HAMEES SUBA
ILIPOISHIA
NILIHOFIA kuwauliza wafanyakazi wenzangu waliokuwa wamefika ofisini kwa sababu sikutaka mtu yeyote ajue kinachoendelea kati yangu na Diamond. Nilitoka nje nikaenda kusimama kwenye ngazi inayotokea nyuma ya jengo hilo nikitafakari juu ya upotevu wa ghafla wa picha hizo. Pembeni ya ngazi kulikuwa na sehemu ya kutupia taka za maofisini (dust bin).
Kwa hiyo mahali nilipokuwa nimesimama nikawa natazama zile taka, ghafla nikaona picha moja ikiwa katikati ya taka zile, nikamuita mlinzi nikamuuliza mbona naiona picha kama ninayoitafuta kwenye dust bin?
Naye kwa mshangao akawa anatazama kule nilipokuwa napatazama mimi. Akapiga hatua za haraka kuelekea ilipokuwa ile picha, akainama akaiokota kisha akasema; “Dah ni zenyewe mkuu sijui nani kafanya hivi.”
TUENDELEE
Mlinzi akainama tena pale jalalani kuanza kufukua makaratasi yaliyokuwa yametapakaa kwenye jalala hilo kisha akainuka na picha nyingine mbili za Diamond kisha akarudia kusema; Dah sijui zimefikaje huku mkuu?”
Sikuwa na jibu la kumpa bali nilimnyooshea mkono kwa ishara kwamba anipatie zile picha. Alinipatia huku akionekana kustaajabishwa sana na kitendo kile. Nilizipokea nikazifuta kwa leso kisha nikarudi ofisini kwangu nikaketi mezani kwangu nikitafakari juu ya picha zile kutupwa jalalani.
Nilijiuliza kama zilitupwa kwa makusudi au kwa habati mbaya lakini sikupata jibu. Papo hapo nikakumbuka kwamba katika vikao vyetu ndani ya chumba cha Habari tulikubalina tusiruhusu picha zozote zisizokuwa na ubora kuingia chumba cha habari kwa ajili ya kutumika kwenye gazeti.
Nikahisi pengine labda ndiyo sababu ya zile picha kuondolewa pale chumba cha habari. Lakini bado nikawa na swali kwamba hata kama tulikubalina hivyo, mbona hatukusema zitupwe jalalani? Na mbona mimi kama kiongozi niliyewahi kuliko wafanyakazi wengine nisijulishwe juu ya tukio hilo kabla picha hizo kwenda kutupwa?
Mwisho wa yote nikahisi kuna kitu kitakuwa kimejificha nyuma ya pazia. Wazo jipya likanijia akilini. Nikaona isiwe tabu, wacha nifanye utaratibu wa kumwita Diamond aje kupiga picha nyingine kwa kutumia kamera zetu na kuachana na zile picha mbovu alizozileta.
Sikupoteza muda, nilitoka nje nikampigia simu Papaa Misifa nikamwamba picha alizoleta Diamond hazikuwa nzuri hivyo amtafute amwambie aje ofisini kuja kupiga picha nyingine.
Bahati nzuri Papaa Misifa aliniambia kuwa Diamond yuko naye wakati tukizungumza. Lakini akashauri kuwa badala ya kumwita ofisni kwa nini nisimuelekeze sehemu ambayo kuna studio nzuri ya kupiga picha ili akapige na kuja nazo. Nilikubalina na wazo lake nikamwelekeza sehemu mbili zilizokuwa na studio kali za upigaji picha wa kisasa. Sehemu ya kwanza ilikuwa Posta Mpya kwenye jengo la Benjamini Mkapa Tower, nilimwambia chini kwenye maduka yaliyokuwepo katika jengo hilo kulikuwa na studio mpya kabisa ya kupiga picha za kisasa ilikuwa ikiitwa Photo Point, anaweza kwenda hapo na kupiga picha ninazozihitaji mimi.
Sehemu ya pili nilimwelekeza Mayfair Plaza, nako kulikuwa na studio kama hiyo kwa ajili ya upigaji picha. Nikamwambia akifanikiwa kupata picha katika studio hizo atakuwa kawapiga bao wasanii wengi kwenye upande wa ubora wa picha kwani wakati huo wasanii wengi walipiga picha katika studio za kawaida za Kariakoo na sehemu nyinginezo ukiachilia mbali wale waliokuwa wakitegemea picha zilizokuwa kwenya maktaba za vyumba vya Habari.
Lakini wakati namweleza hayo Papaa Misifa akaniambia kwamba kuna studio moja maeneo ya Tandale Darajani, kuelekea Kijitonyama nako kulikuwa na studio nzuri sana inayopiga picha za kisasa, hivyo kwa sababu ya ukaribu na uharaka wa picha hizo aliona ni vema Diamond aenda kupiga picha katika studio hiyo. Nikamwambia kama ana uhakika studio hiyo inapiga picha za kisasa basi amruhusu akapige picha hapo lakini kama zitakuja kama zile alizoleta mwanzo sitazitumia. Tukaishia hapo.
Baada ya saa moja hivi kupita Diamond aliwasili ofisini kwangu akiwa na picha tatu. Nilizitazama na kuridhika nazo, ubora wake zilifanana sana na zile za Photo Point kwa Benjamini Mkapa Tower na zile ya Mayfair Plaza japo hazikufikia ubora wake asilimia 100.
Pamoja na kuleta picha hizo, kwa sababu mmoja wa wapiga picha wetu wa ofisini alikuwa ameshafika nilimuomba ampige picha nyingine za nyongeza Diamond kwa ajili ya matumizi ya baadaye.
Alikubali na kuingia ofisini kwenda kuchukua kamera kwa ajili ya kazi hiyo. Lakini alipotoka hakuwa na kamera akaniambia kuwa betri ya kamera haina chaji hivyo nisubiri kidogo ipate chaji kwani alishaiweka kwenye umeme.
Nilisubiri kwa kitambo kidogo kisha nikamfuata na kumuuliza: “Vipi haijapata chaji nipate japo picha mbili tatu kama betri inasumbua?”
Akaniambia chaji iliyoingia ni ndogo sana kiasi kwamba inaweza kuzima baada ya kupiga picha moja tu. Niliona kuendelea kusubiri ni kupoteza muda wakati tayari picha za kuanzia nilishazipata. Nikamwambia yule mpiga picha aahirishe zoezi hilo mpaka siku nyingine. Nikamruhusu Diamond aondoke kuendelea na shughuli zake.
Baada ya Diamond kuondoka, nilirudi kwenye kompyuta yangu kuanza kuandika stori ya kwanza ya promo kwa Diamond. Nilikuwa nikiandika kwa furaha sana kwa sababu ya ubora wa zile picha alizoleta awamu ya pili, nilizikubali sana.
Nikajisemea moyoni kama kuna mtu alifanya fitna ya kuzitupa zile picha jalalani kwa sababu ya kutokuwa na ubora unaoridhisha basi safari hii atakoma mwenyewe.
Stori yangu ilikamilika ikiwa na kichwa cha habari kosemacho: “FIMBO YA ALI KIBA YAPATIKANA!” Hiki ndicho kichwa cha habari cha kwenye habari yangu ya kwanza niliyoandika kumtangaza Diamond tangu aliposajiliwa na Kampuni ya Alajazeerah Entertainment.
Hapanizungumze kidogo; Ukweli ni kwamba kila nikikikumbuka kichwa hiki cha habari huwa najisikia furaha kwa sababu ilibeba kila kitu nilichokikusudia kwa Diamond katika mafanikio yake.
Halikuwa jambo rahisi kumlinganisha Diamond na Ali Kiba kwa wakati huo, ilikuwa kama mzaha au utani kufikiri jambo kama hilo kwamba kuna mtu anakuja kushindana na Ali Kiba achilia mbali kuja kumzidi kimafanikio na kiutajiri.
Alipokuwa amefika Ali Kiba wakati Diamond ana pambana kutoka ni parefu sana. Labda nikuongeze na hii ili twende sawa; Moja ya sababu zilizomfanya Diamond kwenda kurekodi muziki wake Sharobaro Records kwa Bob Junior ni kutokana na kutopata nafasi ya kurekodi katika studio ya G. Records kwa Prodyuza Gulu a.ka G. love alikokuwa akirekodia Ali Kiba wakati huo.
