
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limemaliza mwaka wa bajeti ya 2024/2025 kwa kishindo, likivuka malengo ya utekelezaji wa shughuli zake na ukusanyaji wa mapato kwa zaidi ya asilimia 100.
Rekodi za mwaka wa fedha wa 2024/2025 kuhusu mwenendo wa utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo, zinaonyesha kuwa lilivuka malengo ya ukusanyaji mapato kwa kukusanya asilimia 100.64.

Baadhi ya makamanda waandamizi wa TANAPA, wa kwanza kushoto ni ACC CPA Abdallah Kiwango, anafuatiwa na SAC Izumbe Mghana Msindai, SAC John Nyamhanga na mwisho ni SAC Godwell Meingataki.
Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Musa Nassoro Kuji anasema mafanikio hayo yamewezeshwa na mshikamano wa kikazi baina ya Bodi ya Wakurgenzi, Menejimenti na wafanyakazi wote wa Shirika hilo.

Kamishna wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Musa Nassoro Kuji.
Takwimu rasmi zilizowasilishwa bungeni na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana alipokuwa akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwenye Bunge la Bajeti, lililoketi Mwezi Aprili hadi Juni, mwaka huu zinaonyesha kuwa TANAPA lilikusanya Shilingi 433,612,732,617.63, fedha ambazo ni sawa na asilimia 100.64 ya lengo la makusanyo ya Shilingi 430,864,198,480.00 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi. Dk. Pindi Chana.
Aidha, katika kipindi hicho, TANAPA limefanikiwa kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea Hifadhi za Taifa, ambapo katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Aprili 2025, watalii 1,285,786 walitembelea Hifadhi za Taifa.
Kwa TANAPA, mwaka 2024/2025 ulikuwa mwaka wa kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuiimarisha Sekta ya Utalii kwa kuifanya kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa, sambamba na kutoa fursa kwa watanzania hususan vijana kushiriki kujenga uchumi wa nchi kupitia sekta ya utalii.

Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika kutekeleza hilo, mwaka 2024/2025 TANAPA liliajiri watumishi 550 wa kada mbalimbali hivyo kufikia asilimia 76.5 ya uhitaji wa watumishi wa shirika hilo.
Likikanyaga kila unyayo wa Rais Dkt. Samia Saluhu Hassan wa kuelekea kilele cha uimarishaji sekta ya utalii kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025, TANAPA liliwezesha watumishi 115 kupata mafunzo ya muda mrefu na watumishi 227 kupata mafunzo ya muda mfupi, hivyo kuwajengea uwezo zaidi wa utendaji kazi.

Askari wapya wa TANAPA wakiwa katika paredi ya kuhitimu mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi.
Aidha, lilijikita zaidi kwenye kuboresha uhifadhi, kuimarisha uhusiano na jamii na kuendeleza miundombinu ya utalii; hadi Aprili 2025, TANAPA lilifanya doria 36,411 na kukamata watuhumiwa 3,450 waliotenda makosa mbalimbali ya ujangili.
Wakati wa doria hizo, silaha 43 zilikamatwa na askari wa uhifadhi. Silaha hizo ni shortgun 10, magobore 33 na mitego ya nyaya 13,276 iliyokuwa ikitumika kuwatega wanyamapori.
Akizungumzia mafanikio hayo ya uhifadhi yaliyofikiwa na TANAPA kwa mwaka 2024/2025, Kamishna Kuji anasema yamewezeshwa na matumizi ya teknolojia za kisasa linayotumia hivi sasa ambayo imeboresha usimamizi na ulinzi wa wanyamapori.

