HATUA 10 ZA NHC KUELEKEA UFANISI WA MALENGO 2022/2023

Date:

Share post:

SHIRIKA la Nyumba na Taifa (NHC) limetangaza mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu yake kwa mwaka 2022/23 utakaoliwezesha kuongeza mapato yake na kutoa huduma bora kwa umma ambao una hatua kumi.

Mwelekeo na hatua hizo zimetangazwa wiki hii na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemiah Mchechu wakati akitoa taarifa ya ufanisi wa shirika kwa mwaka 2021/2022 na mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli zake kwa mwaka 2022/2023 kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.

Hatua ya kwanza inayotajwa na Mchechu ni kuendelea kukamilisha ujenzi wa miradi iliyokuwa imesimama, ukiwemo mradi wa Morocco square ambao hivi sasa ujenzi wake upo kwenye hatua za mwisho kukamilika.

Kwa maneno yake mwenyewe, Mchechu anasema; ‘Mradi huu unatarajiwa kuanza kutumika rasmi mwishoni mwa mwezi Machi 2023. Tuna miradi iliyokuwa imesimama na tuna maagizo ya wazi kabisa kutoka serikalini kuwa miradi hiyo ikwamuliwe kwa sababu ikiwa imesimama hapo ni pesa ambayo imelala, pesa ambayo haizalishi chochote.

‘Mradi huu wa Morocco ulikuwa imesimama lakini tuko katika hatua nzuri na tunaamini mpaka mwezi wa tatu mwishoni wananchi wataanza kupata huduma hapo. Baada ya Morocco tutakwenda kwa kasi kujenga majengo ya aina hiyo maeneo mengine kutokana na soko lakini kwa Dar es Salaam ni wazi tutajenga sehemu nyingi zaidi.

‘Morocco Square kuna matumizi ya aina nne, kuna shopping mall ambayo imekwishajaa wapangaji lakini maombi ni mengi hivyo jengo hilo likianza kufanya kazi; watumiaji wakishaingia ndani  tutaanza kushughulika na upanuzi wa shopping mall.

‘Sehemu ya pili ni hoteli ambayo tayari imekwishapata mwekezaji na hiyo ndiyo ilikuwa itupe shida kwa sababu kwa sehemu kubwa hoteli inatakiwa iendeshwe na mtu mmoja kama mmiliki na sasa tayari mwekezaji yupo. Kwenye jengo la ofisi tunapangisha na kuuza na kwenye jengo la makazi tuna nyumba 100 ambazo mpaka sasa, zaidi ya asilimia 40 zimeishanunuliwa na zilizobaki tunaendelea kuuza.

Morocco Square

‘Nyumba za Morocco Square tumelenga watu wa kipato cha kati na kipato cha juu zaidi kama ndiyo walengwa wakuu wa mradi ule.

‘Pia tuna mradi wa seven eleven ambao ulikuwa umesimama, nao tunafikiri mwezi Machi au Aprili tutauanza rasmi kwa sababu tuko kwenye hatua za mwisho za mazungumzo na mkandarasi.’

Mchechu anaitaja hatua ya pili kuwa ni kuendelea na utekelezaji wa mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) katika maeneo mbalimbali nchini na kwamba tayari ujenzi wa nyumba 560, eneo la Kawe jijini Dar es Salaam umekwishaanza.

Akieleza zaidi anasema; ‘kwa Mkoa wa Dodoma tutaanza ujenzi wa nyumba 240 eneo la Medeli kwa ajili ya kuuza. Programu ya nyumba za Samia Housing Scheme imelenga kutatua changamoto ya makazi bora kwa watu wa kipato cha chini na kati.

‘Tunatarajia kuwa asilimia 50 ya nyumba za programu hii zitajengwa jijini Dar es Salaam, Dodoma asilimia 20 na mikoa mingine nchini asilimia 30. Samia Housing Scheme ni mpango utakaotekelezwa kwa awamu lakini mpango huu utakuwa na jumla ya nyumba 5000 zitakazogharimu takriban Shilingi bilioni 466. Programu hii inaenzi kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuijenga nchi yetu kiuchumi na kijamii.

