![]() |
Trekta aina ya New Holland |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
WAKULIMA mkoani Morogoro wameilalamikia kampuni inayojihusisha na ukopeshaji wa magari, trekta na mashine za aina mbalimbali ya Equity for Tanzania Limited (EFTA) kuwa inawakandamiza na kuwanyonya katika mikopo inayotoa.
Wamedai kuwa EFTA ambayo katika Mkoa wa Marogoro imejikita zaidi kukopesha wakulima trekta, inawatoza riba kubwa na kwa kutumia ‘upofu’ wa sheria wa wakulima wengi wanaoingia mikataba ya kukopeshwa trekta na kampuni hiyo, inawanyonya na kuwakandamiza.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog jijini Dar es Salaam hivi karibuni, mmoja wa wakulima hao, Miraji Salehe Hassan aliyekopeshwa trekta na EFTA, alidai kampuni hiyo imemkoposhe trekta hilo mara mbili huku ikimtoza riba kubwa na pesa ya malimbikizo ya mkopo.
Hassan alisema kwa mara ya kwanza alikopa trekta kwa EFTA, Septemba 27, 2017 kwa ghamara ya shilingi milioni 48 na kulipa malipo ya awali shilingi milioni 10, lakini baadaye alianza kuandamwa na maofisa wa kampuni hiyo akidaiwa riba ambayo haipo kwenye mkataba wake ulioandikwa kwa Lugha ya Kiingereza pamoja fedha ya kuchelewesha marejesho.
“Mimi nilikopa trekta kwa Kampuni ya EFTA Septemba 27, 2017. Thamani ya mkopo wa trekta hiyo ambayo siyo mpya bali imekwishatumika ilikuwa shilingi milioni 48 na nilitakiwa kulipa malipo ya awali shilingi milioni 10. Nilisaini mkataba ambao ulikuwa umeandikwa kwa Lugha ya Kiingereza na nililipa shilingi milioni 10 ambazo ni malipo ya awali, wakanipa nikaendelea na shughuli zangu.
“Kuna kipindi kweli nilikuwa nachelewa kulipa kwa sababu hizi shughuli zetu za kilimo nadhani unafahamu wakati mwingine mazao yanagoma kutokana na msimu kuwa mbaya lakini nililipa deni la msingi lote.
“Wao EFTA wakasema ingawa nimelipa deni la msingi lakini bado ninadaiwa riba na pesa ya malimbikizo hivyo nilipe madeni hayo kwa pamoja vinginevyo nanyang’anywa trekta langu. Nikaenda na ule mkataba kwa wenzangu wanaojua kizungu ili waone masharti hayo wakasema hawaoni kipengele cha riba ila cha kuchelewesha malipo kipo. Nikachanganyikiwa kabisa kwa sababu mimi sijui kiingereza lakini mkataba wao nilisaini.
“Nikawarudia nikawaambia sawa nitalipa hizo pesa lakini wanipe muda kidogo, wakagoma wakasema muda wa kufanya marejesho umeishaisha hivyo kama bado nataka hilo trekta inabidi nianze upya mchakato wa kukopa. Basi nikaanza upya taratibu za kukopa trekta lile lile ambalo nilikuwa nimekopa awali na kulipa mkopo wote kasoro riba kidogo na hicho wanachoita wao tozo ya ucheleweshaji marejesho.
“Wakanipa mkataba mpya wa kukopa tena hilo trekta ambao thamani yake ilikuwa shilingi milioni 26. Mkataba mpya nilisaini Disembe 22, 2020, nikaanza kulipa upya huo mkopo na riba wakati ule wa mwanzo nao nilikuwa nadaiwa tena kulipa riba ya tozo ya malimbikizo. Hapo sijui sasa taratibu au sheria ya mikopo inasemaje maana hela yote ya kilimo inaishia kwa hawa EFTA,” alisema Hassan.
Taarifa za ziada ambazo Tanzania PANORAMA Blog imezikusanya kuhusu utata wa mkopo wa trekta hilo, zinadai kuwa Hassan alikopa trekta lililotumika, aina ya New Holland – TT 75- 4 WD, ‘model’ 8000 – series 75 HP, lenye thamani ya shilingi milioni 48 kwa Kampuni ya EFTA.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Hassan alilipa mkopo wote na kiasi kikubwa cha riba na tozo ya malimbikizo lakini EFTA walimnyang’anya trekta hilo kwa kile walichodai amekiuka mkataba kwa kuchelewa kukamilisha malipo ya tozo ya malimbikizo na kumpa masharti aingie mkataba mwingine mpya wa kukopa trekta hilo.
