KAMISHNA wa Uhifadhi, Mussa Nassoro Kuji na bingwa wa medali ya dhahabu wa mbio ndefu duniani mwaka 2025, Alphonce Simbu wamewasili Zanzibar na kupewa mapokezi ya heshima ya kiserikali.
Kamishna Kuji na Simbu waliwasili Zanzibar Desemba 31, 2025 kwa mwaliko maalumu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wa kushiriki bonanza maalumu la mazoezi ya viungo Zanzibar, 2026 lililofanyika Januari Mosi, 2026.
Bonanza hilo lilitanguliwa na matembezi yaliyoongozwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, yaliyoanzia Michenzani na kuishia Uwanja wa New Amani Complex.
Akizungumza wakati wa kuzindua bonanza hilo, Rais Mwinyi aliwapongeza washiriki wote kwa kushiriki michezo ambayo ni nguzo muhimu ya kuimarisha afya, umoja na mshikamano.
Kamishna Kuji alimshukuru Rais Mwinyi na serikali yake kwa mwaliko maalumu alioutoa kwa TANAPA na Simbu kwa sababu ziara hiyo itatoa hamasa kwa vijana wanariadha waliopo Zanzibar.
“Kipekee, ninamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele sekta ya utalii pamoja na michezo nchini,” alisema Kamishna Kuji.
Kwa upande wake Simbu, aliishukuru TANAPA kwa kumuwezesha kufika Zanzibar kwa mara ya kwanza na aliahidi kukuza zaidi kipaji chake ili aweze kuendelea kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Bonanza la mazoezi ya viungo Zanzibar liliandaliwa na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar na ZABESA.

