ARODIA PETER
SIMULIZI ya faru wawili wanaoshikilia rekodi ya kushiriki kufanya mapenzi mara nyingi zaidi kuliko faru wengine, ipo katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.
Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro imewaweka kwenye historia faru hao ili kuwaonesha watanzania na ulimwengu kwa ujumla umuhimu wa kuhifadhi faru ambapo idadi yake ndani ya hifadhi hiyo inazidi kuongezeka na kuvutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.
Faru hao wanatambulika kwa majina ya John na Fausta na ndiyo walioishi katika hifadhi hiyo kwa muda mrefu zaidi. Faru Fausta alizaliwa mwaka 1965 na kufa mwaka 2019 na Faru John alizaliwa mwaka 1978 na kufa mwaka 2016.

Hifadhi ya Ngorongoro.
Ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Faru John alijulikana kama bingwa wa kufanya mapenzi ama ‘dume la mbegu’ kwa sababu ya harakati zake za kuzunguka hifadhi yote akitafuta faru majike ili aweze kushiriki nao kufanya mapenzi huku upendo wake ukitawaliwa na wivu wa kupindukia.
Kwa upande wa Faru Fausta ambaye hakuwa na uwezo wa kushika mimba; wataalamu wanasema kuwa inawezekana aliishi muda mrefu kwa sababu hakuwa na msongo wa mawazo wakati wa kushika mimba, kulea watoto wala kunyonyesha zaidi ya ‘kula bata’ na kushiriki mapenzi na faru wenzake.
Sinmulizi ya faru hawa ni ya aina yake katika ulimwengu wa wanyama na wapo wanaosema ni maajabu yaliyogundulika katika Hifadhi ya Ngorongoro baada ya tafiti mbalimbali za kitaalamu kuhusu wanyama hao.

Faru John
Inaelezwa kuwa tabia nyingine ya Faru John ilikuwa ni utawala wa muda mrefu ndani ya hifadhi hivyo alikuwa chanzo kikubwa cha migogoro na kutaka kila faru jike awe naye peke yake.
Tofauti na Faru John, Faru Fausta ndiye faru pekee aliyeishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa muda mrefu wa miaka 54 na inasemekana pia amevunja rekodi ya dunia ya kuwa miongoni mwa faru wachache weusi walioishi miaka mingi.
Faru Fausta, licha ya kupandwa na madume mbalimbali ikiwemo Faru John, hakubahatika kupata mtoto na kwa mujibu wa wataalamu wa wanyama haikubainika ni kwa nini Faru Fausta katika umri wake wote wa miaka 54 hakujaaliwa uzazi.

Faru Fausta.
Inaelezwa kuwa, kisayansi faru anaweza asipate mtoto kutokana na kuwa na matatizo katika mfumo wa uzazi ikiwa ni pamoja na kuchelewa kupata mimba ambapo faru akiwa na hali hiyo katika umri unaotakiwa anakuwa na homoni kiasi kidogo za jike na hivyo kushindwa kupata mimba.