Nyaraka kadhaa ambazo Tanzania PANORAMA Blog imeziona zinaonyesha kuwa Hassan alisaini mkataba mwingine wa kukopeshwa trekta aina ya New Holland TT75 – 4 WD lenye thamani ya shilingi milioni 26. Hata hivyo mkataba huo wa pili ulioandikwa kwa Lugha ya Kiswahili hauonyeshi baadhi ya maelezo ya trekta kama ule wa mwanzo ulioandikwa kwa Lugha ya Kiingereza.
Taarifa zinadai zaidi kuwa Hassan alilipa shilingi milioni 10 kwa mujibu wa mkataba huo mpya na baadaye alilipa shilingi milioni tatu lakini aliamua kusitisha kulipa baada ya EFTA kumtaka alipe pia gharama za mahakama za kesi ya mgogoro wa trekta ambayo Hassan mwenyewe amekana kuifahamu na kwamba hajawahi kufika mahakamani kwa ajili ya kesi ya trekta baina yake na EFTA.
Tanzania PANORAMA Blog ilifika katika ofisi za EFTA zilizopo jengo la Sky, ghorofa ya tano, makumbusho Dar es Salaam na kukutana na Afisa Uwekezaji aliyejitambulisha kwa jina la Ismail Matete ambaye alipoulizwa kuhusu madai hayo, alisema kinachoangalia katika hilo ni mkataba baina ya mkopaji na mkopeshaji unaelekeza nini na ndicho kinachofuatwa.
Kwa maneno yake mwenyewe alisema, “Hivi ni vitu vya kimkataba, mikataba ipo na ina masharti yake na sisi ndiyo tunayoyasimamia. Mteja kabla hajasaini mkataba anausoma kwanza ndiyo tunaingia kwenye biashara. Tuna taratibu zetu.
“Hilo wanalodai kuuziwa trekta mara mbili hizo ni taratibu za kifedha, popote pale kama mteja anakiuka masharti ya mkataba hatua zinachukuliwa kulingana na mkataba wake. Taasisi zote za kifedha zinafanya hivyo kama mtu anakiuka masharti ya mkataba. Lakini vinginevyo kikawaida tu kama mtu hajakiuka mkataba wake sitaki kuamini kama anaweza kukopeshwa bidhaa moja, mara mbili. Na sisi mikataba yetu inaeleza wazi kuwa riba yetu ni asilimia 2.63.
“Na iko hivi kwa mkopaji. Kwenye kulipa deni, kama kutakuwa na malimbikizo, anapolipa kinachokatwa kwanza ni riba, kisha tozo ya malimbikizo na baadaye fedha inayosalia ndiyo inaingizwa kwenye deni la msingi,” alisema Matete.
![]() |
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) |
Tanzania PANORAMA Blog imezungumza na afisa mmoja wa Benki ya Tanzania (BoT) (jina lake tunalihifadhi) kuhusu sakata hilo ambaye alieleza kuwa jambo kubwa linaloangaliwa katika biashara ya kukopesha ni mkataba na kwamba mkopaji kutojua sheria hakumpa nafasi ya kutotekeleza masharti ya mkataba iwapo ameusaini.
“EFTA inasimamiwa na BoT, hilo nalifahamua na sina shaka nalo. Katika hilo unalouliza, kinachoangalia kwanza hapo ni mkataba unasema nini. Kama mkopaji alisaini mkataba hata kama hajui Kiingereza muhimu ni kwamba alisaini basi analazimika kutekeleza masharti ya mkataba husika.
“Lakini hayo unayoyasema ni mambo mazito sana ambayo nasita kuamini kuwa ni kweli yamefanywa na EFTA, siamini hata kidogo kuwa wamemkopesha mkopaji wao kwa mikataba miwili. Naweza kuongea vizuri na rasmi nikiiona mikataba hiyo, yote miwili.
“Ninachotaka uelewe, usilichukulie kirahisi hili jambo, hiyo ni taasisi ya kifedha sasa kama kuna jambo wanakiuka au kuna ujanja ujanja wa aina yoyote ile kwenye mikataba yao na wateja wakati wanasimamiwa na BoT, ikibainika, matokeo yake siwezi kuyasema hapa.
“Umeanza wewe, baadaye likisambaa hili watadaka wengine kwa sababu ya uzito wa sekta ya fedha na wakulima. Kwahiyo kama nilivyosema niletee kwanza hiyo mikataba niione na nipate maelezo ya kutosha ya wanaolia hao, baada ya hapo ndiyo nitasema au BoT itasema,” alisema.