Hassan Silayo
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amesema ole wao wezi wa mali za wananchi kwa sababu mkono wa sheria hautawaacha salama.
Akizungumza hivi karibuni kwenye kongamano la mwaka la wamachinga, madreva pikipiki na bajaji, jijini Dar es Salaam, alisema waliopora mali za raia ikiwemo ardhi warudishe kabla hawajafikiwa na mkono wa sheria.
Alisema hakuna sababu kwa wananchi kukaa kimya wanapoonewa bali watoe taarifa kwani hakuna mbabe mbele ya Serikali.
Alisisitiza kuwa watanzania wote wana haki sawa, hivyo hakuna mtu mwenye ruhusa ya kuchukua mali au kitu chochote cha mtu mwingine hivyo atakayebainika achukuliwe hatua.
Kauli hiyo ya Nchemba ilikuja baada ya wananchi kulalamika kuchukuliwa mali zao ikiwemo ardhi.
Akizungumza kuhusu hoja zilizowasilishwa na wamachinga na waendesha pikipiki na bajaji, alisema amezipokea na serikali itazifanyia kazi.
