RIPOTA PANORAMA
WAZIRI wa Nishati, January Makamba “amekimbia.” “Amekimbilia” mbali na kujiweka kando na deni la Dola za Marekani milioni 148.4 pamoja na riba, ambazo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linadaiwa na Benki ya Standard Chartered Hong Kong.
“Akikimbia” mapema leo baada ya kufikiwa na Tanzania PANORAMA Blog kupitia simu yake ya kiganjani na kuulizwa kuhusu deni hilo. Waziri Makamba, kwa maneno yake mwenyewe, amesema; “unauliza maswali ya mambo yote ambayo yamefanyika mimi nikiwa sipo wala Rais Samia (Suluhu Hassan) akiwa hayupo. Ulikuwa wapi kuyauliza kipindi cha nyuma kwa wahusika wenyewe?”
Tanzania PANORAMA Blog ikamkumbusha kuwa yeye ndiye waziri aliyeko ofisini sasa na tishio la Tanesco kupoteza mamilioni hayo ya Dola za Marekani limeibuliwa sasa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwenye ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2021/22 na hapo akaruka mbali zaidi, akisema;
“Hapana kaka, tafadhali tafuta kauli za waliyoyafanya haya mambo. Mimi niulize mambo ya sasa tuliyofanya wakati wetu ambayo ninawajibika nayo,” alisema Waziri Makamba na alipoulizwa msimamo wake kama hatahusika kwa namna yoyote akiwa kiongozi wa Wizara ya Nishati kwenye ulipaji wa deni hilo kwa kile anachosema wakati mkataba unasainiwa hakuwepo ofisini, Waziri Makamba hakutoa kauli tena.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG aliyoikabidhi kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Machi, mwaka huu, IPTL na Tanesco walisaini mkataba kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha umeme lakini wakati wa kusambaza umeme huo, kuliibuka mgogoro wa kiwango cha malipo uliosababisha kufunguliwa kwa akaunti ya Escrow, mwaka 2006.
CAG anasema katika ripoti yake kuwa, mwaka 2012 Tanesco na IPTL walimaliza mgogoro wao na fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow zilipelekwa kwa Kampuni ya Pan African Power Solution (PAP) ambayo ni mmoja wa wanahisa wa Kampuni ya IPTL.

“Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited ilikuwa na mkopo Benki ya Standard Chartered Hong Kong, ambao kwa upande wao wanadai kuwa Kampuni ya Pan African Power Solutions Tanzania, walitumia baadhi ya fedha kutoka kwenye akaunti ya Escrow kulipa hisa za Kampuni ya VIP katika Kampuni ya Independent Power Tanzania baada ya kutimiza wajibu wa malipo katika Shirika la Umeme Tanzania chini ya PAP na kulipa mkopo.
“Kwa sababu hiyo, mwaka 2016, kituo cha kimataifa cha kutatua migogoro ya uwekezaji kiliamua kuwa Shirika la Umeme Tanzania, lazima liilipe Benki ya Standard Chartered Hong Kong, Dola za Marekani milioni 148.4 pamoja na riba.
“Kufuatia uamuzi huo, mnamo mwaka 2018, Serikali iliwasilisha kesi ya madai katika Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya Kampuni ya Independent Power Tanzania ili kutekeleza hati ya fidia iliyotiwa saini tarehe 27 Oktoba, 2013 ambayo inalinda hatua ya Serikali kutoa fedha kwenye akaunti ya Escrow kutokana na madai ya wahusika wa nje.
“Uamuzi wa tarehe 1 Machi, 2021 ulikuwa kwa upande wa Serikali na Kampuni ya Independent Power Tanzania ilikubali kuilipa Serikali, Dola za Marekani milioni 148.4 mnamo tarehe 1 Machi, 2021, hata hivyo hadi wakati wa ukaguzi, mwezi Disemba 2022, IPTL hawakuwa wamelipa kiasi kinachodaiwa,” anaeleza CAG katika ripoti yake.
CAG anaeleza zaidi kuwa iwapo Serikali italipa madai ya Benki ya Standard Chartered Hong Kong, kama ilivyoamriwa na kituo cha kimataifa cha kutatua migogoro bila kulipwa fedha inazoidai Kampuni ya IPTL, itakuwa imefanya malipo mara mbili.
Akifafanua anasema Serikali itakuwa inalipa mara mbili mamilioni hayo ya Dola za Marekani kwa sababu ilikwishalipa malipo ya umeme kwenye akaunti ya Escrow na Kampuni ya IPTL iliahidi kupitia hati ya kulinda madai ambayo iliiondolea Serikali ya Tanzania madai ya aina yoyote kutoka Benki ya Standard Chartered Hong Kong.
CAG anaeleza mashaka yake dhidi ya Kampuni ya IPTL kuchelewa kulipa deni inalodaiwa na Serikali kuwa kunaichelewesha kupata fedha za kuilipa Benki ya Standard Chartered Hong Kong na hivyo kusababisha kuongezeka kwa mkopo kwa sababu ya riba inayoongezeka.

Waziri wa Nishati, January Makamba
Anasema hilo linachafua sifa ya nchi katika jukwaa la kimataifa na anaishauri Serikali na Tanesco kuchukua hatua dhidi ya IPTL ili ikamalishe malipo inayodaiwa na Serikali.
Wakati hayo yakiendelea, Tanzania PANORAMA Blog imedokezwa kuwa kesi iliyofunguliwa na Serikali dhidi ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Symbion kudai malipo ya kodi ya ongezeko la mtaji, imefutwa kinyemela huku kukiwa na tuhuma za kutumika rushwa katika mchakato huo.
Katika hilo, majina kadhaa yanatajwa kuhusika na mpango wa kufuta kesi hiyo huku mmoja wa wafanyakazi wa Kampuni ya Symbion akidaiwa kuwa mmoja wa wakurugenzi wa Tanesco.
ENDELEA KUPERUZI TANZANIA PANORAMA BLOG ILI KUPATA HABARI ZA UHAKIKA.