RIPOTA PANORAMA
SASA imethibitika pasipo shaka kuwa mchanga wa ajabu hapa duniani ambao huhama kutoka sehemu moja hadi nyingine, upo Tanzania pekee.
Kuthibitisha hili, watu wote duniani wanaotaka kuuokota au kuuona mchanga unaohama wamekuwa wakifunga safari kwenda Bonde la Olduvai Gorge lililopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kwenda kukata kiu yao.
Mchanga huo ni maajabu mengine ya dunia yanayopatikana kwenye hifadhi hiyo ya kipekee Afrika na duniani kwa ujumla. Na mtalii yeyote wa ndani ama wa nje akipanga safari ya kwenda Ngorongoro, basi asitarajie kuona wanyama pori tu.
Kwa kila Mtanzania, ukipata nafasi fika eneo la mashariki la uwanda wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, karibu na Olduvai Gorge ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Olduvai Gorge
Ni katika eneo hilo, ambako utastajabu kuona maajabu ya matuta makubwa ya mchanga unaohama.
Mchanga huu huhama kwa mita 15 hadi 29 kwa mwaka bila kubadili umbo lake la mwezi mchanga ukiwa umejikusanya pamoja bila kuacha mabaki nyuma.
Mchanga huo hupeperushwa na mawimbi ya upepo kuelekea eneo la magharibi hadi kuvuka eneo la tambarare.
Tukio hili ni mojawapo ya mambo ya kuvutia na kukuacha kinywa wazi uwapo ndani na eneo la Ngorongoro nchini Tanzania.
Mchanga huu wenye rangi nyeusi umetokana na madini ya chuma na majivu yaliyotokana na mlipuko wa Volcano kutoka Mlima Oldoinyo Lengai.

Mlima Oldonyo Lengai.
Mchanga huu ambao husogea kwa kasi ya takribani mita 15–29 kwa mwaka, tuta lake lina urefu wa mita tano na upana wa mita 100.
Kuhama hama huku kumesafisha sehemu nyepesi za majivu kutoka eneo hilo, na kuacha nyuma madini ya chuma yenye rangi nyeusi ambayo yaliunda mchanga huo. Ukilinganisha na mchanga wa eneo lingine, rangi ya mchanga uhamao ni mweusi

Mchanga unaohama
Tuta la mchanga hufikia urefu wa mita tisa na kunyoosha urefu wa mita 100 kwenye mikondo yake.
Unaweza ukahisi kuwa mchanga huo hauendi sehemu yoyote kwani huhama kwa njia ya mtiririko.
Utagundua uhamaji wake kutokana na alama za mawe zilizowekwa eneo hilo, zikionesha mahali mchanga ulipo kwa wakati huo, na wapi ulikuwepo hapo kabla.
Mchanga huo hujumuisha majivu ya volkeno, yenye nguvu ya sumaku na yenye uwezo wa kushikilia chembechembe za mchanga pamoja.
Wageni wanaofika eneo hili, hustaajabu sumaku ya mchanga huu ukinatisha simu zao za mikononi na hata vitu vingine vyenye asili ya chuma.
Hayo ndiyo maajabu ya Hifadhi ya Ngorongoro. Ukitaka kujua zaidi kuhusu mchanga huu tembelea Hifadhi ya Ngorongoro uone kwani fahari ya macho ni kuona na fahari ya macho haifilisi duka.
