Wednesday, March 12, 2025
spot_img

K – VANT FEKI ZANASWA DAR, KACHERO WA POLISI KILWA ROAD ASWEKA NDANI MWANDISHI

 

 

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

WATU sita wanaotuhumiwa kujihusisha na utengenezaji na uuzaji wa pombe kali aina ya K Vant wamekamatwa.

Imeelezwa kuwa watuhumiwa hao walikamatwa katika oparesheni maalumu iliyofanywa na makachero wa polisi baada ya kuombwa na menejimenti ya Kampuni ya Mega Beverages ambayo maofisa wake wameshindwa kuthibiti vitendo vya hujuma dhidi ya kampuni.

Taarifa za uhakika zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog kutoka vyanzo vya kuaminika vilivyo ndani ya Kampuni ya Mega Beverages ambayo ni watengenezaji wa kinywaji hicho zimedai kuwa watuhumiwa hao hutengeneza kinywaji hicho kienyeji kwa sababu hawana utaalamu na vifaa vya kutosha hivyo pombe wanayoitengeneza si salama kwa wanywaji.

Inadaiwa kuwa, menejimenti ya Kampuni ya Mega Beverages yenye makao makuu yake jijini Arusha iliwasilisha kwa makachero wa polisi ambao haijafahamika vituo vyao vya kazi ombi la kuwasaka wahalifu hao kwa ahadi ya kuwapatia donge nono.

Kwamba makachero hao wakishirikiana na msiri mkuu wa mmiliki wa kiwanda hicho (jina lake kapuni) walifanikiwa kuwanasa watuhumiwa wakiwa na K Vant feki na baada ya kuhojiwa walimtaja mmoja wa maofisa wa juu wa kampuni hiyo kuwa ndiye kinara wa uhalifu huo.

“Kampuni imekuwa ikihujumiwa kwa muda mrefu sana na baadhi ya wateja wamekuwa wakiilalamika pombe hii kuwasababishia matatizo ya kiafya. Uchunguzi uliofanywa na kampuni ulibaini kuwa kuna K Vant zinazotengenezwa kienyeji ambazo ndizo zinawasababishia wanywaji matatizo ya kiafya.

“Kazi ya kuwasaka watu wanaohujumu kampuni alipewa bosi (anamtaja jina) lakini kwa muda mrefu amekuwa akifanya uchunguzi pasipo kufanikiwa kumnasa hata mtu mmoja anayejihusisha na vitendo hivyo. Mwishowe bosi akashtuka akaamua kumpa hiyo kazi msiri wake.

“Msiri wa bosi akawafuata polisi akawaomba wasaidie kuwasaka wahalifu hao na kwamba atawapa zawadi wakifanikiwa kuwanasa wakiwa na vidhibiti, ndiyo polisi wakaingia kazini, muda mfupi tu wakawanasa na pombe zao feki.

“Ajabu sasa hao jamaa waliokamatwa walipohojiwa wakamtaja bosi anayesimamia ofisi ya Dar es Salaam kuwa ndiye bosi wao katika uhujumu huo. Ngoma ikawa ngumu hapo na mpaka muda huu mwenye kampuni hajaambiwa kuhusu hizi taarifa kwa sababu hayupo yupo Nairobi,” alisema mmoja wa watoa taarifa.

Taarifa zaidi zilieleza kuwa watuhiumiwa hao walifikishwa katika kituo kidogo cha polisi cha Kilwa Road na kufunguliwa jalada lenye nambari KR/IR/9140/2021 ambako walizuiliwa kwa zaidi ya siku tatu kabla ya kudhaminiwa.

Hata hivyo, baada ya taarifa za kukamatwa kwa watu hao kuifikia Tanzania PANORAMA ambayo ilianza kufuatilia  kwa kumtafuta mmoja wa meneja wa kampuni hiyo Mkoa wa Dar es Salaam (jina tunalihifadhi kwa sasa), kachero kiongozi wa kituo kidogo cha polisi cha Kilwa Road, Ntirungika Sembwa aliingilia kati kuzuia waandishi kutekeleza wajibu wao.

Mwandishi wa Tanzania PANORAMA Blog alimpigia simu meneja anayehusishwa na sakata hilo na kumuuliza kuhusu kukamatwa kwa watu hao na pia jina lake kutajwa kuwa kiongozi wa mtandao wa watu waliokamatwa na yeye alihoji ni nani aliyempatia mwandishi taarifa hizo.

“Brother kwani wewe nani amekupa taarifa hizo? Kwani umefika hapa polisi wewe? Naomba nambie kama umeongea na polisi yeyote akakupa taarifa hizo kwa sababu mimi ndiye ninayeshughulikia suala hili,” alisema.

Mwandishi alipokataa kutaja chanzo chake cha habari, meneja huyo aliomba kukutana naye kwa maelezo kuwa atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuzungumza akijua anazungumza na nani badala ya kuongea kwa simu jambo ambalo mwandishi aliliafiki.

Meneja huyo alikutana na ripota wa Tanzania PANORAMA, akiwa ameambatana na kachero kiongozi wa idara ya ukachero wa kituo kidogo cha polisi cha Kilwa Road, Sembwa ambaye alimuweka chini ya ulinzi kabla ya kwenda kumsweka rumande kwa muda wa siku tatu huku akimtaka  ataje chanzo chake cha habari.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Richard Ngole alipoulizwsa jana kuhusu kukamatwa kwa watu hao alisema hana taarifa  na kuahidi kufuatilia.

Tanzania PANORAMA inaendelea kufuatilia sakata hili.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya