MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Allan Okello, amethibitisha kuwa Yanga haikufanya makosa kumsajili wakati wa dirisha dogo lililopita.
Okello alisajiliwa Januari, 2026, wakati wa usajili wa dirisha dogo, akitokea Ligi Kuu ya Uganda alikokuwa akiitumikia Vipers.
Licha ya kusuasua katika siku zake za mwanzo, hata baadhi ya mashabiki kubeza uwezo wake, nyota huyo ameamka na kuonesha makali yake katika mechi za Ligi Kuu Bara alizocheza hivi karibuni.
Iko hivi; katika michezo mitatu ya Ligi iliyopita, Okello, ambaye pia ni tegemeo kwenye timu yake ya Taifa ya Uganda ‘The Crane’, ametoa pasi za mabao (asisti) sita.
Aprili 4, 2026, katika mchezo dhidi ya Prisons, Yanga ilishinda mabao 3-0, huku Okello akifunga dakika ya 50 na kutoa asisti kwa Mudathir Yahya (dk. 68).
Aprili 8, 2026, wakati Yanga ilipoifunga Pamba Jiji mabao 3-0, alitoa asisti kwa wafungaji wote; Mudathir (dk. 9 na dk. 34) na Maxi Nzengeli (dk. 68).
Aprili 16, 2026, Okello alipiga asisti kwa Ngezeli (dk. 6) na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (dk. 45) wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 6-0.
Huyo ndiye Okello ‘Star Boy’, akitajwa kuwa miongoni mwa vipaji vikubwa katika soka la Uganda kwa sasa.






