Kunde |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
MFANYABIASHARA Hitek Parik, anadaiwa kujipatia mamilioni ya fedha kwa njia za utapeli wa mazao ya wakulima wa mikoa mbalimbali hapa nchini.
Parik, mtanzania mwenye asilia ya kiasia ni mmiliki wa Kampuni ya Indo Africa Investment Limited na anadaiwa kuzunguka mikoa mbalimbali akijitambulisha kuwa ni mfanyabiashara mkubwa anayenunua mazao hasa kunde, mbaazi na choroko.
Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA kutoka kwa watu wa karibu na mfanyabiashara huyo, zimedai kuwa mikoa ambayo amekuwa akifika zaidi kukusanya mazao ni Manyara, Arusha na Mwanza.
Kwamba katika mikoa hiyo anao mawakala wake ambao humkusanyia mazao ya wakulima kwa ahadi kuwa yanakwenda kuuzwa nje ya nchi kwa bei ya juu hivyo wapokee fedha kidogo na baada ya kuuzwa watapewa fedha zilizosalia.
“Huyu mhindi amekuwa tatizo kubwa kwa wakulima, anatumia mawakala wake kukusanya mazao kutoka kwa wakulima na wakati mwingine huwa anafika mwenyewe lakini anakichofanya ni utapeli.
“Anajitambulisha kuwa ni mnunuzi mkubwa wa mazao anayefanya biashara ya kusafirisha na kuuza mazao nje ya nchi. Huwa anawapa wakulima pesa kidogo na kuwaahidi kuwa akishasafirisha mazao wanayompa na kuyauza nje atawapa pesa iliyosalia na wengi huwa wanakubali kwa sababu bei anayowaahidi ni kubwa. Lakini sasa akishachukua mazao huwa harejei na wakulima hawapati chochote,” alisema.
Mbaazi |
Inadaiwa zaidi kuwa baadhi ya wakulima waliompatia kiasi kikubwa cha mazao na yeye kutokomea nayo, walikwenda kumsaka katika ofisi zake zilizopo eneo la Karakana, Barabara ya Nyerere mkoani Dar es Salaam ambako walikuta amekwishafunga ofisi yake.
“Baada ya kuwa amechukua kiasi kikubwa cha mazao ya wakulima, aliifunga ofisi yake iliyopo eneo la Karakana, Dar es Salaam na shughuli zake akawa anazifanyia nyumbani lakini jitihada za kumsaka zilizaa matunda mwishoni mwa mwaka jana alipokutwa akiwa nyumbani kwake Upanga.
“Walipompata walimpeleka polisi, hivi ninavyozungumza na wewe ana kesi tofauti tofauti zaidi ya kumi ambazo zimefunguliwa mwaka jana mwezi Novemba lakini mpaka sasa hajafikishwa mahakamani.
“Na kwa taarifa za karibuni sasa ameamua kuhamishia hizo shughuli zake kwenye mabenki, kuna benki moja ameomba mkopo lakini huo mkopo hatumii dhamana yake, ametafuta watu wamemtafutie mkulima mmoja ambaye amepewa pesa ili ampatie hati ya shamba lake ndiyo aitumie kuchukulia huo mkopo benki, huyo mkulima naye baadaye atalia tu” alisema mtoa taarifa.
Tanzania PANORAMA iliwasiliana na Parik jana kupata kauli yake kuhusu tuhuma anazoelekezewa. Kwanza alikiri kuwa yeye ni mfanyabiashara anayejihusisha na kununua, kusafirisha na kuuza mazao nje ya nchi.
Alipoulizwa kuhusu kutowalipa wakulima, kufunga ofisi yake iliyopo Barabara ya Nyerere kwa lengo la kuwakwepa wanaomdai na mipango yake ya sasa ya kuchukua mkopo mkubwa kutoka moja ya benki zilizopo jijini Dar es Salaam kwa kutumia hati ya shamba ambalo siyo la kwake alisema haelewi maswali anayoulizwa kwa sababu hajui Kiswahili sawasawa kisha akaomba atafutwe baada ya saa moja atakuwa sehemu nzuri kujibu maswali aliyoulizwa.
Alipotafutwa baada ya saa moja kama alivyokuwa ameomba hakupatikana.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro |
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema yupo kwenye msafara hivyo atafutwe wakati mwingine.
TANZANIA PANORAMA INAENDELEA KUFUATILIA MKASA HUU.