Monday, June 23, 2025
spot_img

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWATUMIA SALAMU ZA ONYO WAHUJUMU USHIRIKA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa


NA MWANDISHI MAALUMU – OFISI YA WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa vyama vya ushirika wabadilike na wawe weledi ili warejesha heshima ya ushirika nchini.

Akizungumza jana katika ukumbi wa mikutano wa Hazina jijini Dodoma na wakuu wa mikoa sita, makatibu wakuu, Mrajisi wa Ushirika Taifa, warajisi wasaidizi wa mikoa,  Menejimenti ya Tume ya Ushirika,  wajumbe wa Bodi za NCU (1984) Ltd, KNCU (1984) Ltd, SHIRECU na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mkonge, Waziri Mkuu Majaliwa alisema viongozi wa vyama vya ushirika wanapaswa kubadilika kwa sababu wamepewa dhamana ya kuwasaidia Watanzania wanyonge.

“Viongozi wa ushirika ni lazima tubadilike. Nyie mliopewa dhamana kwenye vyama vikuu hivi vitatu vya KNCU, NYANZA na SHIRECU lazima mbadilike. Nyie mmepewa dhamana ya kuwasaidia Watanzania wenzetu wanyonge wanaolima ekari moja, mbili au tatu,” alisema.

Katika mkutano huo maalumu ambao Waziri Mkuu Majaliwa alipokea taarifa ya ufuatiliaji wa mwenendo wa vyama vya ushirika vya NCU (1984) Ltd, KNCU (1984) Ltd na SHIRECU (1984) Ltd kutoka kwa timu maalumu ya uchunguzi , alisema viongozi wa ushirika bado hawajabadilika kwa sababu hata kazi ya usambazaji mbolea kwa wakulima bado ni changamoto.

Uwasilishwaji wa taarifa hiyo ulishuhudiwa na Wakuu wa Mikoa ya Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Tanga, Geita na Simiyu. Pia Makatibu Wakuu wa Wizara za Fedha, Ardhi, Kilimo, Viwanda na Biashara.

Wengine walioshuhudia ni Mrajisi wa Ushirika Taifa, Warajisi Wasaidizi wa Mikoa, Menejimenti ya Tume ya Ushirika, Wajumbe wa Bodi za KNCU, NYANZA na SHIRECU na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania.

“Ninasema viongozi bado hatujabadilika kwa sababu hata suala la usambazaji wa mbegu kwa wakulima ni changamoto. Wengine wamekuja kujifunza ushirika hapa nchini na wamesonga mbele lakini sisi hatuendi mbali kwa sababu ya kukosa weledi, uaminifu na uwajibikaji katika majukumu tuliyowakabidhi.

“Nendeni mkasimamie ushirika ili heshima ya ushirika wa zamani irejee, hali ya ushirika ule ambao uliacha mali za ushirika. Bado kazi hizo mali haijakamilika. Tunataka tuzisimamie na tuwakabidhi kitu ambacho kimekamilika,” alisema.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa alisema anasikitika kuona makosa ya ushirika yanafanyika wakati warajisi wasaidizi wapo na hata kwenye halmashauri kuna maafisa ushirika.

“Haya madudu yanafanyika lakini warajisi wa mikoa mpo na nyie ndiyo wasimamizi wa ushirika. Je mnafanya nini?”

“Lazima uhakikishe vyama vya msingi vinasimamiwa na vinakwenda kama ambavyo sheria yetu ya ushirika inasema. Warajisi wasaidizi wapo kila mkoa na kila wilaya kuna afisa ushirika. Ni kwa nini mambo hayaendi?

“Hatutasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu anayehujumu mali za ushirika. Tulianza na tutaendelea kusimamia mali za ushirika,” alisema.

Mapema, akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa, kiongozi wa timu hiyo maalumu, Asangye Bangu alisema imefanikiwa kurejesha mali 60 za ushirika zenye thamani ya sh. bilioni 68.98.

“Mali hizo zinajumuisha majengo, viwanja, magari na mitambo ya mashine, hazikuwa mikononi mwa vyama hivi vitatu lakini sasa zimerudishwa kwenye vyama,” alisema Bangu.

Alisema kati ya hizo, NYANZA ilikuwa na mali 37 zenye thamani ya sh. bilioni 61.36, SHIRECU ilikuwa na mali saba zenye thamani ya sh. bilioni 3.33, KNCU ilikuwa na mali 10 zenye thamani ya sh. bilioni 2.03 na TCCCo ilikuwa na mali sita zenye thamani ya sh. bilioni 2.2.

Bangu alikabidhi taarifa hiyo ikiwa na mapendekezo kadhaa kwa serikali.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya