DAR ES SALAAM:
NGOME ya Vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo imetoa mapendekezo manne kwa Serikali ikitaka maboresho katika mfumo wa uwezeshaji vijana kiuchumi kwa sababu changamoto zilizopo zinakwamisha vijana wengi kunufaika na mikopo na fursa za ajira.
Mapendekezo hayo yametolewa februari 23, 2026 na Mwenyekiti wa Ngome hiyo, Abdul Nondo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam.
Nondo amesema Ngome ya Vijana inapendekeza kuundwa kwa chombo maalumu kwa sheria ya Bunge chini ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana kitakachoitwa Wakala wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi nchini (TYEA).
Kwa mujibu wa Nondo, wakala huo utakuwa na jukumu la kuratibu utoaji na urejeshaji wa mikopo kwa vijana, kufuatilia miradi yao, kutoa ushauri wa kitaalamu, kuhamasisha na kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali za kiuchumi pamoja na kukusanya taarifa za fursa kutoka idara nyingine za serikali.
Amesema wakala huo unapaswa kuwa na Mkurugenzi Mkuu, Bodi pamoja na idara mahsusi zikiwemo Idara ya Sera, Utafiti na Mipango; Idara ya Uhamasishaji, Ufuatiliaji na Tathmini na Idara ya Ukopeshaji na Makusanyo. Aidha, uwe na ofisi katika ngazi ya mkoa na wilaya ili kurahisisha huduma kwa vijana.
Pendekezo la pili ni kutungwa kwa Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (Youth Development Fund Act) badala ya kuendelea kutegemea mwongozo wa mwaka 2022 pekee.
Nondo amesema kwa sasa mfuko wa maendeleo ya vijana hauna sheria ya Bunge inayoongoza uendeshaji wake, tofauti na mifuko mingine ya umma ambayo inaongozwa na sheria mahsusi. Alisisitiza kuwa kuwepo kwa sheria kutaimarisha uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika utoaji wa mikopo kwa vijana.
Katika pendekezo la tatu, Ngome ya Vijana ilitaka fedha za asilimia 4 za vijana kutoka katika makusanyo ya halmashauri zisitolewe na kusimamiwa moja kwa moja na halmashauri, bali ziwasilishwe kwenye mfuko wa maendeleo ya vijana chini ya wakala huo mpya.
Kwa mujibu wa Nondo, halmashauri ziendelee kukusanya asilimia 10 kwa makundi maalumu kama inavyoelekezwa na sheria lakini fedha za vijana zipelekwe katika mfuko mkuu wa kitaifa ili kuwa na usimamizi mmoja wenye ufanisi zaidi.
Pendekezo la nne linaitaka Wizara ya Maendeleo ya Vijana kujikita katika kuweka mifumo ya kisera, kiuratibu na kiusimamizi badala ya viongozi wake kujihusisha moja kwa moja na ugawaji wa mikopo mikoani.
“Waziri anatakiwa atengeneze mifumo imara ya kitaasisi itakayorahisisha uratibu, ufuatiliaji na uwajibikaji katika uwezeshaji wa vijana,” amesema Nondo.
