MWANDISHI MAALUMU, ARUMERU
FURAHA ilipotea ya wananchi wa Kijiji cha Manyire, Kata ya Mlangarini, Halmashauri ya Arusha baada ya kunyang’anywa ardhi yao na mtu aliyefahamika kwa jina moja la William, mapema wiki hii ilirejea upya baada ya Serikali ya Wilaya ya Arumeru kuwarejea ardhi hiyo.
Shangwe zilizoambatana na vigelegele vya akina mama ziliibuka katika eneo ulipokuwa ukifanyika mkutano wa kutatua mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa kijiji hicho na William baada ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro kutangaza kuwa ardhi iliyokuwa imetwaliwa na Wiliam kutoka kwa wananchi hao imerejeshwa rasmi kwao na Serikali.
Katika mkutano huo uliofanyika mapema wiki hii kijiji hapo, William alitakiwa na Muro kuwasilisha nyaraka zake zote zilizokuwa zikimpa uhalali wa umiliki wa ardhi hiyo lakini baada kukaguliwa na wataalamu wa ardhi wa Serikali ilibainika kuwa hakukuwa na nyaraka yoyote kati ya alizowasilisha iliyokuwa ikimpa uhalali huo.
“Nimekuja hapa ili tumalize hili tatizo lililodumu kwa miaka mingi! Hii ni Serikali makini na Rais John Pombe Magufuli, ametutuma tuje tusikilize kero zenu wananchi.
” Nimekuja, nimekagua, nimezunguka eneo ambalo kuna mgogoro wa ardhi uliosababisha nyumba kuchomwa moto. Tumeangalia vielelezo na nyaraka zote za maeneo ambayo Mzee William anasema ni mali yake.
“Hakuna nyaraka hata moja imethibitisha maeneo hayo ni mali ya Mzee William. Jinsi alivyopata hana vielelezo na hana nyaraka yoyote inayosema maeneo hayo ni mali yake.
” Hivyo Serikali imejiridhisha na tunatamka maeneo yale ambayo wananchi walinyang’anywa na Mzee William tumewarudishia,” alisema Muro.
Kutolewa kwa kauli hiyo kuliibua shangwe kutoka kwa wananchi na baadhi yao waliishukuru Serikali ya wilaya kwa kuumaliza mgogoro huo uliokuwa ukihatarisha amani katika Kijiji cha Manyire.
Muro alifika kijijini hapo mapema wiki hii akiwa amefuatana na baadhi ya wataalamu wa ardhi kukagua uharibifu uliotokea kwenye nyumba iliyochomwa moto kwa sababu ya mgogoro wa ardhi.
Akiwa kijijini hapo, Muro alifanya kikao na wananchi pamoja na boma la Mzee William ambapo watalaamu wa ardhi walipitia upya vielelezo vya umiliki wa ardhi vya kila upande na kubaini upungufu mkubwa katika nyaraka za William.