RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
JEURI na matumizi mabaya ya majina na nyadhifa za baadhi ya viongozi wakuu wa taasisi, vyombo vya Dola na viongozi wa Serikali iliyoonyeshwa na mfanyabiashara Biao Sun ambaye ni raia wa China anayemiliki duka linalouza mahitaji ya nyumbani (Supermarket) vimeibua mjadala.
Sun ambaye pamoja na mambo mengine, mke wake anadaiwa kuwanyanyasa wafanyakazi wake na kuwatolea maneno machafu, amekuwa akijikinga katika majina ya baadhi ya viongozi wa taasisi nyeti za ulinzi na usalama anaodaiwa kuwa na namba zao za simu.
Kwamba kutokana na malalamiko mengi ya wafanyakazi wake ya kunyanyaswa na kutokewa maneno machafu pamoja na kuwa na makandokando mengi katika biashara yake, anapofikiwa na waandishi wa habari huwa anapiga simu kwa viongozi ama kushtaki kuwa amevamiwa au kuomba wamlinde.
Hilo limedhihirika April 19, 2022 baada ya PANORAMA Blog kufika katika Supermarket ya China Town kwa ajili ya kutafuta ukweli dhidi ya madai ya wafanyakazi kunyanyaswa na kutolewa maneno machafu ambapo Sun alikataa kujibu chochote huku akipiga simu yake ya kiganjani kwa afisa mmoja wa juu wa Kituo cha Polisi Oysterbay kuomba amkingie kifua.
PANORAMA Blog ambayo ilifika eneo hilo ikiwa imeambatana na afisa wa polisi ambaye ni Mratibu wa Usalama wa Kata ya Mikocheni mwenye cheo cha Inspekta kwa ajili ya kufanya mahojiano na Sun ilikutana na wakati mgumu baada ya Sun kukataa kutoa ushirikiano kabla ya kumpigia simu Afisa wa Polisi wa Kituo cha Oysterbay (jina lake limehifadhiwa) kulalamika na kueleza kuwa hayupo tayari kuzungumzia madai ya wafanyakazi wake hao.
Aidha, Sun alikwenda mbali zaidi kwa kumuhoji Mratibu Usalama wa Kata kama yeye ni IGP, (Inspekta Jenerali wa Polisi, waziri au kiongozi wa juu wa Serikali hata kuthubutu kufika dukani kwake kabla ya kuhitimisha kuwa anao uhuru wa kufanya chochote anachoona kinafaa na kwamba wafanyabiashara wenzake katika eneo hilo ambao nao ni raia wa China wanapaswa kuhojiwa kwanza kabla yake kwa sababu nao wana makosa kama aliyonayo yeye.
Baada ya PANORAMA Blog kuripoti habari hiyo, kumekuibuka mjadala kuhusu jeuri iliyoonyeshwa na Sun na imepokea maoni mengi ya watu wanaohoji ni wapi anakopata ujasiri wa kutumia majina na nyadhifa za viongozi wakuu wa taasisi za Dola na hata kufanya na mawasiliano na maafisa wa polisi kwa kuwapigia simu ili kuzuia asihojiwe na vyombo vya habari.
“Sasa huu ndiyo mtindo wake, akiona watu ambao wapo ‘seriuos’ na kazi hawataki bla bla zake basi anapiga simu kwa wakubwa ili wamlinde. Hebu jiulizeni hata nyie ana wasiwasi gani wa kuongea na waandishi wa habari akijibu maswali yao kama hana makando kando huyu? Anaogopa nini? Kwa sababu wanaolalamika ni wafanyakazi wake sasa si unajibu tu kuwa haya madai si ya kweli au ni ya kweli lakini tutayarekebisha. Basi.
“Sasa mtu mnamuuliza maswali yeye anapiga simu kwa wakubwa Oysterbay Polisi, anaficha au anaogopa nini? Na huwa inashangaza sana sijui hizo namba huwa wanampa wakubwa wenyewe au huwa anazitafuta mwenyewe anajenga nao urafiki? Ila tunashukuru Mungu jana mlipoondoka hatukunyanyaswa tena kama inavyokuwaga na ni kwa sababu aliona mpo ‘serious’ na maswali yenu.
“Huwezi kuamini mtu unafanya kazi Supermarket anakuja mama bosi anakwambia ukamtandikie kitanda chake nyumbani na hayo unayoyakuta huko chumbani Mungu ndiyo anajua. Ni afadhali tungekuwa wafanyakazi wa ndani lakini siyo,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa Supermarket hiyo aliyezungumza na PANORAMA Blog jana.
Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Hamza Maneno alidai mbali ya malalamiko ya wafanyakazi, iwapo utafanyika uchunguzi wa mienendo ya raia wa kigeni katika eneo hilo yapo mambo mengi ambayo yatabainika.
“Mimi shughuli zangu ni za hapa hapa ila sifanyi kazi humo kwake, lakini ukifanyika uchunguzi hapa kuna biashara na mambo ya ajabu watayagundua humo. Kama ni mtu mwema ni kwanini anajikinga kwa polisi? Hili eneo hili wakichunguza, wachunguze nani mmiliki wake, ndani humo mbali na hiyo supermarket kuna maduka mengine mengi tu, hebu wachunguze hao wapangaji wanamlipa nani kodi, kuna wachina wana mambo yao humo hebu wachunguze ni mambo gani wanafanyaga humo kama ni kamari au kitu gani?” alisema.
Awali PANORAMA Blog iliripoti kuwa mke wa Sun ambaye pia ni raia wa China hapendi kuitwa jina lake na badala yake anataka aitwe boss na anapotokea mfanyakazi kumuita jina lake humshambulia kwa maneno makali yasiyotamkika.
“Changamoto ni kubwa sana kazini kwetu na tuseme siyo changamoto ni matatizo. Tatizo kubwa lipo kwa bosi mama, yeye kwanza hapendi kuitwa jina lake anataka aitwe bosi. Ukikosea kumuita jina lake unayaoga matusi.
“Mbali na hilo ikitokea wamekuja watu wa Serikali kufanya ukaguzi maana wanakuja kila mara pale kwa sababu kuna maghumashi mengi sana. Sasa wakija huwa kuna mambo tunatakiwa kuyaweka sawa haraka, ikitokea umechelewa yaani bosi mama atakushambulia kwa matusi makubwa makubwa bila kujali wengine ni baba na mama zetu,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao jina lake kapuni.
Katika madai yao mengine, wameleeza kuwa Supermarket hiyo, baadhi ya bidhaa zinazouzwa haziwekewi bei (price tag) kama ulivyo utaratibu wa kawaida na badala yake wateja hukutana na bei ya bidhaa kwenye kaunta ya malipo.
“Kuna bidhaa humu ndani nyingi huwa haziwekewi bei kama ulivyo utaratibu wa kawaida na Supermarket nyingi zinafuata utaratibu huo. Hizo bidhaa hatujui huwa anazitoa wapi tunachojua zinatoka nje ya nchi na wala haijulikana kama zinalipiwa kodi kwa sababu mteja anakutana na bei kaunta na anayotajiwa inatokana kichwani mwa bosi mama.
“Bidhaa zilizoisha muda wa matumizi humu haziondolewi, zinashushwa bei wateja wanauziwa. Hizo ni pamoja na vyakula na bidhaa nyingine za ndani. Sasa wakija watu wa Serikali ni kukimbizana kuweka mambo sawa na ndiyo hapo tunaponyanyasika hasa,” amesema.
Aidha wamedai zaidi kuwa mmiliki wa Supermarket hiyo amekuwa akijenga vyumba vya biashara katika eneo analomiki na kupangisha wafanyabiashara wengine kinyume cha taratibu na inapotokea watu wa Manispaa wanafika kufanya ukaguzi, wakiondoka huanza kuwafokea wafanyakazi wake kwa kutoa siri zake.
“Huyu jamaa ni Mchina kabisa na mkewe ni Mchina lakini hapa ni kwake. Hili ni eneo lake na hivyo vyumba vya biashara vyote unavyoviona yeye ndiyo kavipangisha na analipwa kodi. Kuna baadhi ya watu wa Serikali wanajua hiyo issue hivyo huwa wanakuja kumtingisha anaongea nao.
“Wakiondoka anatugeuzia kibao wafanyakazi anatutukana ile mbaya eti sisi tunatoa siri zake wakati siyo kweli, sisi tumekuja kwake kutafuta mkate wa watoto wetu hayo maghumashi yake hayatuhusu maana hata ukisema umripoti ni kazi bure maana anajuana na watu wengi wakubwa.
“Sasa uvumilivu huwa una mwisho, majuzi katutukana sana mpaka anatutukania wazazi wetu, tumeona bora hili sasa tulisema ili mamlaka za juu waje waangalie na kuchunguza hapa na watusikilize na sisi wafanyakazi kilio chetu,” alisema.