LONDON, Uingereza
SIMANZI nzito imetawala katika ulimwengu wa soka baada ya taarifa za kifo cha mlinda mlango wa zamani wa klabu za Liverpool na Arsenal, Alex Manninger.
Manninger (48), alifariki jana Aprili 16, 2026 baada ya gari lake kugongwa na treni mjini Salzburg, Austria. Kipa huyo alicheza Liverpool msimu wa 2016-17.
Kwa upande mwingine, kipa huyo anaingia kwenye orodha ndefu ya wanasoka waliopoteza maisha katika matukio ya ajali za gari.
DIOGO JOTA
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool alipata ajali ya gari iliyohitimisha maisha yake Julai 3, 2025. Ajali hiyo ilimuua pia kaka yake, Andre Silva, aliyekuwa kwenye gari hilo.
JOSE ANTONIO REYES
Mmoja ya viungo bora wa pembeni kuwahi kucheza Arsenal, pia akiitumikia kwa nyakati tofauti klabu za Real Madrid na Sevilla.
Reyes raia wa Hispania, alifariki kwa ajali ya gari iliyotokea Juni, 2019, wakati huo akiwa na umri wa miaka 35.
FREDDY RINCON
Ni kiungo wa zamani wa timu ya Taifa ya Colombia, pia akiwahi kuzitumikia klabu za Real Madrid na Corinthians ya Brazil.
Kama itakumbukwa, Rincon alifariki kwa ajali ya gari Aprili, 2022. Kifo chake kiliitikisa Colombia, ikifahamika kuwa alikuwa na heshima kubwa katika soka la nchi hiyo.
JUANITO
Jina lake kamili ni Juan Gomez Gonzalez na ni moja ya nembo za vigogo wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), Real Madrid.
Alifariki kwa ajali ya gari mwaka 1992, wakati huo akiwa na umri wa miaka 37 na ameshastaafu kucheza soka.
LAURIE CUNNINGHAM
Winga huyo ni miongoni mwa nyota wa kwanza wenye ngozi nyeusi kucheza timu ya Taifa ya England.
Alicheza Real Madrid na Manchester United, kabla ya ajali ya gari kukatikisha uhai wake Julai, 1989, wakati huo akiwa na umri wa miaka 33 tu.
ROMMEL FERNANDEZ
Straika wa zamani wa timu ya Taifa ya Panama, ambaye aliwahi kutamba La Liga akiwa na Valencia na Albacete.
Ajali ya gari ilikatiza uhai wake Mei, 1993. Alifariki akiwa na umri wa miaka 27 tu lakini alishajenga jina kubwa katika soka la Panama.
PETER HOUSEMAN
Straika raia wa England, ambaye aliwahi kucheza Ligi Kuu nchini humo akiwa na vigogo wa Magharibi mwa London, Chelsea.
Houseman alifariki kwa ajali ya gari mwaka 1977, taarifa iliyoacha simanzi kubwa kwa mashabiki na viongozi wa klabu hiyo.
HERALDO BEZERRA
Wachambuzi wa soka huko Brazil wanamtaja kuwa ni moja ya vipaji vikubwa kuwahi kutokea katika soka la Brazil miaka ya 1970.
Bezerra aliyewahi kucheza La Liga akiwa na Atletico Madrid, aliondoka katika uso wa dunia mwaka 1977, chanzo kikiwa ni ajali mbaya ya gari.






