LONDON, Uingereza
ARSENAL wako kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL) lakini ni pointi sita pekee zinazoitenganisha na Manchester City inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo.
Wakati Arsenal wakiwa wamebakiza mechi tano, Man City wana sita na keshokutwa Aprili 19, 2026, timu hizo zitakutana Etihad, mchezo unaotarajiwa kutoa picha halisi ya mbio za ubingwa.
Arsenal walikuwa na nafasi ya kuongeza pengo la pointi endapo wangeifunga Bournemouth katika mchezo uliopita lakini walitandikwa mabao 2-1 wakiwa Emirates.
Je, Washika Bunduki wataifunga Man City, ambayo imefungwa mechi moja pekee kati ya 19 za EPL ilizocheza hivi karibuni?
Timu hizo zilipokutana katika mechi ya kwanza msimu huu wa EPL, zilimaliza dakika 90 kwa sare ya bao 1-1 pale Emirates.
MECHI ZILIZOBAKI
Baada ya kumalizana na Man City ya Pep Guardiola, Arsenal itakuwa na mechi tatu za nyumbani (Newcastle, Fulham na Burnley) na mbili za ugenini (West Ham na Crystal Palace).
Kwa upande wao, Man City watabaki na tatu za nyumbani (Brentford, Aston Villa na Crystal Palace) na tatu za ugenini (Burnley, Everton na Bournemouth).
VIPI ENDAPO ZITALINGANA POINTI?
Kanuni zinasema kigezo cha kwanza cha kupata bingwa wa EPL ni idadi ya pointi. Kama zitalingana kati ya timu mbili za juu, basi itaangaliwa tofauti ya mabao ya kufungwa na kufungwa (Goal difference).
Endapo bado zitalingana, basi timu iliyokusanya pointi nyingi baada ya timu hizo kukutana mara mbili (nyumbani na ugenini), ndiyo itakayopewa taji.
Ikiwa napo zitalingana, basi timu iliyofunga mabao mengi ugenini dhidi ya mwenzake ndiyo itakayopewa ubingwa.
Endapo zinalingana kila eneo, kama ilivyoelezwa hapo juu, basi hakutakuwa na namna zaidi ya bingwa kutafutwa kwa ‘play-off’ itakayochezwa katika uwanja usio wa timu ‘A’ wala ‘B’.
Imeandaliwa na Hassan Mwasha






