RIPOTA PANORAMA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji amewataka wafanyakazi wa Shirika la Hifadhi za Taifa, (TANAPA) kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia utu ili kuboresha ustawi wa jamii.
Akizungumza na wafanyakazi wa shirika hilo makao makuu ya TANAPA hivi karibuni, Waziri Kijaji aliwataka kuzingatia kauli mbiu ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kazi na utu wanapotekeleza majukumau yao ya uhifadhi.
Alisisitiza kuwa wafanyakazi wa shirika hilo wanapaswa kuwa wabunifu kutangaza vivutio vya utalii ili serikali iweze kufikia lengo lake la kuongeza watalii wanaotembeela Hifadhi za Taifa hadi kufikia milioni nane ifikapo 2030.

Akimkaribisha kuzungumza na watumishi hao, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Mussa Nassoro Kuji alitoa taarifa ya maendeleo ya miundombinu na ongezeko la watalii na mapato yatokanayo na utalii.
Kamishna Kuji alisema kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26 Hifadhi za Taifa zilitembelewa na watalii 62,468 ikiwa ni zaidi ya lengo la watalii 61,742 na kwa wastani ni ongezeko la asilimia 1.18.
“Kwa idadi hiyo, mapato yaliyokusanywa ni shilingi bilioni 3.9 sawa na ongezako la asilimia 15.44,” alisema Kamishna Kuji.
