| Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
BAADA ya kutishia Tanzania PANORAMA Blog kuipeleka mahakamani kwa kuibua kidogo ‘madudu’ ya Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), kamati hiyo sasa ikishirikinana na wapambe wake, waandishi wa habari wawili inapanga kujisafisha kwa kutumia vyombo vya habari.
Mkakati wa TOC baada ya kushindwa kujibu maswali na hoja za msingi walizoulizwa na PANORAMA ni kuitisha mkutano waliodai kuwa wa waandishi wote wa habari wenye lengo la kukanusha tuhuma zinazoelekezwa kwao.
Mkutano huo utawahusisha Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi na Makamu Mwenyekiti Henry Tandau, Kamati ya Utendaji pamoja na waandishi wa habari hao wawili na ambao TOC imeeleza kuwa itautumia kujibu maswali ya tuhuma za ufisadi zinazoelekezwa kwa Bayi na TOC.
Tayari Tandau amekwishaeleza kuwepo kwa mkutano huo mkubwa alipokuwa akizungumzia maswali ambayo PANORAMA Blog iliyawasilisha kwa Bayi kwa ajili ya kupatiwa majibu.
Tandau akisaidiwa na waandishi wa habari wawili wapambe wa TOC juzi walitumia nguvu kubwa kupinga madai ya ufisadi yanayoelelezwa kwa Bayi lakini walikataa wao wenyewe, na walimkataza pia Bayi kujibu maswali aliyoulizwa na PANORAMA na badala yake walisema maswali yote yatajibiwa mbele ya mkutano wa waandishi wa habari wote.
Pamoja na mambo.mengine yaliyojiri juzi wakati Tandau akieleze kuwa mzigo wa tuhuma za Bayi utabebwa na yeye pamoja na TOC, aliitaka pia PANORAMA kumfikishia Bayi maswali yote yaliyosalia inayotaka yajibiwe na kwamba yatajibiwa kwa ufasaha katika kikao hicho.
PANORAMA imetekeleza hilo na haya hapa ni maswali ya mwisho iliyoyasilisha kwa Bayi.
Mosi; PANORAMA inaomba kujua utaratibu wa utoaji zabuni unaotumiwa na TOC kwa shughuli zinazodhaminiwa na kutolewa mafungu ya fedha na IOC na je, ni kweli kwamba wewe Filbert Bayi au mtu yoyote wa familia yako mmepata kunufaika na zabuni za TOC au shughuli nyingine za manunuzi ?
Na je ni kweli kwamba kanuni za IOC zinazuia na zinatamka kwamba ni kinyume cha maadili kwa kiongozi wa TOC au familia yake kunufaika na zabuni za IOC au shughuli zake nyingine za manunuzi?
Swali lililofuata linasomeka hivi; PANORAMA inaomba kujua shughuli za TOC zinazofadhiliwa na IOC huwa zinapagwa na nani na je ni kweli kwamba shughuli zote za TOC hufanyika katika Shule ya Filbert Bayi?
Swali la tatu; PANORAMA inaomba kujua kwa undani kuhusu “Olympic Solidarity” na “Athletes Support Funds” ili kutoa ufahamu wa kutosha kwa Watanzania kuhusu mambo hayo na je kuna fedha yoyoye inayotolewa na IOC kusaidia wanariadha wa Tanzania katika maandalizi ya michezo ijayo ya Olimpiki ambayo huhusisha misaada ya ufadhili wa kimasomo yaani (Schorlaships).
Jingine hili hapa; Inadaiwa kuwa IOC inafadhili Shule ya Filbert Bayi kama Kituo cha Olimpafrica, jambo hili lina ukweli kiasi gani na katika hilo inadaiwa iwapo ufadhili huo upo basi shule hiyo inapaswa kuwa mali ya Serikali badala ya mtu binafsi, hili nalo lina ukweli kiasi gani?
Katika maswali hayo lipo pia linalosomeka hivi; Inadaiwa usajili wa Olympafrica hapo shuleni kwako ulifanyika kwa taswira ya rushwa baada ya kiongozi mmoja wa IOC, raia wa Senegali kuja nchini April, 2019 kisirisiri na kukamilisha usajili huo kisiri kisha kuondoka bila hata Serikali kujua. Jambo hili unalizungumziaje kiongozi?
Lingine linasomeka hivi; Inadaiwa kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa IOC ni washirika wa kampuni zako wewe Filbert Bayi, je ni kweli kwamba una ushirika wowote wa kibiashara na kiongozi yoyote wa IOC.
Swali la saba; Inadaiwa kati ya mwaka 2009 hadi 2012, TOC ilipokea Dola za Marekani 680,192 kutoka IOC, wewe kama Katibu Mkuu wa TOC hili unalifahamu? na ni kweli kwamba 2013 hadi 2016 TOC ilipokea Dola za Marekani 523,993 kutoka IOC? na baadaye kati ya 2017 hadi 2020, TOC ilipokea Dola za Marekani 586,132 kutoka IOC, hili nalo lina ukweli wowote?
PANORAMA imemuuliza pia Bayi kuwa; Zipo taarifa kuwa IOC ilitoa ruzuku ya Covid-19 iliyotakiwa kupewa wanariadha kutokana na kuahirishwa kwa michezo ya Olimpiki ya Tokyo Japan, fedha hizi zilipokelewa na TOC? na je wanariadha walipewa kama ilivyokusudiwa na IOC?
Na mwisho PANORAMA Blog imemuuliza Bayi kuwa Baadhi ya vyombo vya habari vinadaiwa kuripoti taarifa kuwa Januari 20, 2022 wewe Filbert Bayi na baadhi ya viongozi wenzako katika TOC mliteuliwa katika ANOCA, Taarifa hizi za kuteuliwa kwenu zilikuwa za kweli?






