadiliko au hatua zaidi za tahadhari zitahitajika kuchukuliwa.

About The Author

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

spot_img

Related articles

UCHUMI WA CHINA WAZIDI KUIMARIKA

BEIJING, China LICHA ya vita vya Marekani na Iran kuonekana kuitikisa dunia, China imeendelea kupiga hatua kubwa katika eneo...

SIKU 100 ZA RAIS MPYA WA VENEZUELA: MABADILIKO NA MASWALI MAPYA

CARACAS, Venezuela BAADA ya vikosi vya Marekani kumng’oa madarakani aliyekuwa Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro kwenye oparesheni ya Januari...

MAELFU YA FAMILIA SUDAN BADO WAKIMBIA VITA, HALI YA MAISHA YAZIDI KUWA MBAYA

MAELFU ya familia nchini Sudan bado wanalazimika kuyakimbia makazi yao, miji na hata mipaka ya nchi kufuatia vita...

ISRAEL YAENDELEA NA OPERESHEN DHIDI YA HEZBOLLAH NCHINI LEBANON

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Jeshi la nchi yake linaendelea na operesheni dhidi ya wanamgambo wanaoungwa...