‘Nyumba hizi zitakuwa za ghorofa na tutazijenga maeneo ya katikati ya miji katika mikoa yote nchini kutegemeana na mahitaji ya soko huku lengo likiwa kutatua matatizo ya Watanzania ambao ni wafanyakazi wa kima cha kati na chini wanaofanya kazi katika sekta binafsi na serikalini.

‘Kwa Dar es Salaam mradi huu tutajenga Kawe tulikoanzia, tutajenga pia eneo la Upanga na katikati ya mji. Ndani ya mwaka huu tutaanza kutekeleza mpango wa ujenzi wa nyumba za SHS eneo la Upanga.

Samia Housing Scheme

‘Katika maeneo ambayo tutatekeleza mpango huu hakuna mtu mwenye uwezo wa kuuza nyumba kwa bei ya chini kama ambavyo sisi tutauza na ndiyo maana tumetumia jina la Rais kwa sababu lazima liakisi ahueni ambayo wananchi wataipata, kwani lengo la Rais ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na unafuu katika maisha yao.’

Hatua ya tatu anayoitaja Mchechu ni ujenzi wa shopping mall kubwa katika na eneo la Medeli mkoani Dodoma ambayo itakuwa na square meter 25,000. Ujenzi huo utaanza mwaka huu baada ya kukamilika kuchorwa kwa mchoro wa ujenzi lakini eneo itakapojengwa limeishapatikana.

Kukusanya madeni ya kodi ya nyumba za NHC yanayofikia Shilingi bilioni 21 na madeni mbalimbali yatokanayo na uuzaji wa nyumba na viwanja na shughuli za ukandarasi yanayofikia takriban Shilingi bilioni 11 inatajwa na Mchechu kuwa hatua ya nne ya mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu yake kwa mwaka 2022/23.

Hapa Mchechu anasisitiza kuwa kila mpangaji wa NHC anayedaiwa kodi atafikiwa ili kuona njia nzuri kwake ya kulipa deni lake lakini msisitizo anaoutoa kwa wateja kuwa kila anayedaiwa anapaswa kulipa deni lake ili kuliwezesha shirika kuendelea kuwahudumia Watanzania wote kwa kutumia rasilimali za umma.

Hatua ya tano anayoitaja ni kuendelea kutekeleza miradi ya ubia kwa kushirikiana na sekta binafsi kadri itakavyokuwa imepitishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya NHC na kwamba hatua hiyo itasaidia kukuza uchumi na kuwapatia Watanzania makazi bora na nafuu.

Katika hilo anakumbusha kuwa Disembe 2022, NHC ilizindua sera ya ubia. Sera hiyo ilizinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kisha ikatangazwa miradi mbalimbali ambayo tayari imeishapata wawekezaji wengi na hivi sasa shirika lipo kwenye hatua za mwisho za kuwapitisha.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (katikati) alipokuwa akizindua Sera ya Ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mwishoni mwa mwaka jana. Wengine katika picha kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Allan Kijazi na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemiah Mchechu.

Anasema, ‘Lengo letu kwenye miradi ya ubia, katika kipindi cha miaka mitano tunaamini tutaweza kuvutia uwekezaji wa Shilingi trilioni 2 kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Hatua ya sita ambayo Mchechu anaitaja ni kuendelea kusimamia miliki ya nyumba 18,622 za shirika kwa kuzifanyia matengenezo ipasavyo na kwamba katika kufanikisha hilo, NHC litatenga bajeti ya kutosha kila mwaka kutekeleza mpango huo kwani inafahamika baadhi ya nyumba zake hazipendezi sana lakini zipo jitihada za kuweka bajeti ya kutengeneza nyumba hizo sambamba na bajeti kwa ajili ya kujenge nyumba mpya.

Mchechu anaitaja hatua ya saba kuwa ni kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali wakiwemo TARURA, TANROADS, Tanesco, TTCL na wengineo ili kurahisisha utekelezaji wa miradi ya NHC hususan ushiriki wao wa kuweka miundombinu muhimu ya barabara, maji na umeme katika maeneo ya ujenzi wa nyumba.

