RIPOTA PANORAMA, ARUSHA
RUBANI Mstaafu wa Shirika la Ndege la India, Dennis Masha Wekesa anakusudia kuiburuza mahakamani Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya jumuiya hiyo kukataa kumkabidhi gari alilonunua katika mnada wa hadhara uliofanyika Agosti mwaka huu.
Wekesa, mkazi wa jijini hapa alinunua gari hiyo katika mnada wa kuuza vifaa mbalimbali vya jumuiya hiyo yakiwemo magari, uliofanyika jijini hapa Agosti 18, mwaka huu lakini hadi leo, pamoja na kutimiza masharti yote ya mnada hajakabidhiwa gari lake.
Kutokana na kupingwa danadanada kila akifuatilia gari lake, rubani huyo, kupitia kampuni ya wanasheria ya Maro ameipa EAC notisi ya siku saba apewe gari lake vinginevyo ataiburuza mahakamani.
Kupitia kampuni ya udalali ya LOSAREA ya Arusha, jumuiya hiyo iliuza vifaa vyake yakiwamo magari katika mnada wa hadhara ambako Wekesa alifanikiwa kununua gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili TCD 302 EAC.
Katika Notisi hiyo ya siku saba iliyotolewa Novemba mosi, mwaka huu jumuiya hiyo imepewa siku saba ya kukabidhi hilo ikiwa katika hali iliyokuwa awali wakati wa ukaguzi kabla mnada huo kufanyika.
Notisi hiyo yenye kumbukumbu EELM/11/DN/VOL./11/2022 inasomeka: ‘Jumuiya iliuza gari aina ya Toyota Land Cruiser yenye usajili namba TCD 302 EAC katika mnada wa hadhara kwa mteja wetu Dennis Masha Wekesa kwa malipo ya shilingi 48,000,000.’
Aidha notisi inaeleza kuwa baada ya mnada huo wa hadhara Agosti 22, mwaka huu Wekesa alipewa cheti cha ununuzi (certificate of sale) iliyomwezesha kulipa kodi mbalimbali za serikali ili abadilishe umiliki wa gari hilo.
Septemba 29, mwaka huu EAC kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu, Steven Mlote iliandika barua kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuifahamisha mamlaka hiyo kuwa Dennis Masha Wekesa ndiye alishinda mnada wa kununua gari hilo hivyo taratibu nyingine za kikodi na kubadilisha umiliki zifanyike.
‘Kati ya Oktoba 4 na 8 mteja wetu alilipa kodi zote za Serikali kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili gari hilo lipatiwe namba mpya za usajili na kukabidhiwa kwa mmiliki mpya lakini jumuiya haikutekeleza,’ sehemu ya notisi hiyo inasomeka.
Mwanasheria huyo wa kampuni ya Maro katika notisi hiyo ameeleza kuwa
hatua ya taasisi hiyo kushindwa kukabidhi gari hilo imesababisha usumbufu mkubwa kwa mteja wao na iwapo taasisi hiyo haitakabidhi gari hilo ndani ya siku saba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya jumuiya hiyo.
Akizungumzia sakata hilo, Wekesa ambaye kitaaluma ni rubani aliyeendesha ndege za Shirika la Ndege la India (Air India) na Precison Air alithibitisha kuingia katika mgogoro na jumuiya hiyo kutokana na kutokabidhiwa gari alilonunua katika mnada wa hadhara.
‘Magari mengine yaliyouzwa katika mnada huo yalishakabidhiwa kwa wateja waliofanikiwa kuyanunua lakini katika hali ya kushangaza jumuiya imekuwa ikinizungusha kwa zaidi ya miezi mitatu sasa kunikabidhi gari langu,’ alisema Wekesa.
Aliongeza: ‘Sikutarajia kupata usumbufu niliokutana nao nikiamini kuwa jumuiya hii ni taasisi yenye weledi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake kitaifa na kimataifa.’
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya LOSOREA iliyosimamia mnada huo, John Ezekiel Longolela alisema ni kweli Wekesa alishinda mnada wa kununua gari hilo na alikamilisha taratibu zote za kisheria ili akabidhiwe gari hilo.
‘Kabla sijamkabidhi gari hilo nilipokea ujumbe wa barua pepe kutoka kwa moja wa watumishi wa EAC kuwa nirudishe funguo za gari hilo kwao bila maelezo,’ alifafanua mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, Mlote alisema kwa njia ya simu kuwa hakuwa ofisini kwa muda mrefu kutokana na kuwa safari nje ya nchi na kuahidi kuwa atautafutia ufumbuzi mgogoro huo baada kurudi ofisini.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliundwa upya mwaka 1999 ikiwa na nchi wanachama waanzilishi ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda na baadaye kuongezeka kwa wanachama wengine Rwanda, Burundi, Sudan ya Kusini na hivi karibuni Congo DRC.






