Mkuu wa Wilaya amepokea ujio wa timu maalum ya wataalamu wa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), waliotoka katika mikoa ya Kigoma, Tanga na Dar es Salaam, kwa lengo la kuboresha ukusanyaji wa mapato na mifumo ya kodi katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mkuu wa Wilaya amesema ujio wa timu hiyo ni fursa muhimu kwa wilaya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kufanya tathmini ya mifumo pamoja na vyanzo vya mapato vinavyotokana na walipakodi.
Ameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi na kuimarisha usimamizi wa mapato kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa.
Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wataalamu kutoka maeneo mbalimbali, akibainisha kuwa utaongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuboresha mifumo ya kodi nchini.
Aidha, amewataka wananchi na walipakodi kushirikiana kikamilifu na timu hiyo, hasa katika kupata elimu ya kodi na kubaini changamoto zilizopo ili zipatiwe ufumbuzi. Ameongeza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na uelewa sahihi wa wajibu wake wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wa wafanyabiashara, Mkuu wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa kuzingatia taratibu zilizowekwa katika maeneo ya biashara. Amewataka wanaofanyia shughuli zao katika maeneo maalum kufuata miongozo iliyopo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hawauzi bidhaa nje ya maeneo yaliyotengwa bali wanatumia sehemu rasmi zilizopangwa.
Akihitimisha, Mkuu wa Wilaya amewahimiza wananchi kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa timu hiyo katika kipindi chote cha wiki moja watakachokuwepo wilayani hapo, huku akisisitiza kuwa ulinzi na mazingira rafiki yatahakikishwa ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi.






