Wednesday, March 12, 2025
spot_img

FAILI LA MTUHUMIWA ULANGUZI WA UMEME LATOKA KWA DCI KWENDA KWA DPP

Jengo linalomilikiwa na mfanyabiashara Ugur Gurses lililopo Mtaa wa Livingstone, Kariakoo. wakazi wanaoishi ndani ya jengo hili wanalalamika kulanguliwa umeme.

 

RIPOTA PANORAMA

0711 46 49 84

FAILI lenye tuhuma zinazomkabili mfanyabiashara Ugur Gurses za ulanguzi wa umeme, kufanya biashara ya umeme bila kuwa na leseni ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) sasa limefikishwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) baada ya kutoka kwa Mkurugenzi wa Makosa wa Jinai (DCI)

Akizungumza jana na Tanzania PANORAMA Blog, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Dar es Salaam (PRO), Pius Hilla alisema faili hilo limetoka kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) na limepelekwa ofisini kwa DPP, Dodoma kwa ajili ya hatua zaidi.

“Tulipozungumza mara ya kwanza nilikwambia kwamba nitalifuatilia faili hilo, nililifuatulia na kubaini kwamba lilikuwa njiani kutoka kwa DCI kwenda kwa DPP Dodoma, halijaletwa ngazi ya mkoa kwa ajili ya kulishughulikia, tunasubiri maelekezo ya DPP, akilishusha kwetu tutaendelee na taratibu zinazohusika,” alisema Hilla,  

PRO Hilla alizungumza na Tanzania PANORAMA Blog mwishoni mwa Oktoba kuhusu suala hilo na kueleza kuwa shauri hilo halijafika mikononi mwake lakini analifuatilia kwenye ofisi za mikoa zinazounda Kanda ya Dar es Salaam ili lifikishwe kwake na kuahidi kuwa atatoa kauli yake.

“Iko hivi, unajua tangu mwezi Agosti mwaka huu, DPP aliunda mikoa ya kimashtaka, kuna ofisi za mashtaka za mikoa ya Kinondoni, Ilala na Temeke. Hizi zinaunda Kanda ya Dar es Salaam na mimi ni kiongozi wa kanda. Sasa hapa mikononi mwangu hilo faili halijafika.

“Naomba muda nifuatilie, acha nifuatilie lipo wapi hilo faili. Wewe naomba nitafute jumatatu mchana nitakuwa na jibu, nitatoa kauli jumatatu kuhusu suala hili,” alisema Hilla.

Awali, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu alipozungumza na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu suala hilo naye alisema atafuatilia faili la shauri hilo ambalo lilikuwa halijafika mezani kwake.

DPP Mwakitalu alisema upo uwezekano faili hilo liliwasilishwa katika ofisi ya kanda na alielekezaTanzania PANORAMA Blog kuwasiliana na ofisi hiyo kujua kama lilipokelewa huko na namna lilivyofanyiwa kazi.

“Faili la shauri hilo halijafika ofisini kwangu, inawezekana EWURA waliliwasilisha katika ofisi za kanda, haya mambo mengine yafanyika huko ofisi za kanda lakini nakushukuru umeniambia, nalifuatilia,” alisema DPP Mwakitalu.

Gurses anatuhumiwa kwa ulanguzi wa umeme, kufanya biashara ya umeme bila kuwa na leseni ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji na kukataa kupokea karipio la kisheria la EWURA la kutojihusisha na vitendo vya uvunjivu wa sheria,.

EWURA ndiyo wanaomtuhumu Gurses, raia wa Uturuki na mmiliki wa Kampuni ya Adamas Group yenye ofisi zake Karioakoo, Dar es Salaam inayojihusisha na biashara ya nyumba; kufanya biashara ya kuuza umeme kinyume cha sheria akiwa hana leseni ya mamlaka hiyo na kuuuza kwa bei ya juu.

Akizungumzia tuhuma hizo, Meneja Mawasiliano wa EWURA, Titus Kaguo aliiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa Gurses ana makosa mawili, la kwanza ni kuuza umeme bila kuwa na leseni ya EWURA na kosa la pili ni kuuza umeme kwa bei ya juu.

Alisema EWURA baada ya kubaini makosa hayo kwa Gurses ilimpelekea karipio la kisheria lakini alikataa kulipokea hivyo imelifikisha shauri hilo kwa DPP ambaye ana nguvu za kisheria na pia ana vyombo vya dola kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.

“Huyu mtu ana makosa yafuatayo, 1) kuuza umeme wakati hana leseni ya EWURA, 2) kuuza umeme kwa bei ya juu. Tulimpelekea ‘complaince order’ karipio la kisheria na alikataa kupokea.

“Katika hali kama hii, sheria inatutaka tumpelekee DPP ambaye ana vyombo vya dola kama polisi ili ampeleke mahakamani. DPP analifanyia kazi na tumeishakaa na DPP juu ya hili shauri.

“Tunasubiri hatua za DPP. DPP ana taratibu zake na anaweza kufanya uchunguzi kabla ya kuchukua hatua. Sasa fuatilia kwa DPP ‘unless’ DPP aamue kuwa hana nia ‘but’ itakuwa fundisho,” alisema Kaguo.

 

 

  

  

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya