TERESIA MHAGAMA
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema uwepo wa vyanzo vingi vya nishati ya jotoardhi nchini Tanzania unaiwezesha kuviendeleza vyanzo hivyo ili viwanufaishe wananchi.
Waziri Ndejembi ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza kwenye Baraza la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Muungano wa Kimataifa wa Jotoardhi (Global Geothermal Alliance – GGA), uliofanyika Jijini Abu Dhabi, Falme za Kiarabu.
Alisema Serikali imeweka mipango ya uzalishaji wa umeme wa jotoardhi katika dira ya maendeleo 2050, sera ya taifa ya nishati ya mwaka 2015, malengo ya maendeleo endelevu ya dunia (SDGs) na mkataba wa nchi kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabia nchi (NDCs).
Waziri huyo alisema Tanzania kupitia Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TGDC) inaendeleza maeneo kadhaa ya kipaumbele ya jotoardhi, ikiwemo Ngozi (MW 70), Songwe (MW 5–38), Kiejo-Mbaka (MW 60), Natron (MW 60) na Luhoi (MW 5), huku lengo likiwa kuwa na mtambo wa kwanza wa kuzalisha umeme wa megawati 130 ifikapo 2030 utakaozalisha megawati 30.
aliwaalika wawekezaji kuja Tanzania kwani inaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, kuimarisha mifumo ya kisheria na kanuni ili kutoa uhakika wa uwekezaji, kuboresha michakato ya kupata leseni na vibali pamoja na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa data za jotoardhi.
Alisema bado inahitajika mikopo ya riba nafuu pamoja na ushirikiano na jumuiya za kimataifa pamoja na sekta binafsi ili kukabiliana na changamoto ya uendelezaji utafiti.
wazieri Ndejembi alisema Tanzania inakaribisha mataifa yaliyopiga hatua katika uendelezaji wa jotoardhi kuendeleza wataalamu wazawa katika masuala ya Jotoardhi.
Kwamba kutokana na uwepo wa Bonde la Ufa, Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya jotoardhi vinavyoweza kuzalisha megawati 5,000 za umeme.
“Kuna maeneo 52 yenye viashiria vya jotoardhi ndani ya mikoa 16,” alisema.
Akifungua mkutano huo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IRENA, Gauri Singh alisema nishati ya jotoardhi ni muhimu duniani kwani inatoa hakikisho la usalama wa nishati lakini mchango wake katika kuzalisha umeme diniani bado ni mdogo.