“Kawe tunaenda vizuri sana, kampuni za simu zinataka kila nyumba iwe na internet na Kampuni za Azam na DSTV wanataka huduma zao pia ziwe pale. Tunataka tuishi kwenye dunia ambayo wenzetu wanaishi, kuna mbingu mbili; ya kwanza duniani kwa sababu Mungu hakutuleta duniani tupate tabu na ya pili ni huko tunakohubiriwa na viongozi wetu wa dini ambako tutapakuta tukifa.

Mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Kawe jijini Dar es Salaam. Picha hii inaonyesha taswira ya mradi huo utakapokamilika.

‘Tunaamini tunapaswa kutengeneza mazingira sahihi kwa watu wanaponunua bidhaa zetu ili waweze kufurahia maisha yao.’

Mchechu anaendelea kwa kutaja hatua ya nane kuwa ni kuendelea kujenga uhusiano wenye tija na wabia na taasisi mbalimbali ili ziweze kuelewa malengo ya NHC. Hapo anaeleza zaidi kuwa taasisi hizo ni zile zenye kuiathiri moja kwa moja NHC na anazitaja kwa uchache kuwa ni pamoja na mashirika, Bunge na vyombo mbalimbali vya sheria.

Akizungumzia hatua ya tisa na ya kumi anasema; ‘tutaendelea kusimamia nidhamu ya utendaji kazi ndani ya shirika ili kuweza kuamsha ari na tija kwa watendaji. Huduma bora kwa wateja ndiyo kipaumbele cha utendaji wa watumishi wa shirika. Bado tunatakiwa tujiongeza zaidi ili mipango yetu iwe bora.

‘Na tutaendelea kushirikiana na vyombo vya habari kama muhimili muhimu wa upashanaji habari kwa wananchi, uelimishaji na kujenga taswira ya shirika.’

Taarifa ya Mchechu inajumuisha pia ripoti ya ufanisi ya NHC kwa mwaka 2021/22, ambayo inaonyesha mwenendo wa ukuaji wa kasi kiuchumi pamoja na kuongezeka kwa mtaji wa shirika ambapo ripoti hiyo inaonyesha kuwa NHC limeendelea kuongeza mapato yake ambayo sasa yamefikia Shilingi bilioni 257.47 kwa mwaka 2022 kutoka  mapato ya Shilingi bilioni 144.42 kwa mwaka 2021.

Ripoti hiyo inaonyesha kupanda kwa mapato ya kodi hadi kufikia Shilingi bilioni 90.76 kutoka Shilingi bilioni 89.23 mwaka 2020/21 na kadhalika, mapato ya mauzo ya nyumba nayo yamepanda kutoka Shilingi bilioni 29.33 mwaka 2020/21 hadi kufikia Shilingi bilioni 121.95 mwaka 2021/22. 

Sehemu ya ripoti hiyo ambayo imetolewa baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kulifanyia ukaguzi shirika hilo inasomeka hivi; ‘Vilevile, mapato ya miradi ya ukandarasi yamekua kutoka Shilingi bilioni 25.60 mwaka 2020/21 hadi kufikia Shilingi bilioni 43. 98 mwaka 2021/22.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere.

Shirika limeendelea kuongeza faida kabla ya kodi hadi kufikia kiasi cha Shilingi bilioni 92.9 kwa 2021 na faida ya Shilingi bilioni 93,966. Aidha, mwaka 2020/2021 faida ilishuka kutokana na kushuka kwa hali ya soko la nyumba nchini.

‘Hata hivyo, faida halisi inayotokana na shughuli za shirika iliongezeka hadi kufikia Shilingi bilioni 60.7 mwaka 2021/22 kutoka Shilingi bilioni 31.7 mwaka 2020/21. Ongezeko hili lilienda sambamba na ongezeko la majengo.  Hali ya soko la nyumba imeanza kuimarika hivyo ni matarajio ya shirika kuwa mwaka wa fedha 2022/23 litaendelea kupata faida kubwa.

