Wednesday, June 25, 2025
spot_img

WAFANYAKAZI KIWANDA CHA NONDO WAPANGA MAANDAMANO

 

Ofis za Kiwanda cha Nondo cha Hong Yu Steels

NA RIPOTA PANORAMA

WAFANYAKAZI  wa kiwanda cha kutengeneza Nondo cha Hong Yu Steels (T) Co LTD, kilichopo ukanda wa viwanda Misugusugu, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani wanakusudia kuandamana kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu kupeleka malalamiko na taarifa walizonazo kuhusu kiwanda hicho.

Wakizungumza na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni nje ya ofisi za kiwanda hicho, wafanyakazi hao walisema maandamano yao yatahusisha baadhi ya wafanyakazi ambao watasafiri kutoka Mkoa wa Pwani kwenda Dodoma kwa ajili ya kuandamana.

Walisema wakiwa Dodoma watatembea kwa amani kutoka eneo la Nyerere Square hadi Ofisi ya Waziri Mkuu ambako watatoa mabango yenye malalamiko yao na pia taarifa walizonazo kuhusu kiwanda hicho.

Kiongozi wa wafanyakazi hao (jina tunalihifadhi) aliiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa malalamiko wanayokusudia kuyawasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu ni mazingira yenye uchafu uliokithiri unaohatarisha afya za wafanyakazi ndani ya kiwanda hicho na kutopewa mikataba ya ajira licha ya kufanya kazi kiwandani hapo kwa kipindi kirefu.

Alisema uamuzi wao wa kuandamana unatokana na watendaji waliopewa dhamana na Serikali kusimamia mwenendo wa viwanda nchini ili kuhahakisha vinatoa haki kwa wafanyakazi na vinafuata sheria za uendeshaji viwanda, kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Kwanza tunawashukuru sana waandishi kwa uamuzi wenu wa kufanya ziara ya kujionea jinsi viwanda hivi vinavyoendesha shughuli zake. Asanteni sana na tunaamini mmeona mengi. Kwetu sisi ni kama mlivyoona mazingira yetu ya kazi ni machafu mno, hapa watu wanaugua kila siku na tunafukuzwa kazi kienyeji tu.

“Hiki ni kiwanda cha nondo, kuna tanuru la kuyeyusha nondo ambalo moto wake ni mkali sana lakini wafanyakazi hatuna vifaa maalumu tunavyopaswa kuvaa kwenye kazi hii, tuna miaka mingi tu kazini lakini hatuna mikataba ya kazi hivyo hatuna mishahara, hatupimwi afya zetu, hatuna pensheni. Yaani pamoja na kufanya kazi hii ngumu na ya hatari, mwisho wetu ni mbaya.

“Huyu bosi alichofanya ni kutugawa, baadhi yetu kawapa mikataba na wakija watu wa Serikali ndiyo anatumia mikataba hiyo kusema ametoa ajira lakini tupo wengi tu hatuna mikataba. Na kutokana na mazingiira ya kufanya kazi kwenye moto mkali tunapaswa kunywa maziwa lakini hatupewi isipokuwa wale wa jikoni kwenye uyeyushaji. Yaani katugawa hivyo tunaumizana wenyewe kwa wenyewe. 

“Watendaji wa chini wa eneo hili wameshindwa kutusaidia sasa tumeona twende Ofisi ya Waziri Mkuu, tunajua tukifika ofisini kwake atapata taarifa zetu na kwa tunavyomjua kiongozi wetu akisikia habari zetu atakuja yeye mwenyewe kujionea hali ilivyo au atatuma watu wake. Sisi tutawapa kila kitu kama watatumwa kuja kufanya uchunguzi. Hata kama tutafukuzwa lakini tutakuwa tumewaokoa wengine watakaokuja kufanya kazi hapa,” alisema. 

Alipoulizwa mbali na malalamiko yao ya kufanya kazi kwenye mazingira machafu na kukiukwa kwa sheria za ajira, mambo mengine yanayohusu kiwanda hicho wanayokusudia kuyafikisha kwa Waziri Mkuu ni yapi alisema yatafahamika siku ya maandamano ambapo waandishi wataalikwa.

“Tutawaita waandishi kwenye maandamano yetu kwa sababu tunataka watanzania wote wajue kinachoendelea kwenye kiwanda hiki, tumekubaliana hayo mambo mengine tutayatoa hapo hapo ofisini kwa Waziri Mkuu,” alisema. 

Alipoulizwa kuhusu kibali cha kufanya maandsmano hayo na iwapo kabla ya kufikia hatua hiyo wamekwishafikisha malalamiko yao kwa viongozi wa Wilaya na Mkoa alisema malalamiko yao ni ya muda mrefu lakini hayafanyiwi kazi.

“Tutafuata taratibu zote, tutatembea tu kwa amani tukifika kwa Waziri Mkuu tutatoa ujumbe wetu halafu tutaondoka. Sisi siyo wanasiasa kwamba tutaleta fujo hapana, sisi tunapeleka malalamiko na taarifa zetu kwa kiongozi wetu tunayemuamini,” alisema.

Alipoulizwa Meneja Rasilimali wa Watu (HR) kiwanda hicho, Jumanne Mwegelo kuhusu malalamiko ya wafanyakazi hao alisema hawezi kuyazungumzia bali kama vyombo vya habari vitaamua kuyafanyia kazi viongozi wake ndiyo watakaoshughulika.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya