RIPOTA WA WAZIRI MKUU
SERIKALI imewaruhusu wanafunzi 28,000 waliokidhi vigezo vya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 lakini hawajapangiwa kupata mikopo kwenda vyuoni kujisajili chini ya utaratibu maalumu wa Wizara ya Elimu.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akisoma hotuba ya kuahirisha Bunge mkutano wa tisa wa Bunge la 12 jijini Dodoma.
Majaliwa alisema wanafunzi hao wmeruhusiwa kuendelea kujisajili katika vyuo walivyopangiwa wakati Wizara ya Elimu ikiendelea kukamilisha taratibu muhimu.
āLengo la Rais ni kuwanufaisha wanafunzi wote wenye uhitaji, waliopata udahili na wenye vigezo vya kupata mikopo. Katika mapitio ya bajeti ya nusu mwaka baadaye mwaka huu tutaliomba Bunge lako tukufu liridhie matumizi ya fedha zitakazohitajika,ā alisema.
Katika hotuba yake hiyo, Majaliwa aliwashukuru wabunge kwa kuibua hoja zenye lengo la kuboresha utendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu pamoja na mfumo mzima wa ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini.
Alisema miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa kwa hisia na kupewa uzito mkubwa na wabunge wakati wa mkutano huo ni hoja ya ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
āNyote mtakubaliana nami kwamba lengo la mjadala huo lilikuwa kutafuta suluhu ya suala la wanafunzi takribani 28,000 wenye uhitaji wa kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 ambao walikuwa hawajapangiwa mikopo kutokana na ukomo wa kibajeti,ā alisema.
Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema hadi sasa taasisi za umma 455 zimeunganishwa na zinatumia mfumo mpya wa taarifa za kiutumishi na mishahara ili kupunguza muda wa kuchakata malipo ya mishahara kutoka siku 14 hadi siku moja pamoja na kuwa na taarifa sahihi za watumishi wanaotarajia kustaafu.
Akizungumzia utendaji kazi na uwajibikaji wa watumishi wa umma, Majaliwa alisema Serikali imeendelea kuboresha, kuimarisha na kuweka mifumo imara ya usimamizi wa rasilimali watu na utendaji kazi wa watumishi wa umma na taasisi za umma ili kuhakikisha mifumo iliyopo na inayojengwa inasaidia kuharakisha utendaji kazi na usimamizi wa watumishi na inakuwa na taarifa sahihi kwa lengo la kuongeza tija na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Alisema mfumo huo mpya ambao ulianza kutumika rasmi Mei 2021, umeunganishwa na mfumo wa PSSSF kwa ajili ya kubadilishana taarifa za michango ya watumishi na nyaraka za hitimisho la ajira, mfumo wa mikopo ya elimu ya juu (HESLB) kwa ajili ya kubadilishana taarifa za mikopo ya elimu ya juu kwa watumishi, mfumo wa ajira portal kwa ajili ya kubadilishana taarifa za waajiriwa wapya na mfumo wa NIDA kwa ajili ya kubadilishana taarifa za utambulisho wa Taifa wa watumishi.
Aliitaja mifumo mingine iliyojengwa kwa lengo la kukabiliana na changamoto za upimaji wautendaji kazi wa watumishi na mikataba ya utendaji kazi ya taasisi kuwa ni mfumo wa kusimamia utendaji kazi wa watumishi wa umma (PEPMIS) na mfumo wa kusimamia utendaji kazi wa Taasisi za Umma (PIPMIS).
āUjenzi wa mifumo hiyo mipya umekamilika. Hivi sasa inafanyiwa majaribio na inatarajiwa kuanzaĀ baada ya kukamilika kwa majaribio na kutoa mafunzo kwa watumishi katika taasisi zote za umma,ā alisema.
Alisema hatua ya mifumo hiyo kuwa ya kielektroniki itaondoa muhali, hisia za kupendeleana au kuoneana katika usimamizi wa utendaji kazi na itahamasisha uwajibikaji wa hiari wa watumishi wa umma itakayosaidia utoaji huduma bora na kwa wakati kwa umma wa watanzania.