RIPOTA PANORAMA
SERIKALI ya Rais Samia Suluhu Hassan, imefanikiwa kuvuka malengo ya ukusanyaji mapato katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2021/22.
Mafanikio hayo ya Serikali ya Rais Samia yamefikiwa kwa ukusanyaji kodi, makusanyo yasiyotokana na kodi, makusanyo ya Serikali za Mitaa yakijumuishwa na misaada, mikopo ya ndani, mikopo ya nje yenye masharti nafuu na mikopo ya nje isiyo ya masharti nafuu.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ya 2021/22; Serikali ya Rais Samia imekusanya Shilingi trilioni 37,992, juu ya mpango wake wa kukusanya Shilingi trilioni 36,681.
Ripoti ya ukaguzi wa CAG kuhusu maandalizi na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka unaomalizika inaonyesha kuwa, Serikali ya Rais Samia ilipanga kukusanya na kutumia Shilingi trilioni 36,681 lakini kiasi hicho kiliongezeka baada ya kupokea mkopo wa Shilingi trilioni 1,311 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Anasema mkopo huo ulitolewa kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kukabiliana na hali ya uchumi baada ya kupungua kwa ugonjwa wa UVIKO 19, hivyo kufanya bajeti ya Serikali kutuna zaidi ikielekeza fedha hizo za mkopo kwenye sekta za afya, elimu, maji utalii, hifadhi ya jamii, nishati na uwezeshaji wa kiuchumi.
Akichambua mwenendo wa utendaji wa bajeti, CAG anasema 2021/22 Serikali ya Rais Samia ilikusanya Shilingi trilioni 38,298 ambazo ni zaidi ya bajeti ya Shilingi trilioni 37,992 ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa 2020/21 ambacho ni Shilingi trilioni 31,326.
Umulikaji wa makusanyo ya ndani wa CAG unaonyesha kuwa, makusanyo ya kodi ya Tanzania Bara yalikuwa Shilingi trilioni 20,945, sawa na asilimia 96 ya bajeti ya Shilingi trilioni 21,778, hivyo hesabu za makusanyo ya Serikali ya Rais Samia kusomeka kuwa haikukusanya Shilingi bilioni 883.
Anasema makusanyo hayo yana ongezeko la Shilingi trilioni 3,347 ambazo ni sawa na asilimia 19 ya ongezeko la makusanyo, ikilinganishwa na Shilingi trilioni 17,598 za mwaka 2020/21.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere
Ripoti inazungumzia pia makusanyo yasiyotokana na kodi kutoka kwa wizara, idara na sekretarieti za mikoa na taasisi nyinginezo yaliyofikia Shilingi trilioni 2,709, sawa na asilimia 89 ya bajeti iliyoidhinishwa ya Shilingi trilioni 3,050, ikipungua Shilingi bilioni 341 ambayo haikukusanywa.
“Ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi trilioni 2,023 ya mwaka 2020/21, nilibaini ongezeko la makusanyo yasiyotokana na kodi kwa Shilingi bilioni 686, sawa na ongezeko la asilimia 34,” CAG anasema.
CAG anaendelea kwa kuangalia ongezeko la makusanyo ya Shilingi bilioni 194 kutoka Serikali za Mitaa ambako jumla ya makusanyo yalikuwa Shilingi bilioni 892, sawa na asilimia 103 ya bajeti iliyoidhinishwa ya Shilingi bilioni 864.
Kuhusu misaada CAG anasema; “mwaka wa fedha 2021/22 misaada ya Shilingi trilioni 1.305 sawa na asilimia 115 ya bajeti ya 1,138 ilikusanywa hivyo kiasi cha Shilingi bilioni 167 zilikusanywa zaidi.”
Anasema mikopo ya ndani ikiwa ni pamoja na ankara za hazina, hati fungani na ufadhili wa ndani zilikusanywa Shilingi trilioni 6,489 ambazo ni juu ya bajeti iliyoidhinishwa ya Shilingi trilioni 4,989.
Kwa upande wa mikopo ya nje yenye masharti nafuu, anasema zilikusanywa Shilingi trilioni 4,149 ikiwa ni juu ya bajeti iliyoidhinishwa ya Shilingi trilioni 3,128 na mikopo ya nje isiyo na masharti nafuu, zilipatikana Shilingi trilioni1,809.