![]() |
Korosho. Moja ya mazao yanayonunuliwa na kuuzwa na nje na Kampuni ya Somani Agro Export Limited ya Dar es Salaam |
NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI mbili za mkoani Dar es Salaam zinazojihusisha na biashara ya kununua na kuuza mazao ya aina mbalimbali ndani na nje ya nchi zinadaiwa kucheza mchezo mchafu wa kukwepa kulipa kodi.
Kampuni hizo ni Somani Agro Export Limited yenye ofisi zake eneo la Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mazao ya Nje (EPZA) Mabibo Extenal, Ubungo na Paramount Commodities Limited ambayo haina ofisi na badala yake inaendesha shughuli zake za biashara ndani ya Kampuni ya Somani.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na Tanzania PANORAMA Blog umebaini kuwa Kampuni ya Paramount iliyoripotiwa awali kuendesha shughuli zake kinyemela ndani ya eneo la EPZA na kutuhumiwa kukwepa kulipa kodi, kukiuka sheria za ajira, kuajiri wafanyakazi wa kigeni wasiokuwa na vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini pamoja na kunyanyasa wafanyakazi, inafanya shughuli zake ndani ya Kampuni ya Somani.
Imedaiwa kuwa Somani imekuwa ikinufainika na malipo ya fedha ambazo Paramount ilipaswa kulipia pango la ofisi, kodi mbalimbali za Serikali ikiwemo mitambo ya kusafishia mazao na kukwepa sheria za ajira zinazowalinda wafanyakazi pamoja na kupata stahiki zao kwa kutokuwa na ofisi inayotambulika.
Kwamba Paramount imekuwa ikiilipa Somani sehemu ya fedha ambazo ilipaswa kuzilipa kama kodi serikalini kutokana na biashara ya kununua, kusafirisha na kuuza mazao nje ya nchi, malipo ya ofisi, malipo ya pensheni za wafanyakazi na stahiki zao pamoja na kutunza na kutumika kwa mitambo ya kusafisha mazao ambayo ni mali ya Paramount.
Mmoja wa maafisa wa Kampuni ya Somani aliyezungumza na Tanzania PANORAMA Blog baada ya kuibuka kwa malalamiko ya wafanyakazi wa Kampuni Paramount alithibitisha kuwa ni kweli kampuni hizo zinacheza mchezo mchafu lakini zimekuwa zikifanya hivyo ili kupunguza mzigo wa kulipa kodi.
Aliilamu Kampuni ya Paramount kwa kuwa na mgogoro na wafanyakazi wake ambao wametoa siri za makampuni hiyo.
Tanzania PANORAMA Blog bado haifanikiwa kupata kauli ya Kampuni ya Somani kuhusu madau hayo baada ya mwito wa simu ya kampuni hiyo kutopokelewa.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Paramount, Dhaval Patel ambaye alihojiwa awali na Tanzanua PANORAMA Blog kuhusu kampuni yake kuhusika na mchezo huo alielekeza msemaji wake atoe majibu.
Msemaji wa Paramount, Evans Kisavio alipoulizwa kwanza alisema hayuko kwenye nafasi nzuri ya kuzungumza hivyo atafutwe baadaye, alipotafutwa badaaye alisema yupo harusini lakini alipobanwa alisema yeye siyo msemaji wa kampuni hiyo bali atafutwe Dhaval amalize matatizo yake mwenyewe.