‘Mizania ya shirika imeendelea kuimarika na thamani ya mali za shirika (Total Assets) kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyesha kuwa hadi kufikia Juni 31, 2022 zilikuwa Shilingi trilioni 5.04.

‘Mizania hii imeendelea kukua mwaka hadi mwaka kwa wastani wa asilimia 12 katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2019. Thamani hii inahusisha vitega uchumi vya majengo na ardhi ghafi inayomilikiwa na shirika ambayo bado haijaendelezwa ikiwa ni pamoja na miradi ya nyumba inayoendelea.

Mtaji wa shirika umeongezeka kutoka Shilingi trilioni 2.9, Juni 2019 hadi kufikia Shilingi trilioni 3.4 Juni 2022 na kwa upande wa Sera ya Uwajibikaji kwa jamii ya shirika katika kipindi cha mwaka 2021/2022, limeendelea kuchangia kwenye Sekta ya Elimu na Afya.

‘Kwa upande wa elimu, shirika limechangia ujenzi wa madarasa na kwa upande wa afya michango ililenga kuboresha huduma za afya kwa kupunguza changamoto za afya na masuala mengine ya kijamii ili kuleta unafuu na maisha bora kwa jamii. Katika kipindi hiki shirika lilitumia kiasi cha Shilingi milioni 415.2.

‘Kuhusu kodi mbalimbali zilizolipwa serikalini, shirika lililipa kodi mbalimbali inayofikia Shilingi bilioni 22.0 kwa mwaka 2021/2022. Aidha, shirika limelipa gawio serikalini la Shilingi milioni 750 kwa mwaka 2021/2022.

‘Gawio hili ni kiwango kinachopaswa kulipwa na shirika kila mwaka kutokana na maelekezo ya Msajili wa Hazina lakini pia Shirika limekuwa likichangia kila mwaka gawio la Serikali na kulipa kodi za Serikali pamoja na kujiendesha lenyewe kibiashara bila ya kupata ruzuku kutoka serikalini.’

NHC lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge namba 45 ya mwaka 1962 kabla ya kuunganiswa na iliyokuwa Msajili wa Majumba kwa Sheria namba 2 ya mwaka 1990, ambayo ilirekebishwa mwaka 2005 ili kulifanya shirika lijiendeshe lenyewe kibiashara.

Malengo ya NHC kwa mujibu wa mpango mkakati wake wa mwaka 2015/16 hadi 2024/25 ni pamoja na kuwa msimamizi mahiri wa miliki, kuimarisha uwezo wa kiuendeshaji na udhibiti, kutumia kikamilifu rasilimali watu, kuwa kiongozi katika uendelezaji miliki, kuhuisha mikataba na mazingira ya kisheria na kujenga taswira ya shirika.

Na ili kutimiza malengo yake hayo, NHC linaongozwa na maadili ya msingi sita ambayo ni weledi, ufanisi, uwazi, ubunifu, ushirikiano na uadilifu.

About The Author

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

spot_img

Related articles

USIYOYAJUA KUHUSU KOCHA ALIYEANDIKA HISTORIA BUNDESLIGA

MUNICH, Ujerumani JINA la Marie-Louise Eta limeandika historia katika soka la Ujerumani baada ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa...

BURNA BOY HATAKI MAZOEA, ‘BIFU’ KWAKE KAWAIDA TU

HIVI karibuni, supastaa wa muziki wa Afrobeat, Burna Boy, aliingia kwenye mikono ya Chama cha 'Ma-dj' nchini Nigeria,...

BURKINA FASO IKO HOI AU HAI CHINI YA KAPTENI TRAORE?

HATUA ya kutangaza kuwa raia wake waaitarajie demokrasia imeibua maswali mengi juu ya uongozi wa Kapteni Ibrahim Traore...

SIMU YAKO CHANZO CHA UGONJWA WA MOYO, SARATANI?

UKWELI ulio wazi ni kwamba matumizi ya simu za mkononi yameongezeka kwa kasi duniani, Tanzania ikiwa na 'laini'...