JINSI SERIKALI ILIVYOPORWA MALI ZA UMMA
SKANDALI ya kuporwa kwa mali za umma kisha kutumiwa kuchukua mkopo wa mabilioni ya fedha kwenye Benki ya NBC; na Serikali kukiri kuwepo kwa skandali hiyo huku ikieleza jitihada ilizochukua na inazoendelea kuchukua kukabiliana na uhalifu huo; ni moja ya mambo ambayo Tanzania PANORAMA Blog iliyaripoti kwa kina mwaka 2022.
Hatma ya skandali hiyo bado ipo kwenye kiza kinene kwa sababu kampuni inayohusika na kashfa hiyo, SISI Construction Company Limited (SISICOL) ambayo Agosti 30, 2001 ilinunua hisa asilimia 75 za Serikali kwa Shilingi milioni 287.03 katika Kampuni ya Mwananchi Engineering and Contracting Company Limited (MECCO) inaendelea kupumua.
Kauli ya Serikali kuhusu skandali hiyo ilieleza kuwa imekwama kukamilisha urejeshaji wa mali za umma kwenye mikono yake ambazo zimeporwa na SISICOL kwa sababu SISICOL haikutoa ushirikiano uliohitajika kwa Mamlaka ya Mapato (TRA); na kwa sababu ya ukaidi huo wa SISICOL, skandali hiyo ingejadiliwa kwa mapana na marefu kwenye mkutano wa wanahisa wa Kampuni ya MECCO uliopangwa kufanyika mwaka jana, mkutano ambao hata hivyo haukufanyika.
Wanasheria waliozungumzia skandali hiyo walisema ni skandali kubwa inayoangukia kwenye makosa ya jinai na kwamba SISICOL na Meneja wa Benki ya NBC aliyehusika kuidhinisha mabilioni ya mkopo kwa kampuni ya SISICOL kwa kutumia mali za umma wanapaswa kushtakiwa mahakamani.
Kwa upande mwingine, mwanahisa mkubwa wa MECCO ambaye ni SISICOL alipoizungumzia skandali hiyo mwaka jana, alisema atajibu mapigo dhidi ya shutuma na madai yote aliyoelekezewa kwenye mkutano na waandishi wa habari; mkutano ambao hadi leo haujafanyika.
Hii ni sehemu ya pili ya ripoti maalumu inayoeleza kinaga ubaga skandali hiyo.
Baada ya Msajili wa Hazina kuwasiliana na Benki ya NBC, hatua za kubadilisha umiliki wa mali za MECCO zilizokuwa zimebadilishwa na mwanahisa mkubwa mwenye jukumu la kuendesha MECCO ambaye ni Kampuni ya SISICOL bila Serikali kutaarifiwa zilianza kuchukuliwa hadi kufika hatua ya kufanya malipo ya Stamp Duty na Capital Gain ili kukamilisha taratibu za kubadilisha umiliki.
MECCO ilifanya malipo ya Stamp Duty kisha ikaomba ipatiwe msamaha wa Capital Gain Tax lakini baada ya MECCO kuwasilisha maombi ya msamaha wa kodi, Mamlaka ya Mapato (TRA), iliielekeza ipeleke hesabu zake na zile za Kampuni ya MAS Holding and Container Depot Limited ili izifanyie makadirio ya kodi.
MECCO chini ya uendeshaji wa mwanahisa mkubwa ambaye ni Kampuni ya SISICOL haikupeleka nyaraka za MAS Holding and Container Depot Limited hivyo TRA ikashindwa kufanya makadirio ya kodi kama ilivyokuwa imekusdia na baada ya agizo lake kutotekelezwa, ikasisitiza kodi husika ilipwe kama ilivyo na kama kuna haja ya kuomba msamaha, maombi ya msamaha yaelekezwe kwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Uchunguzi unaonyesha MECCO iliamua kuachana TRA na badala yake iliwasilisha maombi ya msamaha wa kodi kwa barua yenye nambari MECCO/HQ/0043/ACC ya Novemba 19, 2021 kwa Wizara ya Fedha na Mipango ya kuomba msahama wa kodi.
Waziri wa Fedha na Mipango baada ya kuyapitia maombi hayo, aliigeukia MECCO kwa barua yenye kumbukumbu nambari CAB.481/547/01 ya Mei 25, 2022 ikiwa na maelekezo ya kuwasilishwa kwa nyaraka ambazo MECCO ilielekezwa na TRA ili iweze kubaini kiasi cha msamaha unaoombwa kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya msamaha huo.
Mpaka Tanzania PANORAMA Blog ilipoanza kuripoti skandali hii, hilo nalo halikutekelezwa na MECCO kutokana na kile ilichodai kuwa Kampuni ya MAS Holding and Container Depot Limited kwa muda haikuwa ikifanya kazi baada ya shughuli zake za uhifadhi wa makontena kusitishwa.
Uchunguzi zaidi ulionyesha kuwa Kampuni ya MECCO ilikuwa haijaitisha kikao cha wanahisa tangu mwaka 2020/2021 na Mjumbe wa Bodi wa Serikali alikuwa hapewi ushirikiano. Jambo hilo liliilazimu Ofisi ya Msajili wa Hazina kuiandika barua MECCO ikiielekeza kutekeleza wajibu huo na MECCO ilikiri kupokea barua hiyo.
Katika uchunguzi huo ilibainika kuwa MECCO ilikuwa haitoi ushirikiano kwa mjumbe wa bodi aliyeteuliwa na Serikali kuiwakilisha katika kampuni hiyo kwenye Bodi ambapo tangu ateuliwe 12 Agosti 12, 2021 na kujulishwa kwa barua Agosti 13, 2021 alikuwa akiwasiliana na MECCO bila kupata ushirikiano stahiki na haijulikani endapo bodi ilikuwa ikikaa pasipo ushiriki wake au haikuwa imekutana kabisa.
INAENDELEA