Kamishna wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Musa Nassoro Kuji.
Kamishna Kuji anasema hivi sasa TANAPA linatumia visukuma-mawimbi, doria kwa kutumia ndege na uwekaji wa alama za masikio kwa faru.
Kwamba hatua hizi za kuboresha usimamizi wa uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori zilizochukuliwa na TANAPA zimeimarisha usalama wa hifadhi na kupunguza matukio ya ujangili.
Katika kuimarisha uhusiano kati ya Hifadhi za Taifa na wananchi waishio pembezoni hususan kupitia mpango wa ujirani mwema, TANAPA limechangia utekelezaji wa jumla ya miradi 47.
Miradi hiyo inahusisha sekta za afya ambayo ni minne, elimu 21, maji 10, ulinzi minane na uchumi minne.
Miradi husika ipo katika Wilaya za Bunda, Tarime, Kaliua, Kyerwa, Karatu, Arumeru, Serengeti, Bariadi, Kalambo, Mbarali, Kilwa, Ruangwa, Tunduru, Kigoma, Hai, Chato, Mwanga, Mpanda, Urambo, Biharamulo, Makete, Rufiji, Uvinza, Korogwe, Kondoa, Simanjiro, Babati, Liwale, Moshi, Rombo na Longido.
Utekelezaji wa miradi hiyo unahusisha elimu iliyotolewa kwa wananchi kuwawezesha kuboresha uhusiano na hifadhi na kudhibiti matukio mbalimbali ya uhalifu sambamba na jamii kupata taarifa zinazohusu uhifadhi.
Aidha, Shirika limekamilisha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji 18. Wilaya ya Tanganyika vipo 10 na Wilaya ya Uvinza vipo nane pamoja na kutoa mafunzo ya COCOBA kwa vikundi 36 vyenye wanachama 659 katika Wilaya za Bariadi, Tarime na Bunda kupitia Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Sambamba na hilo, TANAPA limehusika moja kwa moja kuendeleza vikundi vya kukuza uchumi katika Wilaya za Busega, Meatu na Itilima.
Kwa upande mwingine, TANAPA limeendelea kudhibiti mimea vamizi katika maeneo ya hifadhi ili kukabiliana na athari zinazosababishwa na mimea hiyo ndani ya hifadhi.

Askari wa TANAPA wakiondoa mimea vamizi hifadhini.
Hadi Aprili 2025, mimea vamizi iliondolewa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 2,400.23. maeneo ambayo mimea vamizi iliondolewa ni Hifadhi za Taifa Arusha, Burigi-Chato, Gombe, Ibanda-Kyerwa, Katavi, Kitulo, Ziwa Manyara, Mikumi, Mkomazi, Nyerere, Ruaha, Kisiwa cha Rubondo, milima ya Mahale na Rumanyika-Karagwe.
Vilevile katika kipindi cha mwaka 2024/2025 mpango wa usimamizi wa moto katika Hifadhi ya Taifa Nyerere umeandaliwa.
Hatua hii ya kuandaa mpango wa usimamizi wa moto katika Hifadhi ya Taifa Nyerere imesaidia kuhakikisha makazi na malisho ya wanyamapori yanaendelea kuwa ya asili kwa ajili ya kuimarisha mifumo ikolojia.
Kuhusu miundombinu, TANAPA limekarabati barabara za mchepuko zenye urefu wa kilomita 73.52. Katika Wilaya ya Serengeti jumla ya kilometa 27.82 zenye makalavati matano zimekarabatiwa na Wilaya ya Ngorongoro kilometa 46.7 zimekarabatiwa.
Kwa upande wa kuimarisha miundombinu ya uhifadhi na utalii, TANAPA limeendelea kufanya matengenezo ya mara kwa mara kwenye barabara zenye urefu wa kilomita 2,403.4.

Matengenezo ya barabara.
Katika Hifadhi za Taifa Arusha kilomita 97 zimefanyiwa matengenezo. Maeneo mengine ni Hifadhi ya Taifa ya Katavi kilomita 247, Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kilomita 73, Hifadhi ya Taifa Kitulo kilomita 26, Ziwa Manyara kilomita 85.4, Hifadhi ya Taifa Mikumi kilomita 87.5 na Hifadhi ya Taifa Mkomazi kilomita 116.5

Simba waliopo Hifadhi ya Taifa Rubondo.
Pia Hifadhi ya Taifa Ruaha kilomita 371, Kisiwa cha Rubondo kilomita 23, Hifadhi ya Saadani kilomita 118, Hifadhi ya Taifa Serengeti kilomita 682, Hifadhi ya Taifa Tarangire kilomiota 113, Hifadhi ya Taifa Burigi Chato kilomita 84, Hifadhi ya Taifa ya Ibanda-Kyerwa kilomita 43, Hifadhi ya Taifa Rumanyika-Karagwe kilomita 19 na Hifadhi ya Taifa Nyerere kilomita 218.
Aidha, ujenzi wa daraja la Matete katika Hifadhi ya Taifa Tarangire umefikia asilimia 68 ya utekelezaji.