Kwa mwanamuziki mmoja aliyekuwa akirekodi G.Records (jina namuhifadhi kwa sasa) aliniambia kuwa Ali Kiba ndiye aliyemshawishi na kumuombea Diamond kwenda Kwa Bob Junior kutokana na kusota sana kwenye foleni ya G. Records pale Kariakoo.
Kwa maana nyingine ni kwamba Diamond hakuthaminika ndani ya G. Records kwa wakati huo kutokana na uchanga wake kiasi cha kukosa nafasi ya kurekodi katika studio hiyo.
Hivyo basi unaweza ukaona au kutambua ukubwa wa Ali Kiba ulivyokuwa wakati Diamond anapambana kutoka. Wakali wengine waliokuwa ‘membazi’ wa kudumu pale G Records mbali na Ali Kiba ni pamoja na Dully Sykes, Noorah, Abby Skillz, Mr Blue na wengineo.
Hivyo, kitendo cha kusema FIMBO YA ALI KIBA YAPATIKANA halikuwa jambo jepesi hata kidogo, ilionekana kama ndoto za mchana au upuuzi.
Sikiliza sasa, gazeti lilitoka siku ya Jumatatu likiwa na habari ya Diamond yenye kichwa kisemacho FIMBO YA ALI KIBA YAPATIKANA, majira ya saa moja asubuhi simu yangu iliita. Nilipoipokea nikakutana na salamu yenye ubaridi, ‘mkuu shikamoo.’
Niliitambua sauti iliyotoa salamu hiyo kuwa ni ya Diamond sababu nilishaizoea. Niliitika, ‘marahaba, mambo vipi dogo?”
“Dah, powa tu mkuu… nimeona stori inatisha kinyama mkuu, safari hii lazima tutuboe.” Nilifurahi kusikia maneno hayo toka kwa kijana mwenye uchu wa mafanikio Diamond lakini kabla sijatoa neno, Diamond akaendelea, ‘…ila mkuu kuna jambo nilitaka tuongee kidogo.’
Nikamuuliza, “jambo gani?” akasema: “Mkuu kuna watu wamenipigia simu wanachonga sana na kuongea ‘shit’ za ajabu eti kwa sababu umenichanganya na Ali Kiba kwenye stori yangu…wamemaindi sana ile kusema fimbo ya Ali Kiba imepatikana.’
Kwa upande wangu sikushtuka hata kidogo kusikia taarifa hizo kwa Diamond kwa sababu nilijua vitu kama hivyo lazima vingetokea. Ni kawaida kwa kila stori tunazo andika zije na mirejesho tofauti, kuna watakaosifu na kuna watakaoponda, hivyo ndivyo ilivyo.
Nikamwambia, ‘kwa hiyo wewe unaonaje? akasema ‘mi naona stori ijayo unipige promo kivyangu bila kunipambanisha na msanii mwingine au unaonaje mkuu?’
Nikamwambia ‘sikiliza dogo ukitaka hivyo unavyosema itachukua muda sana kutoka, lazima nikupambanishe na mtu, labda kama humtaki Ali Kiba uniambie ni msanii gani mwingine unayeona anafaa kukupambanisha naye.’
Diamond akasema, ‘basi mkuu safari hii nipambanishe na Mr Blue.’
Ukweli Mr Blue alikuwa ni miongoni mwa wasanii waliokuwa wakifanya vizuri sana wakati huo na hata mimi nimekuwa nikimkubali siku zote lakini aina ya muziki anayofanya Mr Blue na Diamond ni tofauti, Blue anfanya HipHop na Diamond anafanya Bongo Fleva?
Nikamwambia, ‘uje ofisini baadae tulijadili hili jambo vizuri tutajua nini cha kufanya.’ Nilimwambia hivyo kwa sababu ilikuwa ni asubuhi sana aliponipigia simu, nadhani ilikuwa majira ya saa kumi na mbili na ushehe hivi au saa moja kasoro asubuhi.
