RIPOTA PANORAMA
HALI si shwari katika Jumuiya ya Kiislamu inayotambulika kwa jina la KSIJ Tanga Jamaat ya mkoani Tanga kutokana na mgogoro wa muda mrefu wa uongozi ambao chanzo chake kinadaiwa kuwa uongozi wa kimabavu na matumizi mabaya ya mali za jumuiya.
Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog leo na kuthibitishwa na mmoja wa wanajumuiya hiyo ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa zimeeleza kuwa baadhi ya wanajumuiya hiyo ambao hawaridhishwi na mwenendo wa uongozi wa jumuiya uliopo wanajipanga kuung’oa kwa nguvu.
Tanzania PANORAMA Blog imeelezwa kuwa wanajumuiya zaidi ya 40 wa KSIJ Jamaat ambao awali walitia saini waraka wa kutokuwa na imani na mwenyekiti wa Jamaat yao, Hussein Walji baada ya juhudi zao za kutaka mabadiliko ya uongozi kushindwa kuzaa matunda kwa njia ya amani, sasa wanapanga kuongeza shinikizo la kumng’oa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Walji anatuhumiwa kuendesha Jamaat hiyo peke yake akiwa hana Katibu wala kamati inayopaswa kuwepo na kufanya kazi bega kwa bega na mwenyekiti huyo.
Tuhuma nyingine anazoelekezewa Walji ni kuendesha Jamaat kidikteta, kudhulumu fedha za misaada za watu masikini wakiwemo wajane na walemavu ambao amekuwa akiwapa kiasi kidogo cha fedha za misaada na kuwalazimisha kusaini nyaraka zinazoonyesha wamepokea kiasi kikubwa cha fedha pamoja na kuwatisha baadhi ya wakosoaji wake kuwa atawapoteza wasionekane tena duniani.
Walji pia anatuhumiwa kutumia uwezo wake kifedha pamoja na kufahamiana kwake na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Tanga kuwashughulikia wakosoaji wake kwa kuwafungulia kesi za uongo polisi na kuwatisha kwa kutumia majina ya viongozi.
Akizungumzia hilo, mmoja wa wanajumuiya hiyo alisema ni kweli kuna tishio la kuwepo matumizi ya nguvu ya kumuondoa Walji kwenye uongozi wa Jamaat ili kunusuru maisha ya watu masikini ambao anawadhulumu fedha za misaada wanazopaswa kupewa na kuondokana na uongozi wa kidikteta na wenye vitisho vikiwemo vya kupotezana hapa duniani.
Alipoulizwa Walji kuhusu tuhuma anazoelekezewa, alishindwa kukanusha wala kukubali kuhusu madai hayo na badala yake alisema mambo hayo anaweza kuyazungumzia iwapo Tanzania PANORAMA Blog itafika ofisini kwake na kukutana naye ana kwa ana.
Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta bila mafanikio, Kamanda wa Polisi (RPC) wa Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi (ACP), Henry Mwaibambe kuzungumzia mgogoro huo unaodaiwa kufikishwa mezani kwake, lakini simu yake haikupokelewa na wala hakujibu ujumbe wa maandishi aliotumiwa. Tanzania PANORAMA Blog inaendelea kumtafuta RPC Mwaibambe sambamba na kufuatilia mgogoro huu.