Uwanja wa ndege wa Soronera ulio katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
TANAPA pia limekamilisha ukarabati mkubwa wa viwanja vya ndege vitatu vya Lobo, Kusini na Seronera katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Pia limeendelea kufanya ukarabati wa mara kwa mara kwenye viwanja sita vya ndege ambavyo ni kiwanja cha ndege cha Hifadhi ya Taifa ya Saadan, Mkomazi kimoja, Ruaha kimoja, Serengeti viwili na Katavi kimoja ili kuimarisha usalama wa usafiri wa anga na kuvutia watalii zaidi kutembelea hifadhi hizo.

Uwanja wa ndege ulio katika Hifadhi ya Taifa Ruaha.
Kazi nyingine zilizofanywa na TANAPA ni kuendelea na ujenzi wa hoteli yenye hadhi ya nyota tatu katika eneo la Rubambagwe, wilayani Chato chini ya Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo na hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 70 ya utekelezaji.

Ujenzi wa hoteli yenye hadhi ya nyota tatu eneo la Rubambagwe, wilayani Chato chini ya Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondoumefikia asilimia 70.
Pia TANAPA limeendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa mabanda matatu ya wageni (cottages) katika eneo la Horombo Hut yenye uwezo wa kubeba vitanda 90 na ujenzi wa vyoo vya wageni katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro, banda moja katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, vibanda vitano vya kupumzikiawageni (visitor’s sheds) katika Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla na kuweka samani katika hosteli ya Hifadhi ya Taifa Saadani.
TANAPA limejenga malango saba ya kuingilia wageni ambapo katika Hifadhi ya Taifa Serengeti yapo mawili, Tarangire moja, Nyerere mawili, Ibanda-Kyerwa moja na Mkomazi moja.

Idadi ya watalii wanaotembelea Hifadhi za Taifa imeongezeka sana.
Miundombinu hii imelenga kuboresha huduma za utalii na ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande mwingine, TANAPA limejenga kituo cha taarifa katika eneo la Seronera kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Kama lilivyoelekezwa na Rais Dkt. Samia kujikita kwenye kupanua wigo wa shughuli za utalii, TANAPA limeendelea na juhudi na kupanua wigo wa shughuli za utalii kwa kuibua na kuendeleza mazao mapya ya utalii, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa mpira wa gofu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti ambao umefikia asilimia 60 ya utekelezaji wake ikiwa ni ujenzi wa jumla ya mashimo 18, visima viwili, mabwawa mawili, miundombinu ya maji na umeme.

Uwanja wa gofu unaojengwa kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Aidha, ujenzi wa daraja la juu lenye urefu wa kilometa moja katika Hifadhi ya Taifa Milima Udzungwa umekamilika kwa asilimia 67.
Tayari TANAPA limeanzisha utalii wa kuogelea kwenye chemchem ya maji moto katika Hifadhi ya Taifa Ruaha; utalii wa kuruka kwa ndege ndogo katika Hifadhi za Taifa za Kilimanjaro, Arusha na Ziwa Manyara na utalii wa kulala nje kuangalia nyota katika Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara.
Upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuanzisha utalii wa faru katika Hifadhi za Taifa za Burigi-Chato na Mikumi unaendelea.
TANAPA limeendelea kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi kwa kurusha matangazo ya moja kwa moja, kushiriki matukio ya utalii na kutumia mitandao ya kijamii ili kuvutia watalii kutembelea Hifadhi za Taifa.
TANAPA pia limekamilisha ujenzi wa nyumba za watumishi 30 katika Hifadhi za Taifa mbalimbali.
Kati ya nyumba hizo, nane zipo Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Hifadhi ya Taifa Nyerere 12, Hifadhi ya Taifa Ruaha nyumba tano, Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato nyumba tatu, Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika-Karagwe nyumba moja na Milima ya Mahale nyumba moja.

Hifadhi ya Taifa Mkomazi.
Sambamba na hilo, mifumo mipya ya nishati ya jua imewekwa katika vituo 12 vya askari kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti na utafiti wa maji (hydrological survey) katika vituo viwili vya askari umefanyika pamoja na kukarabati visima vinne vya mafuta katika Hifadhi ya Taifa Nyerere.