Unaweza ukashangaa muda huu watu walisoma magazeti saa ngani na kumtumia meseji Diamond saa ngapi lakini ukweli ni kwamba magazeti jijini Dar es Salaam yanasambazwa kuanzia saa sita usiku hivyo basi ni jambo la kawaida watu kusoma magazeti tangu yanapoingia sokoni hasa kwa wenyeji wa Jiji la Dar es Salaam. Na kwa kipindi hicho mahazeti ya Udaku yalikuwa ‘hot’ sana sokoni.
Baada ya kumaliza kuongea na Diamond sikulala tena niliingia bafuni kuoga kisha nikavaa nguo fasta fasta nikawasha gari na kwenda ofisini.
Nilitangulia kufika nikachukua gazeti na kuanza kuisoma ile habari neno kwa neno wazungu wanasema ‘between the lines’ ili kujua ni kitu gani kilichowakasirisha baadhi ya wasomaji hususan mashabiki wa King Kiba hadi wamtiririshie maneno makali Diamond.
Lakini nikawa najiuliza mbona mimi sikupata mrejesho wa meseji alizotumiwa Diamond wakati namba yangu uliokuwepo kwenye gazeti?
Nilipomaliza kuisoma ile habari nikakumbuka kuwa ‘line’ iliyokuwa kwenye simu yangu siyo ile yenye namba zangu zilizoko kwenye gazeti. Nilikuwa na tabia ya kubadili laini usiku ninaporudi nyumbani ili kupunguza usumbufu wa simu na meseji za wasomaji wa magazeti yetu.
Nikabadili line haraka ili kuangalia nini kimejiri toka kwa wasomaji wetu (sio kwa ajili ya stori ya Diamond bali mrejesho wa maoni ya wasomaji kwa gazeti zima). Nilipoweka tu ile line zikaanza kumiminika meseji.
Kumbe zile ‘shits’ alizopewa Diamond na mimi zilitumwa kwenye simu yangu, kwa upande wangu nilitumiwa meseji nyingi kuliko hata alizotumiwa Diamond.
Baada ya kuzikagua zile meseji ndipo nikapata jibu sahihi kwamba kulikuwa na makundi mawili yaliyotuma meseji. Kundi la kwanza ni kutoka kambi ya Ali Kiba ambao hao ndio waliomkogesha Diamond maneno makali na kundi la pili lilikuwa la wasomaji wa gazeti la Kiu ya jibu ambapo wengi wao walishauri na kutoa maoni kuhusu kutomlinganisha Diamond na Ali Kiba, wengi waliona kuwalinganissha wawili hao ni sawa na kumkosea adabu Ali Kiba. Walishauri Diamond afanyiwe promo kivyake na siyo kupitia mgongo wa Ali Kiba. Meseji toka kundi hili hazikutumwa kwa Diamond. Nyingi zilitumwa kwangu kama Mhariri wa gazeti.
Zile za wapambe wa Ali Kiba zilijaa matusi kiasi kwamba nilihisi kama nyingine zilitumwa na Ali Kiba mwenyewe.
Hatimaye Diamond alifika ofisini, sikutaka kumueleza yaliyonikuta kwa kuhofia kumkatisha tamaa. Sikuwa na mambo mengi ya kuzungumza naye zaidi ya kumwambia haya: “Nimefikiria sana nimeona siwezi kukupambanisha na Mr Blue wala msanii mwingine zaidi ya Ali Kiba, unachotakiwa wewe ni kuvumilia tu, matusi hayaui, tambua kwamba unatakiwa kufika pale alipo Ali Kiba kwa hiyo huwezi kufika kwa kupambanishwa na watu wengine, tutakwenda hivyo hivyo, wanaochonga wacha wachonge mwisho watatulia.’
Diamond aliinamisha kichwa chini kwa sekunde kadhaa kisha akainua kichwa na kusema, ‘nimekuelewa mkuu, wee piga kazi tuone itakavyokuwa.’
TUKUTANE SEHEMU YA NNE YA SIMULIZI HII YA KWELI NA YENYE MAFUNZO MENGI